NILIKUWEPO WAKATI WANAJIFUNZA UPOLISI

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala yenye kuteua KATUNI NNE miongoni mwa katuni tele, kuzielezea, kuzichambua na kuijenga makala haya yaliyopewa jina Makala ya Katuni.

Kuianza safari hiyo ya makala haya Mwanakwetu anaisogeza katuni ya awali ambayo inaonesha linamwasesere moja kubwa, lenye midomo miwili; mmoja juu na mdomo wa pili upo katika tumbo lake pale kwenye kitambi. Haya ni mambo makubwa. Dubuwana hili lililopewa wajihi wa binadamu likiwa linacheka sana, flemu zote mbili za meno yake wazi, limejaa furaha tele.

Midomo hii miwili wa juu umefumbata meno lakini mdomo wa pili uwazi, huku kuna vitu kama vyakula vikifakamiwa na kuingizwa kwa kasi katika mdomo uliopachikwa kitambini. Huku juu ya kitambi kuna kamtu kadogo kamekonda, kakiwa kameshika faneli kama ile yakupitishia mafuta dukani, faneli hii inapitisha vyakula hivyo ambavyo vinapitia humo humo kutoka katika bomba moja kubwa ambalo limepewa jina MISAADA. Jamaa hili kubwa kubwa linaonekana linakula kweli kweli, JAHILI, BEDUI na HARAMIA lisilo na SONI wala HURUMA huku linashindwa hata kufunga vifungo vya shati , koti na hata mkanda wa sarawili yake bila kuhofia kukaa uchi kwa sababu ya kula.

Katuni hili la mwanasesere linampa tafakari kubwa Mwanakwetu- Kwa hakika mchoraji wake anaonesha namna mataifa masikini yanavyopokea misaada kadhaa kwa kigezo cha umasikini lakini misaada hiyo inawafanufaisha wakubwa tu na wao wananenepa na kunawili huku masikini hao wamebaki kukondeana mno, huku masikini hao wakiendelea kutoa ushirikiano kwa kushika faneli za kupitishia misaada. Kikubwa kinachosisitizwa ni kuwa lazima misaada hii iwafikie walengwa na kuwaondoa katika umasikini, wasikondeana na hawa wakubwa kana kambwa wanaonywa kwa maneno yaliyokoza wino ACHENI UROHO na URAFI.


 

Sasa ninaikamata katuni ya pili ambayo inaonesha jamaa fundi magari akiikarabati injini ya gari ambayo inaonekana imeingia dosari, injini hii ni ya Lori kama ISUZU DIRECT INJECTION, kwa kando yupo mama mmoja amevalia gauni jeusi na hijabu nyekundu. Jamaa huyu Bwana Fundi anamwambia Bi Mkubwa, mama tumejitahidi kuikarabati injini lakini haisadii nashauri tununue gari jipya. Lori hili Isuzu boksi bodi limepiwa jina POLISI.

Mwanakwetu anapolitazama Lori hili amekumbuka jambo, wakati wa Ujamaa Kijiji cha Ujamaa MKIU huko Pwani ya Tanzania walikuwa na lori kama hilo ambao lilipewa jina UJAMAA MKIU, haya yalikuwa matunda ya ujamaa ambapo vijiji kadhaa vilikuwa na rasilimali tele kama vile matrekta, maduka, maghala, nyumba za wageni na rasilimali tele mathalani Kijiji cha Ujamaa Kwalukonge huko Tanga kilikuwa kijiji cha mfano chenye rasilimali tele na Kijiji cha Ujamaa Isimani walikuwa hodari wa kulima mahidi. Je Leo hii Kijiji chako ulichozaliwa, wewe unayeyasoma makala haya kinamiliki nini? Vijiji vingi vya Tanzania leo vinamiliki tu hati za kuanzisha vijiji na mafaili tele, Je Tanzania tumeendelea au tumerudi nyuma? Msomaji wangu jibu unalo.

Tusiende mbali sana sasa turudi katika katuni hii, kwa hakika hii katuni inaonesha hali iliyochorwa na mchoraji juu Jeshi la Polisi Tanzania kuwa lipo hoi bini taabani na kando huyu mama aliyevaa hijabu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassani, ambapo mchoraji anamshauri kuwa jeshi hilo linatakiwa kuundwa upya. Mwanakwetu hakubaliani na hoja ya kuliunda upya Jeshi la Polisi Tanzania, kwani vijana wa jeshi hili wapo imara sana katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, maana wanapotekeleza majukumu yao mara nyingi wanakuwa katika sare na namba za utambulisho, changamotoni ya utakelezaji wa majukumuya jeshi hili kuna haja wawe huru na kutoingiliwa na taasisi zingine na hayta vyama vyovyote vya siasa iwe tawala na hata pinzani. Polisi wanapoingiliwa kati mwisho wa siku wakikengeuka au kupakwa matope wao wenyewe na wanaadhibiwa mbele ya mahakama , hili vijana Jeshi la Polisi Tanzania wanatambua. 


 DCI KINGAI ENZI ZAKE AKIWA RPC

Polisi wetu waongozwe na sheria ya kuanzishwa kwa jeshi hili, wakumbuke kuwa wao ndiyo wanaovaa sare, ndiyo wenye namba na ndiyo waliohudhuria mafunzo ya upolisi kama CCP au kule ZANZIBAR. Anayetoa agizo la kukengeuka ajiulize swali hili,

“Nilikuwepo CCP au Kule ZANZIBAR wakati wanajifunza Upolisi?”

Mwanakwetu anauomba umma wa Watanzania kutambua kuwa polisi ni ndugu zetu, wanatoka katika familia zetu za kimasikini wanakwenda huko kupata ajira na kututumikia sisi wenyewe Watanzania. Mwanakwetu pia anawaomba Jeshi la Polisi Tanzania watambue jamii inawategemea, jeshi hilo si mali ya mtu, si mali ya kikundi cha watu wachache, ni mali ya jamii ya Watanzania yaani mimi na wewe na mashaka yoyote dhidi ya jeshi hili ni hatari kwa kushamiri kwa amani ya jamii ya Watanzania.Tena wengine wanatoa maagizo ukijiuliza mbona hakuwa polisi hawana majibu.

Makala ya Katuni yanasema Wanasiasa wa Tanzania wawe wa chama tawala au pinzani wawe makini, hili ni jeshi la kila Mtanzania, limekusanya vijana kutoka Tanzania nzima, familia tofauti, dini tafauti, kabila tafauti, misimamo ya kisiasa tofauti, tuwaache wafanye kazi kwa mujibu wa sheria yao na si vinginevyo.

Nakutana na katuni ya tatu ambayo inaonesha dubuwana kama kitu kinachozuguka ambacho kimewabamiza watu kadhaa chini ambao wamepewa jina Wapiga Kura na juu wapo jamaa wamevaa vizuri wanapendeza huku wakitumia simu zao kujipiga picha na mbele ya mzunguko huu yupo jamaa ambaye anawasalimu wale waliojuu na chini. Huyu ni kiongozi aliyeshinda uchaguzi.


 

Mchoraji wa katuni hii anatilia maanani kuwa viongozi wanashinda chaguzi alafu badala ya kuwasaidia wapiga kura hali inakuwa vinginevyo kabisa wanawakandamiza wapiga kura hao walio wengi na kundi la wachache ndiyo wanaonufahika nao. Mchoraji wa katuni hii analikemea hilo kwa sauti ya juu na kuwakaripia wanasiasa hao akinadi waache mara moja.

Sasa ninayo katuni ya nne ambayo inaonesha magari mawili moja kubwa kama BMW lipo chini likakata mbuga na limeibeba gari ndogo juu ambayo imeunganishwa na mashine fulani . Gari ya chini wapo jamaa wanayoiendesha lakini hawajulikana, huku gari iliyojuu inaye dereva ambaye anaonekana mama mmoja aliyevalia hijabu na huku kibao cha gari ndogo juu kimepewa jina SSH. Kando ya gari hizo kuna kibao kimeandika Uchaguzi wa Tanzania 2025.

Mwanakwetu anapoitazama katuni hii inaonesha hali ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2025 kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wapo watu wanaomsaidia ambao hawajulikani kuuelekea katika uchaguzi huo. Uwepo wa gari kubwa uliyoibeba ndogo kuwa hata kama gari kubwa chini itakwama basi gari kubwa isadie gari ndogo kuisukuma mbele kwa kutumia mashine ilyounganisha gari hizo alafu gari ndogo kupewwa matairi alafu itafikia ushindi wa Rais Samia katika uchaguzi huu bila changamoto yoyote.

Mwanakwetu anaamini kuwa taswira hii ni mwangaza kwa wale wanaohitaji kushindana na kiongozi huyu kamani Dkt Josephart Gwajima au Tundu Lissu katika uchaguzi huu wa 2025 wa taifa mojawapo la Afrika Mashariki lililowahi kuongozwa na Mwalimu Julius Nyerere. Wanaotarajia kupambana na Rais Samia kama n Dkt Gwajima au Lissu lazima watambue uwepo wa magari haya mawili basi kama wanapanga kupambananaye waje na magari makubwa zaidi yenye winji kubambana na mwanasiasa huyu wa Chama cha Mapinduzi ambaye ni mzaliwa wa huko Kizimkazi Zanzibari. Kikubwa tusiandikie mate wakati wino upo, tuwe wastamilivu hadi Oktoba 2025 , tuombe uhai tu kwa Mweenyeenzi Mungu.


 

Mwanakwetu upo?

Basi hadi hapo na mimi ndiyo naufunga ukurasa huu wa makala ya katuni siku ya leo, kumbuka nilikuwa na katuni nne, ile ya mwanasesere mwenye midomo miwili, hii ya ISUZU DIRECT INJECTION YA POLISI, katuni ya tatu ni ya gurudumu linalowakanyaga bila huruma wapiga kura na hii ya mwisho ni ya Urais wa Samia Suluhu Hassan 2025.

Kumbuka

“Nilikuwepo CCP Wakati Wanajifunza Upolisi?”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 





Huyu ndiye Afande MISEMe msemaji wa Jeshi letu la Polisi

 

0/Post a Comment/Comments