Adeladius Makwega-MBAGALA
Msomaji wangu huu ni wakati mwingine wa kukukaribisha tena kwa heshima na taadhima tele katika makala ya katuni, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi yenye katuni nne zilizoteuliwa na mtayarishaji wa makala yetu, zinaelezewa kisha kufanyiwa uchambuzi.
Kuyaanza makala haya Mwanakwetu ameikamata katuni ambayo imechorwa na ndugu yetu Said Michael ambapo Mwanakwetu humuita Saidiwamikaeli, hapa kunaonekana vikaragosi sita ambapo zinaonekaa sura zao, sura hizo sita kuna wanaume watano na mwanamke mmoja, kati ya sura hizo sita sura nne zimepachikwa miwani na sura mbili za mwanzo hazina miwani . Juu ya vikaragosi hivyo kuna maneno haya –Katuni inasema Waache Wachore –Sanaa na Maisha. Mwanakwetu ninasema NAAAAM Katuni Inasema Waache Wachore.
Ukiitazama katuni hii hawa jamaa wanafanana na marais sita; watano waliyoiongoza Tanzania zamani yaani Mwl Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete, Magufuli na pia Rais wa sasa Bi Samia Suluhu Hassan na yeye yumo , na yeye yumo.
Mwanakwetu anapoitazama katuni hii inatoa ishara kuwa kila mmoja ya viongozi hao kapokea madaraka kutoka mwenziwe na yeye Rais Samia wakati wake ukifika atakabidhi madaraka hayo kwa ajaye. Mwanakwetu anamwambia Rais Samia ajitahidi mno kuongeza nguvu na jitihada katika kutilia maana majambo na mashida ya watu na kuyafanyia kazi kwa spidi mitaani maneno ni mengi pia Rais Samia anapaswa kuwa mwanafunzi hodari kujifunza toka kwa viongozi hao katika katuni waliyomtangulia hasa kwa mambo makubwa mawili tu; kwanza kama walikwama wapi na kwanini na kama walifanikiwa wapi na kwanini;
“Kwa maana kama Rais Samia sasa unalima shamba, mama yetu, shamba lako lilishapasuliwa msitu na kung’olewa visiki, jukumu lako ni kukodi trekta na kuyaondoa magugu na kuendelea na kilimo.”
Mwanakwetu nakwambia msomaji wangu- Jukumu Rais Samia Kukodi Trekta na Kuendelea na Kilimo.
Sasa nakutana na katuni ya pili ambayo inaonesha mandhari ya maandamano ambapo kunaonekana gari linalobeba maji ya kuwasha, pia kunaonekana jamaa kama polisi akiwa amewakamata wana habari, je na wao walikuwa wanaandamano? Jamani wanahabari hawa wapo katika majukumu yao kuripoti maandamano,hapo hapo yanasikika maneno haya- kosa langu afande nini? Afande anajibu kosa lako ni kufikisha ujumbe. Hapa afande huyu mwenye ubavu kamkamata mwandamanaji na kamkamata mwanahabari, kwa hakika katika varangati kama hili lazima kamera, tepu rekoda, simu na vifaa vingine vya kihabari vipotee, viharibike au kuchukuliwa na kuvipata inakuwa msiba, hivyo vifaa ni gharama.
Ukiitazama katuni hii kwa kina inaonesha kuwa afande huyo haioni thamani ya wanahabari katika maandamano ambalo hilo ni kosa kubwa kwa afande huyu aliyechora na saidiwa mikaeli. Kwa hakika na kwa taratibu za kuendesha nchi wapo wafanya maamuzi wengi ambao hawawezi kuwapo katika maandamano lakini taarifa za maandano watazipata kupitia Jeshi la Polisi Tanzania na kuziona kupitia vyombo vya habari. Hata katika maandamano ya amani wapo polisi na raia wanaoweza kuumia hata kujikwaa na kukanyagwa na wenzi wao maandamanoni ndiyo maana maandamno mengi Msalaba Mwekundu na matabibu wanaojitambua lazima wawepo.Vyombo vya habari visitazamwe kama adui bali ni ndugu na hata hao hao polisi na nyinyi ndugu zetu kama walivyo waandamanaji. Kikubwa hata kama vyombo vya habari vikapata changamoto na kuzuiwa, hivi sasa ulimwengu una tekinolojia ya satalite ambapo aliye mbali anaweza kuona kila kinachoendelea umbali mrefu na yeye alipo kikubwa kuishi kidugu ili kila mmoja wetu awe salama na ayafikie malengo yake na familia yake.
Mwanakwetu anakutana na katuni ya tatu ambayo inaonesha magari mawili moja la maji ya kuwasha la polisi na lingine imepewa jina serikali ambalo haliwaki bali linakwenda kwa kusukumwa na waandamanaji,hawa waandamanaji wamebeba mabango yenye maneno kadhaa-Tunataka ulinzi wa raia na mali zetu , bango lingine linanadi Tunaitaka haki ya kuishi. Hapa cha kusikitisha gari la maji yakuwasha linawarushia waandamanaji maji hayo kupitia juu ya gari la serikali. Kando yake kuna maneno, nguvu inayotumika kututawaya ingetumika kutulinda.
Kwa hakika msomaji wangu katuni hii inajieleza vizuri kama ilivyochorwa na saidiwa mikaeli ambaye katuni zake zinatumiwa na Shirika la Utangazaji la Ujerumani(DW), Kikubwa serikali itimize wajibu wako maana kinacholalamikiwa ni haki ya kuishi kama ilivyoonekana katika kutekwa na kuuwawa kwa mwanasias wa CHADEMA Ally Mohammed Kibao huku tukio hilo limechorwa vizuri katika katuni ya nne ambayo inaonesha namna ndugu huyu alivyotekwa na maagizo ya viongozi wa serikali baada ya kadhia hii, katuni hii imechorwa na saidiwamikaeli
.
Kwa hakika msomaji wangu Mwanakwetu bado anakumbuka mauwaji ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya marehemu Robert Ouko yalitokea Februari 1990 ambapo baada ya tukio hilo yaliibuka mengi ikiwamo baadhi ya watumishi wa umma na vyombo vya ulinzi kukimbia taifa hilo akiwamo mwanasiasa wa sasa wa Kenya ambaye anaonekana kama Kituko anayezungumzia Kenya kuruhusu bangi kutumiwa, Prof. George Luchiri Wajackoya
“Huyu jamaa alisajiliwa kwa mafunzo ya polisi katika chuo cha polisi cha Kiganjo. Alifanya kazi kama afisa wa polisi hadi akafikia ngazi ya inspector. Alipewa majukumu ya kukusanya Ushahidi kuhusiana na kifo cha aliyekuwa waziri wa mambo ya Kigeni wa Kenya Robert Ouko. Mambo yalimgeukia kutokana na Ushahidi aliokuwa anakusanya na akakamatwa, maana alirekodi sauti ya mazungumzo ya simu baina Rais Moi na waziri wake , sauti hii ilisikika Rais Moi akimlaumu waziri huyo kushiriki tukio hilo. Kwa hiyo Prof. George Luchiri Wajackoya alikamatwa na akawekwa kizuizini bila kufikishwa mahakamani na kuteswa mno lakini baadaye kuna raia wa Marekani na Kenya walimsaidia na kutoroka kizuizini. ”
Mwanakwetu upo?
Kw hakika makala haya siku ya leo yamejengwa na katuni nne ile ya marais wa Tanzania, ya pili ni ya maandamano na polisi kuwakamata hadi wanahabari, ya tatu ni ya maandamano pia na ya yale magari mawili na katuni ya mwisho ni hii la tukio a kutekwa na kuuwawa kwa Ally Mohammed Kibao ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa CHADEMA.
Kumbuka,
“Jukumu la Rais Samia Kukodi Trekta na Kuendelea na Kilimo”
Watu walishapasua msitu ; Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail. Com
0717649257
NB-Makala haya ya sauti na youtube yanamalizia tukio la mauwaji ya Dkt Robert Ouko ya mwaka 1990 yalimuibua Profesa George Luchiri Wajackoya
Post a Comment