WAAMINI PAROKIA MALYA KULA CHAKULA NA KUHANI MKUU

Adeladius Makwega-MWANZA

Wakristo wameambiwa kuwa hata kama mnakuwa na madaraka iwe katika familia, iwe katika jumuiya yoyote ile , iwe kanisani na hata serikalini mnapokabidhiwa mamlaka si kwa manufaa yao bali manufaa ya jamii nzima ili ipate neema ya madaraka hayo.

Hayo yamehubiriwa na Padri Samson Masanja katika Kanisa la Bikira Maria, Malkia wa Wamisionari–Parokia ya Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza katika ibada ya misa ya jumapili ya 25, Septemba 22, 2024 ya mwaka B wa Liturujia ya kanisa.

“Kati ya mambo yanayotuvuruga kukosa usingizi, kukosa amani duniani ni madaraka, miongoni mwake ni ukubwa, tunatamani madaraka hayo si kwamba tuwasaidie wengine, bali tuabudiwe, bali tutukuzwe, bali tuheshimiwe na mambo mengine yanayoambatana na hayo, ndugu zangu wapendwa, ukubwa tunaoutafuta , madaraka tunayoyasaka hayatokuwa na maana yoyote kwa mwanadamu kama hatutokubali kujishusha,kama hatutokubali kuwa watumishi wa wengine, tunapotazama miongoni mwetu, tunapojitazama miongoni mwetu tunao watu wa madaraka na vyeo mbalimbali, tujitafakari katika dominika ya leo huo uongozi, hayo madaraka tuliyo nayo ni kwa ajili ya watu wengine au kwa ajili yetu wenyewe? Madaraka na uongozi tulionao tumepewa kwa ajili ya wengine ili sisi hata kama tunateseka, hao wengine waonje na wafuruhie uwepo wa Mungu katika maisha yetu”

Paroko Padri Samson Masanja akauupigilia msumari wa mwisho wa mahubiri yake akisema huo ndiyo msisitizo unaojengwa katika masomo yote matatu ya dominika ya 25 ya Mwaka B wa Liturujia ya Kanisa.


 

Kandoni mwa Ibada hii ya misa waamini wa Parokia ya Malya wanajadili mambo makuu mawili; Mosi ni kuchelewa kwa mvua za masika mwaka huu 2024, wakati uzoefu mwaka uliopita mvua za masika zilianza kunyesha mwishoni mwa Agosti na Septemba tayari wakulima waliopanda mapema mahindi yao yalikuwa yana majani matano hadi sita na hata kabla ya ibada hii ya misa waamini hao walikuwa wakiweka miadi ya kunuia katika maombi yao binafsi ibadani kuomba mvua hizo kunyesha kwa wakati.

Jambo la pili lililokuwa gumzo ni juu ya harambee yao kubwa ya Parokia ya Malya ya miradi yao ya maendeleo na maboresho ya miundo mbinu ya Kanisa lao, Harambee hiyo inayotarajiwa kufanyika Septemba 29, 2024 ambapo kutakuwa na ibada ya misa ya Kiaskofu ya Muhashamu Baba Askofu Renatus Mkwande, huku waamini hao wakihimizana kukamilisha maadalizi ya tukio hilo kwa wakati na ikinadiwa kanisani kuwa baada ya ibada hiyo siku ya harambee waamini wote watakula chakula cha pamoja na Baba Askofu, ikisisitizwa kila muamini kubeba sahani yake kutoka nyumbani siku hiyo iwe rahisi kugawiwa chakula bure kwa waamini wote.

Kwa hakika mwandishi wa makala haya tayari ameshaitayarisha sahani yake na kijiko, ili apate wasaa mzuri wa kula chakula jirani na Baba Askofu ambaye ndiye Kuhani Mkuu.

Nakutakia dominika Njema.

makwadeladius@gmail com

0717649257









 


0/Post a Comment/Comments