KONDOO MWENYE MANYOYA TELE


Adeladius Makwega-MWANZA

Msomaji wangu siku ya leo nakuomba niambatane na wewe tena katika suala la usalama wa raia hasa kuhusiana na matukio ambayo yanadaiwa kutokea katika jamii ya Tanzania kwa nyakati tofauti ambapo hata Jeshi la Polisi Tanzania linatoa ripoti juu ya visa hivyo vya kutekwa, kuumizwa, kupotea na kufariki kwa kuuwawa kwa watu kadhaa kwa sababu tele.

Kwa hakika kuna walio wengi hasa wenye nafasi ukiwatazama, ukiwapima na kuwatathimini unaweza kuona kama wanadhani kuwa suala la usalama wa raia ni suala la watu chini, watu wasio na nafasi , ni jambo watu makabwela , watu wasio na nguvu, watu wanyonge na watu wasio na mamlaka hilo Mwanakwetu anakwambia msomaji wake ni abadani. Huu mtazamo siyo sahihi, kama yupo anayedhani hivyo anatakiwa kufuta mara moja hilo wazo na tena hasa hasa wanasiasa wa Tanzania.

Sasa ngoja nikuume sikio msomaji wangu,

“Mara zote katika siasa hamuwezi kuelewana kila kitu, kama kila mmoja ana nia ya kuisadia jamii, mpendane 100 kwa 100 hapo haiwezekani, siasa hizi hazifanywi na malaika kutoka mbinguni, ipo siku mtaparangana, mkishaparangana kuna kuwa na kondoo wawili yule mwenye manyoya tele na kondoo mwenye manyoya haba hapa ndipo tamu zinaondoka na kuja chungu za siasa, nakwambia  usalama wa kondoo mwenye manyoya haba lazima uwe mashakani.”

Kwa hiyo wanasiasa wa Tanzania na hasa CCM wajitahidi kulifanyia kazi suala hili la usalama wa raia kwa nguvu zote na nawaomba kwa heshima na taadhima waache kulichezea shere .

Nakuomba msomaji wangu nikusimulie kisa hiki cha taifa la Iraki mara baada ya Saddam Hussein kuingia madarakani mwaka 1979 kumbuka Saddam Hussein aliingoza Iraki tangu 1979-2003

Chama cha Ba'ath kilichokuwa na jina hilo kinachoongoza Iraki na chama chenye jina hilo hilo kinachoongoza Syria mwaka 1979 vilipishana na kukaibuka mauaji ya makomredi wa wa Chama cha Ba'ath cha Iraqi uliyooratibiwa Julai 22, 1979 na rais wa wakati huo Saddam Hussein, siku sita baada ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Iraq mnamo Julai 16, 1979 ikiwa ni siku sita baada ya kujiuzulu kwa Rais Ahmed Hassan al-Bakr na Saddam Hussein kuwa rais. Siku hiyo liliandaliwa kongamano la cha Baath Julai. 22 katika Ukumbi wa Al-Khuld huko Baghdad ili kutekeleza kampeni ya kukamatwa na kunyongwa ambayo ilijumuisha wanachama wa chama hicho ambao walituhumiwa kushiriki katika njama inayounga mkono Syria ya kumpindua Saddam Hussein. Orodha hiyo ilijumuisha wengi wa makomredi waliompinga Saddam Hussein kuingia madarakani baada ya Al-Bakr kujiuzuo na miongoni mwao alikuwa katibu wa rais wa zamani, Muhyi Abdul-Hussein Mashhadi. Majina ya watu yalitangazwa na wakatolewa nje ya ukumbi kuuawa.Propaganda za chama cha Baath wakati huo zilionyesha kwamba walitiwa hatiani kwa kula njama na uhaini ikimtuhumu Hafiz al-Assad wa Syria kufadhili hilo kwa kupanga njama hiyo.


 

Kwa wale ambao hawamfahamu Hafiz a Assadi alikuw ani rais wa 18 Syria amabye aliongoza taifa hilo tangu mwaka 1971 hadi alipofariki 2000 ambao mtoto wake wa tatu ndiye akawa mtawala wa Syria ambaye ni Bashar al Assad.

Awali mazungumzo ya muungano wa Syria na Iraq yalifanyika , Duru mbalimbali za mazungumzo ya muungano zilikuwa zikiendelea kati ya vyama viwili vya Ba’ath katika ngazi rasmi, huku makamu wa rais wa Iraq Saddam Hussein akiidhinisha hadharani muungano wa Iraq na Syria mwaka 1978. Kufikia wakati huo, Saddam alikuwa amekuwa kiongozi madhubuti wa chama hiki huko Iraki hili ni kutokana na sababu ya kiafya ya Rais wa Iraq Ahmed Hussein Al-Bakr. Matakwa makuu la Saddam lilikuwa kuunganishwa kwa mbawa za Syria na Iraq za chama cha Baath, kama hatua ya kwanza ya kuunganisha Syria na Iraq. Pia alitafuta urekebishaji wa Michel Aflaq, ambaye alikuwa kwenye orodha ya wauaji wa chama cha Ba'ath cha Syria, na kumfanya Aflaq kuwa mkuu wa Chama kilichoungana tena cha Ba'ath. Iliripotiwa kwamba Rais wa Syria Hafiz al-Assad wakati huo alipinga madai haya na alipinga vikali wazo la mpango ya umoja ya kijeshi. Julai 11,1979, Rais Ahmed Hussein al-Bakr alitangaza kujiuzulu kwake mbele ya mkutano wa Baraza la Mapinduzi na nia yake ya kuuhamishia huo urais kwa Saddam Hussein. Wakati Redio Free Europe ya serikali ya Marekani ilidai mwaka wa 2003. kwamba hapa hakukuwa na kujiuzulu bali yalikuwa ni mapinduzi, kujiuzulu ilikuwa ni danganya toto kula kunde mbichi.

“Saddam Hussein alimlazimisha Rais mgonjwa kustaafu kwa sababu za kiafya"

Muhyi Abdul-Hussein Mashhadi kumbuka alikuwa katibu wa rais alipinga vikali kujiuzulu kwa Rais al-Bakr wakati wa kikao na akamtaka al-Bakr kuchukua likizo ya muda bila kukabidhi madaraka kwa mrithi wake, pendekezo ambalo lilikataliwa na Al-Bakr kikaoni. Hili liliibua mashaka ya Saddam Hussein hadharani katika mkutano huu wa viongozi wa chama ulioitishwa Julai 22,1979.

 Tukio lenyewe lilikuwaje?

 

“Saddam aliitisha haraka kikao cha dharula cha viongozi wa chama mnamo Julai 22. Wakati wa mkutano huo, ambao aliamuru kurekodiwa kwa video, alidai kuwa aligundua safu ya tano ndani ya chama. Abdul-Hussein ambaye alikiri kuwa sehemu ya kundi linalofadhiliwa na Syria lililoanzishwa mwaka 1975 ambalo lilikuwa na jukumu kubwa katika njama zinazoungwa mkono na Syria dhidi ya serikali ya Iraq. Pia alitoa majina ya watu 68 wanaodaiwa kushirikiana nao. Hawa waliondolewa chumbani mmoja baada ya mwingine huku majina yao yakiitwa na kuwekwa chini ya ulinzi. Baada ya orodha hiyo kusomwa. Saddam aliwapongeza wale ambao bado walikuwa wameketi katika chumba hicho kwa uaminifu wao wa zamani na uaminifu wa siku zijazo. Wale waliokamatwa kwenye mkutano huo walihukumiwa pamoja na kupatikana na hatia ya uhaini. Wanaume 22, wakiwemo wajumbe watano wa Baraza la Mapinduzi, walihukumiwa kunyongwa.Maelezo ya matukio hayo yalitangazwa Julai 28 1979, na vyombo vya habari vya Iraq vikaanza kuishutumu Syria kwa kuunga mkono madai hayo. Wanachama wa chama cha Waba’ath wa Syria walijibu kwa kukataa uhusiano wowote na waliopanga mapinduzi. Agosti 8, Shirika la Habari la Iraq lilitangaza kwamba Wairaki ishirini na moja kati ya ishirini na wawili waliuawa kwa kupigwa risasi kwa ajili ya uhaini wa kupanga kumpindua rais mpya wa Iraq. Mwanamume huyo wa ishirini na mbili alihukumiwa kifo bila kuwepo kwa sababu hakupatikana popote,”

Mkanda ya kikao hicho na mkanda wa mauaji hayo ulisambazwa nchi nzima. Agosti 1979 -muda mfupi baadaye , Saddam Hussein alienda kwenye makazi ya Rais wa taifa hilo huko Baghdad kuwajulisha umati wa wafuasi 50,000 waliokuwa wakiimba kwamba alikuwa ametoka tu kushuhudia adhabu ambayo mahakama ilikuwa imeamuru kwa watu 21 walikuwa wameuawa kwa kufyatua risasi. Umati huu ulishangilia sana .


 Twende taratibu msomaji
wangu sasa nakuomba vitazame visa hivi ;

“Mlinzi wa nyumba ya aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mh.Bethueli Milla, Bwana Samson Ndavi na mkewe Bi Chistina Mwakilembe waliuwawa kikatili kwa kupigwa na nondo vichwani hapa jijini Mbeya na watu wanaodaiwa  kuwa walikuwa na nia ya kumiliki mali zilizokuwamo ndani nyumba hiyo.”

Hii ni taarifa ya Machi 10, 2021 ya ITV na ikipewa kichwa-Mlinzi wa Nyumba ya Jaji na Mkewe Wauawa Kikatili Mbeya.

Taarifa nyingine ni hii;

“Profesa Juan Timoth Mwaikusa(58) aliuwawa kinyama kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiw a kuwa majambazi, nyumbani kwake .”

Hii ni taarifa iliyoripotiwa na gazeti la Tanzania Daima la Julai 15, 2010.

Taarifa ya tatu ni hii;

“Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dkt Segondo Mvungi (61) alifariki dunia katika hospitali ya Milpark Netcare Johanesburg Afrika ya Kusini Novemba 12, 2013 ambapo awali alivamiwa nyumbani kwake jijini  Dar es Salaam na watu wanaodaiwa kuwa majambazi na kumpora silaha yake na kompyuta mpakato na kutokomea navyo kusikojulikana, marehemu ambaye alikuwa mwanasheria na kiongozi wa NCCR MAGEUZI awali alipata huduma za tiba Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Afrika ya Kusini ambapo alifariki dunia.”

Hii ni taarifa lliyoripotiwa na vyombo vingi vya habari Novemba 12, 2013.

Katika hii haya yote nakuomba msomaji wangu ambatanisha na shambulio la Tundu Lissu ambaye aliposhambuliwa alikuwa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Natambua msomaji wangu unafuatilia kwa karibu na tupo pamoja tangu katika kisa kile chama cha chama Ba’ath cha Iraki mwaka ule 1979 hadi visa hivi vya matukio haya ya Tanzania huru hiki cha walinzi wa makazi ya jaji,kifocha Segondo Mvungi, mauwaji wa Profesa Juan Mwaikusa na hata shambulio la Tundu Lissu.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mosi kwa sasa kimeibuka madai kuwa baadhi ya wanachama na makada wa CCM ni wasaliti huku wengine wakitenguliwa teuzi zao ikidaiwa kuwa wanatoa kauli kadhaa ambazo zinakidhalilisha chama hiki hadharani. Kwa hakika vikao vya CCM sasa na kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 lazima viwe vya moto. Mwanakwetu ameyatayarisha makala haya ili kutoa somo kwa kila MwanaCCM hasa wale wenye nafasi watambue namna madaraka yalivyo matamu na hali ya kupambania madaraka inavyoweza kufikia katika hatua kadhaa zenye madhara katika chama cha siasa na awali kondoo mwenye manyoya haba ndiye anayefikwa na mzizimo wa baridi.

 

Mwanakwetu anaishauri CCM kwa sasa ijitahidi vikao vyake vyote viwe vya wazi na vya kuwapa wajumbe wa vikao hivyo nafasi ya kusema na kushauri bila kumpendelea mtu yoyote pia vikao vyote vya CCM tangu ngazi ya shina hadi taifa vifanyike katika ofisi halali za chama siyo pahala pengine, vipo vikao vinaonekana kufanyika katika ofisi za umma mathalani Ikulu, hili  Katibu Mkuu wa Chama awe makini, kama CCM haina ukumbi basi eneo hilo la ukumbi liwe katika maandalizi ya chama hapa inawapa uhuru wajumbe wa kikao kuchanga hoja kwa uhuru.

Nao vingozi wa CCM lazima wawe wavumilivu katika mambo ya chama,maana chama si mali ya mtu bali ya wanachama kama hilo litafanyika litsaidia kutokutokea mambo ambayo yasieleweka na migogoro tela kama ile ya Julai 22, 979 kwa chama cha Ba’ath cha Iraki

 

Shabaha ya pili ya makala haya ukitazama hivyo visa vinne tangu kile cha familia ya Jaji Bethueli Milla ambao mlinzi na mkewe waliuwawa, alafu kuuwawa kwa Profesa Juan Mwaikyusa wakili, kifo cha aliyekuwa Mjumbe Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyeshambuliwa na jamaa wanaodaiwa kuwa ni majambazi na pia hata hili shambulio la Tundu Lissu ambalo halieleweki hadi kesho.Haya ni matukio yaliyotokea katika ardhi ya Tanzania na tena Tanzania huru. Swali ni je watu wenye nafasi wapo salama? Kwa uhakika hapo usalama wao haupo, haya ni mashakani mazito lazima wenye nafasi kama wana nia njema watuongoze tusio na nafasi kuhakikisha panakuwepo na usalama wa kila Mtanzania na siyo vinginevyo na yoyote yuleanayepinga hilo siyo mwenzetu na hapaswi kuwa miongoni mwetu iwe dunia na hata akhera.Ukivitazama visa hivyo hawa ni watu wenye uwezo ambao pengine waliweza kuwa wanamiliki silaha, wana ulinzi binafsi lakini walifika na shida hizi, hali inakuwaje kwa mtu wa kawaida ambaye hana uwezo, hawezi kuwa na ulinzi hawezi kumiliki silaha?

“Je Mbunge Bungeni anaweza kuchagia hoja vizuri akiwa na uhakika wa usalama wake? Je Jaji anaweza kuhukumu kwa haki akiwa na uhakika wa usalama wake?Hakimu na wakili mahakamani wanaweza kuifanya kazi yao vizuri?Mwalimu anaweza kusomesha vizuri, je mkulima anaweza kulima kwa amani , Je Mkuu wa wilaya anaweza kuingoza wilaya yake vizuri na kwa haki, vipi kwa mwandishi wa habari?”

Hali siyo nzuri, anayejiona yu salama hata kama ana ulinzi namna gani atambue kuwa hayupo salama kwa maana kama atashindwa kutimiza wajibu wake kulinda maslahi ya usalama wa wengi iwe Bungeni, iwe Mahakamani iwe shambani na hata iwe Serikalini na hata yeye hawezi kuwa salama.

Majina haya yaliyotajwa ni sehemu ndogo katika visa vingi vya kuhudhunisha vya Watanzania wengi walipotea , kufariki au kuumizwa na nia siyo kuyatoa machozi ya ndugu wa familia hizo la hasha nia ni kufanyiwa kazi suala hili la usalama wa binadamu ili kila mmoja aweze kushiriki shughuli zake za kila siku, hilo ni jukumu la serikali yoyote iliyopo madarakani maana madhara yake ni kwa kondoo mwenye manyoya haba na yule mwenye manyoya tele.


 

Mwanakwetu upo?

“KONDOO MWENYE MANYOYA TELE.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257






 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments