HII SAFARI YA WOTE

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi ambapo uchaguzi katuni nne zenye maudhui mbalimbali hufanyika, kisha kuelezewa na tamati kufanyiwa uchambuzi huo .

Kwa kuyaanza makala haya siku ya leo Mwanakwetu amekamata katuni inayowaonesha jamaa wawili –mwanamke na mwanaume wamefika kijijini katika nyumba moja ya mafukara mno, jamaa hawa wawili waliovaa nadhifu wanasema- tumekuja kufanya utafiti- mama mmoja mlemavu katika makazi haya anasema baba tumechoswa na tafiti zenu zisizoisha, baba mwingine mmoja ambaye nadhani ni mume wa huyu mama mlemavu anasema tupeni kwanza fedha, kwa chonjo jamaa wengine kijijini wanakimbia ugeni huu, wakisema hawa ni wafanyabishara wa ngozi za binadamu? Jamaa kando anajibu hawa na wenyewe ni wasaka tonge tu hawana lolote .

Kwa hakika katuni hii inabainisha uhalisia wa mambo, hasa kile kinachoelezwa mitaa/vijiji dhidi ya tafiti mbalimbali na hilo linasababisha jamii nayo kusaka fedha maana jamii haioni tija ya tafiti hizo. Kikubwa tafiti zinapofanya  zina manufaa kwa jamii, lakini tafiti zikikamilika ni vizuri kutumiwa na siyo kubaki maofisini na katika maktaba zetu tu.

Sasa Mwanakwetu anaikamata katuni ya pili ambayo inaonesha jamaa mmoja amebeba sahani yenye chakula anampelekea  jamaa ambaye yu hoi bini taabani hadi kusimama hawezi, Jamaa ameketi chini , Mwanakwetu njaa mbaya. Ndiyo maana waswahili wanasema adui yako muombee njaa tu.  

Huyu jamaa aliyeketi chini kapewa jina Kenya, nyuma ya huyu jamaa kuna jamaa mwingine kapewa jina Tanzania (TZ)huku akipiga miayo na mtoto wake kando anamwamba  angalia mwenzetu Kenya anapewa chakula, Baba na mtoto umelo wa chakula anachopewa jirani unamjia, njaa inazidi pale unapomuona mwenzako kapewa msosi, jamaa huyu mwenye kubeba chakula anawananga anasema pokea huu msaada utapoza njaa maana miayo haina adabu .

Kikubwa katuni hii inadokeza kuwa mataifa mengi ya Afrika hayawezi kufanya lolote bila ya kutegemea misaada kutoka ng’ambo na huo ndiyo ukweli swali ni je wanaotusaidia na wao watasaidiwa na nani mambo yakiharibika? Kwa makala haya Afrika tunawajibu wa kutoka katika utegemezi ili tuweze kuendesha mambo yetu wenyewe kwa kidogo kidogo maana sasa ni miaka mingi tangu afrika ipande uhuru.


 

Sasa nakutana na katuni ya tatu ambayo imechorwa Novemba 1, 2020 ikionesha hali ya taifa letu baada ya uchaguzi wa wa Oktoba 25, 2020 kukiwa na mabalaa mengi hasa ukiukwaji wa haki za binadamu  huku katuni hi ikionesa askari kilakona naye kiongozi mwenye wajihi wa Rais John Magufuli akiwa ameshika Biblia kama anakula kiapo lakini miguu yake imeyakanyaga mabalaa hayo, kando akionekana jaji akisimamia kiapo hicho huku akiyakodolea tu mabalaa hayo miguun kwa huyu anayekula kiapo. Kwa hakika katuni hii inamkumbusha kila mtazamaji wake kuwa mwaka 2024 na 2025 kuna chaguzi, hivyo kila mmoja wetu awe makini kuhakisha wapiga kura wanashirki zoezii hili kwa uhuru na haki bila uonevu wowote ule, katuni hii inakumbusha uadilifu kwa wapiga kura , viongozi na wale wanaosimamia chaguzi hizo.

Sasa ninakutana na katuni ya nne ambayo imechorwa na Said Michael wa Shirika la Utangazaji Ujerumani, katuni hii inamuonesha mama mmoja ambaye amevalia suti yake kama nyeusi na hijabu kama nyekundu akisema hali hii haivumiliki naagiza kufanyike uchunguzi mara moja, kando kuna ubao una maneno matatu- hatari utekaji,utesaji na mauwaji , nao upande wa pili kuna ubao wenye maneno hayo hayo alafu kuna jamaa aliyevalia kama Polisi anasema-hali ya usalama ni shwari.

Katuni hii inaeleza hali ya usalama nchini Tanzania mara baada ya kutekwa na kuuwawa kwa Ally Mohammed Kibao ambaye alikuwa kiongozi wa CHADEMA, katuni hii inaonesha wajihi wa Rais Samia Sulhu Hassan na kauliza za viongozi akiwamo pia Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Afande Camilius Wambura.  Katuni hii imemkumbusha Mwanakwetu tukio la kupotea kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya marehemu Robert Ouko Febuari mwaka 1990 katika taifa a Kenya na baadaye kiongozi huyu mwili wake kuokotwa machakani ukiwa umechomwa kwa moto enzi za utawala wa Rais Daniel Arap Moi.


 

Mwanakwetu kwa makala haya akiwa na masikitiko na kifo cha mzee Ally Mohammed Kibao anabainisha kuwa kwa mauwaji yenye mlengo wa kisiasa au vyovyote vile hakuna binadamu mwenye haki ya kuupoteza uhai wa binadamu mwenzeke kama wa mnyama . Lazima serikali na vyombo vyake vilivyokadhiwa jukumu la ulinzi na usalama vitimize wajibu wao.

Tukio la kifo cha Robert Ouko nchini Kenya mengi yaliongewa lakini hata kama Robert Ouko aliuwawa na hata kama wengi wao waliotuhumiwa ,Ukweli ni kwamba wamemfuata marehmu Ouko, iwe kwa kifo cha magonjwa au kifo cha kawaida , kifo ni safari ya wote.


 

 


Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Kifo ni Safari ya Wote .”

Nakutakia siku njema/

makwadeladius@gmail com

0717649257

NB Makala ya Sauti na ya Youtube yanaambatana na sehemu ya tukio la kifo cha marehemu Robert Ouko mwaka 1990 na matukio yaliyofuata baadaye nchini Kenya.


 

 







 

0/Post a Comment/Comments