TANZANIA INAHITAJI JAJI MKUU MPYA-MwAnAKwEtu

Adeladius Makwega-MWANZA

Nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala yanayokusanya katuni nne zenye maudhui tafauti, zinachaguliwa, zinaelezewa, zinachambuliwa kwa maoni ya mtayarishaji wa makala haya alafu unaachiwa wewe msomaji kupima kile kilichomo katika makala haya.

Kulipiga jalamba la makala haya makini nakutana na katuni moja, inayomuonesha binti mdogo akiwa amebeba keni(dumu) ya maji, akiwa pekupeku akikatisha mazingira ya kijijini akitoka kuyachota maji. Binti huyu kisogoni kwake kuna ishara inayoonesha ametembea KM 2 kuyasaka maji hayo maana yake KM 2 kwenda na KM 2 kurudi , binti mdogo-binti kigoli anatembea KM 4 na ushehe kuyasaka maji kwa matumizi ya binadamu.

Mwanakwetu anapoitazama katuni hii anatambua fika inatilia maanani kwanza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini hapa Tanzania na pili maji hayo yawe jirani nao na siyo kutembea umbali mrefu.

Mwanakwetu anatambua na kuheshimu utendaji kazi wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji nduguye mh Jumaa Awesu lakini juhudi zake haziwezi kufua dafu kama wizara hii itapatiwa bajeti ya kidogo ambapokwa mwaka wa fedha 2023/2024 ilipokea 84.6% ya bajeti yote iliyotengwa.Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ilikondoa adha ya maji Wizara iliomba shilingi 627,778,338,000 ambapo shilingi 69,662,959,000 zamatumizi ya kawaida wakati shilling 558,115,379,000 ni fedha za miradi ya maendeleo katika miradi ya maji, hiyo Mwanakwetu analipiga chapuo hiyo pesa wapewe 100%.


 

Makala ya Katuni ya siku ya leo yanachanja mbuga na kukutana na katuni ya pii inayoonesha mama mmoja aliyevalia gauni jeusi na hijabu juu yake, mama huyu kapachika na miwani. Kulia kwa mama huyu, yupo jamaa kavaa gauni jekundu, mshipi mweusi na kola nyeupe na kando kuna jamaa waliyovaa hivyo hivyo kama wanakula kiapo hivi.

Unapoitazama katuni hii, huyu mama mvaa hijabu anafanana fika na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapokuwa kazini akiwaapisha majaji na kando yake Jaji Mkuu akifuatilia zoezi hilo.

Mwanakwetu katuni hii imemkumbusha kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania nduguye Profesa Ibrahimu Hamis Jumaa amezaliwa Juni 15, 1958, akiwa mjuzi wa masuala ya sheria aliyoyapata  Chuo Kikuu cha Lund, Chuo Kikuu cha SOAS, Chuo Kikuu cha Ghent na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa umri wake Jaji Mkuu inatrajiwa atafikisha miaka 70 Juni 15, 2028, ambapo alianza kuongoza Mahakama ya Tanzania Septemba 10, 2017.

Kwa hakika kwa umri wa Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Hamis Jumaa ni kama kaka wa Mwanakwetu na mchango wa Profesa Jumaa wa miaka saba katika mahakama ya Tanzania sasa unatosha, Mwanakwetu anayasema haya kwa sababu ipi?

“Katika mtazamo wa kibaiolojia, kuzeeka kunatokana na athari za mkusanyiko wa aina mbalimbali za uharibifu wa molekuli na seli za binadamu mwilini kulingana na umri wa binadamu unavyozidi kuwa mkubwa.Hii inasababisha kupungua polepole kwa uwezo wa kimwili na kiakili, hatari ya magonjwa na hatima anayo mwenyeezi Mungu. Mabadiliko haya si ya mstari au thabiti, na yanahusishwa tu na umri wa mtu katika miaka. Tofauti inayoonekana katika uzee sio bahati nasibu ni ya uhakika. Zaidi ya mabadiliko ya kibaiolojia. Uzee mara nyingi huhusishwa na mabadiliko mengine ya maisha kama kufanya kazi sana , kama vile kustaafu, kuhamishwa hamishwa kutoka eneo moja kwenda eneo gumu zaidi na hata kupoteza idadi wa watu wa karibu yako uliyosoma nao kukua nao na hata kufanya nao kazi zamani ambao hawapo ulimwengu.”

Haya ni maelekezo ya Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, yakielezea suala la uzee na maelezo haya chanzo chake ni hiki,

“Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) lilitangaza mwaka 2021–2030 kuwa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa KUZEEKA &AFYA na kuomba WHO kuongoza utekelezaji huo. Muongo wa Umoja wa Mataifa wa kuzeeka & afya ni ushirikiano wa kimataifa unaoleta pamoja serikali, mashirika ya kiraia, mashirika ya kimataifa, wataalamu, wasomi, VYOMBO VYA HABARI na sekta binafsi, kwa miaka 10 ya hatua za pamoja, za kichocheo na shirikishi ili kukuza maisha marefu na yenye afya kwa wazee. Muongo huu unajengwa juu ya Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa Kimataifa wa WHO na Mpango wa Utekelezaji wa Kimataifa wa Madrid wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uzee na kuunga mkono kutekelezwa kwa Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 kuhusu Maendeleo Endelevu na Malengo ya Maendeleo Endelevu.”

Haya ni maelezo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya uzee ambayo yanaiagiza WHO

Kwa kifupi mtu anapongezewa muda kazini unampa majukumu zaidi ambayo yanamchosha zaidi, hawa wazee wetu wanatakiwa kupumzishwa majukumu wabaki wanapokea posa kwa kuoza binti zao na kushiriki harusi haya ni mambo ya familia tu.

Tangu mwaka 2017 hadi 2024 mahakama itakuwa na majaji kadhaa wenye sifa ya kukikalia kiti hichi au itakuwa sahihi Mwanakwetu kuuliza swali hili,

“Profesa Ibrahimu Hamisi Jumaa alikuwa mchoyo wa kurithisha ujuzi wa uongozi katika Mahakama yetu kwa majaji waliyo chini yake kwa miaka hiyo sabaa?”

Kama jibu lake ni HAPANA, shida ipo wapi?

 


Mwanakwetu anasema,

“Tanzania inahitaji Kupata Jaji Mkuu Mpya.”

Sasa naisogeza katuni yangu ya tatu ambayo inamuonesha mama mmoja yupo hotelini, amevalia gauni lake jeusi maridadi na juu kapachika hijabu nyekundu, mama huyu ameshika kijitabu kimeandikwa menu mama anataka kuagiza msosi ale. Kwa kando kuna mhudumu kijana maridadi anamdokeza mama huyu kumuomba kwa heshima na taadhima kutazama ubao uliyoandikwa Today Special, mhudumu anasema mama tupia jicho kwenye spesho ya leo.

Ubao huo uliosimamishwa mshazari unaonesha KATIBA MPYA.

Mwanakwetu anapoizama katuni hii anatambua kuwa Mchoraji wake anamkumbusha huyu mama kando anayeshabiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya Kupatikana kwa KATIBA MPYA.

Mwanakwetu katika hili hana la kuongeza

Sasa anakutana na katuni ya nne ambayo inamuonesha mama kama yule yule anagawa zawadi ya viwalo kwa watoto wake lakini kwa kando yupo mtoto kavaa misurupwete hapewi chochote na mtoto huyu kapewa jina KATIBA MPYA. Cha kusikitisha hawa wanaopewa viwalo wana nguo nzuri Lakini mama hata kumtazama huyu mtoto mwenye misurupwete, lakini mtoto anasubiri maana subira inavuta heri.

Katuni hii inalingana na kwa madai yaleyale ya Katiba Mpya ya Watanzania, lakini kapu la mama limejaa viwalo Mwanakwetu anayo matumaini makubwa kuwa Rais Samia siyo mchoyo bali mkarimu na suala hili atalifanyia kazi .

Mwanakwetu Upo?

Basi msomaji wangu kwa katuni hizo nne, ile ya kuyaska maji KM 2, Ile ya  Kiapo cha Majaji, hii ya  Rais Samia na Katiba Mpya ambayo inalingana na katuni hii ya mwisho juu ya Ukarimu wa Rais Samia ndiyo na mimi naufunga ukurasa huu wa makala ya katuni siku ya leo.


 

Kumbuka ,

“Tanzania Inahitaji Jaji Mkuu Mpya.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 



Post a Comment