BURIANI MIDLADJY MAEZ

 



Adeladius Makwega-MWANZA

 

Saa tatu ya Asubuhi ya Oktoba 3 ,2024 Mwanahabari Mkongwe Midladjy Maez amefariki dunia katika hospitali ya Mnazi Mmmoja na maziko yake kufanyika huko katika makaburi ya Shekhe Mohammed Ramia Bwagamoyo mkoani Pwani, taarifa za msiba huu Mwanakwetu amezipata usiku ya Oktoba 3, 2024 baada ya mwanahabari mmoja mkongwe kumpigia simu na kusema,

“Makwega Rafiki yako Midladjy Maez Amefariki Dunia .”

Kwa hakika Mwanakwetu alikuwa na urafiki wa karibu na mzee Maez ambao ulijengwa kupitia katika kazi, utani na kupigiana simu za kila mara .Kutokana na msiba huo msomaji wangu ambatana nami katika makala haya ya Buriani.

Mwaka 2007 Mwanakwetu alifika Haidary Plaza jijini Dar es Salaam, makao makuu ya chombo cha habari kilichofahamika kama Media Solution LTD wachapaji wa magazeti mawili dada THIS DAY & KULIKONI ambao walikuwa wakifanya kazi nyingi za habari za uchunguzi kwa kina, ambapo kwa sasa Tanzania haina chombo chenye sifa hiyo. Hapo Mwanakwetu alikwenda kama mwanafunzi wa mazoezi ya Shahada ya Sanaa ya Habari akiwa mwaka wa tatu, mazoezi ya vitendo kazini, japokuwa baadaye Mwanakwetu alikuwa akilipwa pesa kwa kuandika makala, chambuzi na habari mbalimbali na hawa jamaa.

Hapo alipokelewa vizuri na wakubwa kwa wadogo wa taasisi hiyo, huku mkubwa kabisa alikuwa ni Evarsit Mwitumba na wakubwa wengine walikuwa Nyaronyo Kicheere na Simoni Mkina, hapa Mwanakwetu alijifunza mambo mengi na kukutana na watu kadhaa katika tasnia ya habari.


 

Siku moja mkubwa aliyekuwa analisimamia gazeti la Kulikoni Nyaronyo Kicheere ambaye baadaye alikuwa wakili alimtuma Mwanakwetu Kituo cha Polisi cha Kati alafu akaagizwa pia apitie TRL akisema,

“Wewe kijana kutoka Iringa, leo utaandika habari ya Polisi na TRL, kumbuka kuandika vizuri kama tunavyoandika sisi watu tunaozaliwa kanda ya ziwa maana tuna akili nyingi, sisi tunakula samaki wengi. Sawa kijana?”

Mwanakwetu aliitikia ndiyo na aliekea huko, alifika polisi na maafande hao wakazungumza na vyombo vya habari vizuri mno, huku kila mwanahabari hakuondoka bure, hapo maboresho yalikuwepo na tena manono. Alipotoka hapo akapita TRL ambapo ofisi hizo zilitazamana na Kituo cha Polisi cha Kati, kumbuka msomaji wangu asubuhi ya siku hiyo Mwanakwetu alipewa jina la Afisa Habari ya TRL Midladjy Maez na aliliandika katika shajara yake vizuri sana. Mwanakwetu jina hilo alikuwa analifahamu maana lilikuwa ni miongoni mwa watangazaji wa mwanzo mwanzo wa ITV kuonekana katika kioo lakini hakuwahi kumuona kwa karibuni hata siku moja, japokuwa jina hilo likapotea kwenye kioo cha ITV.

Mwanakwetu akafuata maelekezo ya walinzi na kugonga ofisi hiyo na kufungua mlango, hapa akakutana na mhusika huyo katika chumba kimoja kidogo ambacho kilikuwa kina viti viwili tu na makaratasi mengi. Mwanakwetu hakukosa heshima alimuamkia mkubwa huyo kwa shikamoo, akayatoa maswali yake baada ya kujitambulisha, Wakubwa wa Kulikoni walimkakabidhi maswali Mwanakwetu ya kumuuliza huyu Madladjy Maez, Mwanakwetu akayauliza maswali yote, apomaliza alafu akaaga, wakati anatoka ndugu Maez alikuwa mbali mno na maboresho, hakutoa posho yoyote kumbuka kule Polisi posho zilitolewa, hapo Mwanakwetu alitoka mtupu huku posho za maafande zilimpa amani.

Wakati Afisa huyu wa TRL anamsindikiza kijana wake Mwanakwetu alisema maneno haya,

“Kumbuka kumsalimia sana Evarist Mwitumba kabla ya kuandika stori yangu maana nimefanya nae kazi yule na nikirudi ofisini nitampigia simu.”

Mwanakwetu akilini mwake alikuwa akisema leo TRL lazima wapigwe stori moja hatari hadi bodi TRL itoke usingizini, lakini sasa Afisa Habari Maez kumbe anamjua Evarist Mwitumba, hapo Mwanakwetu akawa mpole sana. Mwanakwetu akarudi na kuandika stori ya polisi juu ya kukamatwa kwa majambazi na silaha na huku akaandika habari ya TRL na mabehewa yao yaliyopotea njia nayo TRL wakibadilisha tarehe za safari. Hapo Midladjy Maez na TRL wakapona na maneno yaliyosemwa na afisa habari wao ya salaam kwa Bosi Mwitumba.


 

Maisha yaliendelea na miaka mitano baadaye yaani Oktoba 11, 2012 Midladjy Maez ambaye sasa alikuwa rafiki wa Mwanakwetu huko katika mitandao ya kijamii alichapisha ujumbe huu katika ukurasa wake mmojawapo.

“Natupia hili halafu nawahi kwa vigogo wa TRL Mtaa wa Ohio… tete teee… Hivi mbona siwaelewi Watanzania wasiopenda kusikia Bin Lowassa, Bini Kikwete, Binti Makinda, Bini Pinda, Bin Masaburi, Bini Mhavile, Bini Nchimbi , Bin Songambele , nk , nk wanagombea Uongozi inakuwa nongwa na dhambi… lakini ingekuwa majina hayo ya ukoo ni wanariadhaa au wasakata kabumbu… au Basketibali ingekuwa kimnyaa… nauliza hivi  .Watanzania tuna matatizo gani na kuanza na ugonjwa wa unyanyapaa katika majina yanayoitwa kuwa ya watoto wa vigogo, ambao wanioneshe kati niliwataja nani anamiliki hata kidege kidogo binafsi? Maana nimetumiwa  kwenye simu yangu sms ambayo inasambazwa katika mitandao kwa kasi sana leo ati, Ukombozi uko CHADEMA? Angalieni safu ya wabunge viti maalumu CHADEMA ndio mtabaini na kulijua jiji? Mbona wako watu ukoo wao wote ni wanajeshi, polisi, madaktari, bandarini, posta wanareli nk, Huu unyanyapaa na ukome mara moja.”

Hoja hiyo ilihamishiwa katika kundi la WANABIDII na Mwanakwetu na kujadiliwa mno na wachangia katika kundi hilo na pamoja na ukurasa wa mitandao ya kijamii ya Midladjy Maez mwenyewe. Mmojawapo wa wadau alitoa maoni haya,

“Hata mimi nashangaa nimeona humu FB mtu amebeba bango hivi mtoto wa Kikwete, Pinda na Makamba si Watanzania ? Huyu hana haki kuwa na chama cha siasa, huyu hana haki ya kugombea /si kuteuliwa kwa sababu ya Baba Rais.”

Mwanakwetu mjadala hapo unaendelea je yeye Mwanakwetu alitoa maoni gani? Msomaji wangu ndugu yetu Mwanakwetu alisema haya,

“Ha ha ha hii nchi si ya kifalme, baba mtawala, mtoto mtawala na mjukuu mtawala, mama mtawala. Hoja hiyo inatakiwa kutazamwa kwa uwezo wa mtu tu. Mbona Mwalimu Nyerere alimchagua kaka yake kuwa Mkuu wa Mkoa? Huyu kaka wa Mwalimu Nyerere akuibuliwa na nduguye bali alianza siasa na Mwalimu Nyerere tangu harakati za TANU na Kina Ngombale Mwiru, alikuwa kiongozi tangu TANU inadai uhuru, hakuibuka tu, wawe na sifa hilo ni la msingi. Mbona hatuwaoni na hawapendi kuwa walimu, madaktari, mafundi ujenzi, maafisa habari, manesi lakini siasa tu?”

Mwanakwetu siku hiyo alijibiwa na Salma Ali Hassan akisema maneno haya,

“Kazimbaya... sidhani kama umefanya uchunguzi kuhusu watoto wa ‘vigogo’ kutokuwemo kwenye hayo makundi uliyoyataja, chukua list ya unaowajua, angalia watoto wao WOTE wanafanya shughuli gani? Wakati mnapiga hizi kelele wenzenu wanapata tuzo za kutambuliwa ulimwenguni... au na hii ya Dr Mwele watasema amepewa kwa vile ni binti fulani?

Salima Ali Hassan, dada wa Mwanakwetu sifahamu yupo wapi kwa sasa lakini hayo yalikuwa maoni yake. Msomaji wangu usishangae majina yanayotajwa wengine ni marehemu leo hii, kumbuka huo ni mjadala wa mwaka 2012. Baada ya mjadala huo mzito mwisho wa siku Midladjy Maez aliibuka na kuyajibu maswali kadhaa na kuwashukuru watoa maoni wote akiwamo Salma Ali Hassan na Mwanakwetu.

 


Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Siku ya leo Mwanakwetu amejaribu kuyakumbusha haya kwa heshima ya Wanahabari Midladjy Maaz ambaye pengine leo hii hafahamiki na watu wengi kwakuwa hakufanya kazi kama afisa habari tu kumbe alikuwa miongoni mwa magwiji wa kusoma habari katika runinga kwa lugha kadhaa huku ndugu huyu akizungumza Kiingereza , Kiswahili na Kirusi bila tabu wala kuitafuta misamiati lakini sasa mwili wake unalala kaburini kule Bagamoyo.

Akiwa mwana habari Maez alipitia changamoto nyingi ambazo kwa hakika kama angeandika kitabu kingesomwa na wengi na changamoto mojawapo ni ile ya kufanyiwa ubaguzi kwa kuondolewa kusoma taarifa ya habari kutokana na kuwa na mwili mkubwa. Mwanakwetu wengi hawalifahamu hilo lakini huo ndiyo ukweli.Nia ya Mwanakwetu siku ya leo siyo kufukua makaburi bali kujaribu tu kueleza hatua kadhaa ambazo binadamu anaweza kupitia akiwa kazini kama alizopitia marehemu Midladjy Maez mwanahabari mkongwe.

Mwanakwetu anakujulisha msomaji wake kuwa mjadala huu wa watoto wa vigogo umetumika tu kumjenga mwanahabari Maez katika simulizi yake ya leo lakini wale watoto viongozi watambue kuwa wakipewa majukumu wasipige madochi, wafanya kazi kweli kweli iwe zaidi ya wazazi wao kuepusha malalamiko kwamba wamependelewa, hilo hakuna kuyauma maneno watoto wa vigogo walitilie maanani mno hilo na hao hao wanaowateua.

Mwanakwetu anatambua kuwa Mei 25 ya kila mwaka ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa, makala haya yanaandikwa kwa heshima zote kwa mwanahabari huyo. Japokuwa Mwanakwetu hakuwahi kualikwa na kaka huyo siku hizo za kuzaliwa aliposherekea hasa zile alipokuwa TRL maaa naambiwa alipostaafu alikuwa mgonjwa.


 

Mwanakwetu anatambua urafiki wa Mzee Maez na wanahabari na wanasiasa kadhaa kama vile Neema Mbuja na Ridhiwani Kikwete, Mwanakwetu anatambua pengine hao ndugu wametuwakilisha vema katika msiba huo. Binafsi siku ya mazishi nilitamani kushiriki kumzika Bingwa huyu wa tasnia ya habari wa Tanzania niipcheki ndege ya Dar Mwanza na hesabu ya muda nikao ningechelewa kufika Bagamoyo,nipo Mwanza na taarifa nimeipata kwa kuchelewa.

Kwa Maafisa habari wote jifunzeni hili kutoka kwa marehmu Maez;

“Lazima uwe na mahusaino mazuri na wanabari,kuwaapigia simu, unaongea nao, ukiandikwa vibaya –itazame taasisi yao toa ushauri vikao vya ndani, siyo kutumia pesa na taasisi ikiandikwa vibaya unakimbilia polisi, unafirikia unaweza kuwafunga wana habari wote au kufungia vyombo vyote vya habari, maisha ni mahusiano mema .”

Kwa msomaji wa Mwanakwetu tambua kuwa Midladjy Maez alisoma Tanzania School of Jornalism sasa ni SJMC kati ya mwaka 1980-1982 wakati huo mwana wa Makwega anahangaika kuumba herufi chekechea, Kaka Maez Shikamoo huko kaburini !  Na Mwaka 1986-1992 alikuwa Urusi akisomea Shahada ya uzamili ya Uandishi wa Habari katika Redio na Runinga. Baadaye alifanya kazi kama afisa habari wa Ushirika kati ya mwaka 1985-1994, pia alikuwa Mtangazaji na mhariri wa ITV na Redio One mwaka 1994-1994 na mwaka 2007 ndipo alipokwenda TRL. Mwanakwetu siku ya leo anaweka chini kalamu yake, huku akimuuliza marehemu Midladjy Maez huko alipo swali lile lile je bado msimamo wake bado ule ule?Je watoto wa vigogo mmeshiriki kumzika mzee wetu Maez?


 

BURIANI MIDLADJY MAEZ

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

0/Post a Comment/Comments