MCSD WAKABIDHIANA VIFAA VYA MICHEZO

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya (MCSD) Oktoba 31, 2024 wamekikabidhi chuo chao vifaa kadhaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi za Kitanzania karibu 1,000,000/=.

“Fedha hizo zilipatikana kwa timu yetu ya Mpira wa Miguu kushinda mashindano yaliyoandaliwa na Kijiji cha Malya, huku timu 28 kutoka wilaya ya Kwimba zilishiriki, nayo Timu ya MCSD-UTAMADUNI Sports Club iliichabanga bila huruma Nyabubinza kwa bao moja sufuri katika fainali ya kukata na shoka.”

Akiendelea kuzungumza katika makabidhiano haya, Waziri wa Michezo wa Serikali ya Wanachuo mwalimu Abdallah Msabaha aliongeza kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa kuzingatiwa ubora wake na kutatua changamoto ya vifaa kwa timu yao inayofanya vizuri Wilayani Kwimba na mkoani Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi Mkufunzi Omari Mataka ambaye pia ni Kaimu Mwadili wa Wanachuo alisema,

“Timu yetu ya soka inafanya vizuri na leo hii ninatembea kifua mbele kupokea matunda ya mafanikio ya soka kutoka kwa wanachuo ninawasomesha masomo kadhaa kama vile ; Uamuzi wa Soka na Uandajia wa Matukio ya Kimichezo. “

Akipokea vifaa hivyo Kaimu Mkuu wa chuo hiki Mkufunzi Joachim Maganga alipongeza wanachuo hao kwa kushiriki mashindano haya , kushinda na kufikiria kununua vifaa hivyo kwa timu yao na kuvikadhi kwa uongozi wa chuo.



 

Wakizungumza mara baada ya hafla hiyo fupi wanachuo kadhaa walioshiki mashindano haya walisema kuwa kabla ya kufikia wazo la kununua vifaa hivyo  kibindoni wakiwa na kitika hicho cha shlingi 1,000,000/= walitekwa na mjadala mrefu katika makundi makubwa mawili, juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo lakini tamati ya yote wakakata shauri la ununuzi wa vifaa hivi kwa timu yao.

“Shabaha ni kuweka alama iwe ya muda mfupi au mrefu huku kutilia maanani  umuhimu wa vifaa bora michezoni na matarajio mashindano yajayo timu yetu itavaa uzi mpya.”

Shughuli hiyo ya makabidhiano ya vifaa hivyo imehudhuliwa na Afisa Utumishi wa taasisi hii Bi Rahma Abdi, wakufunzi kadhaa, watumishi ,  wanachuo wote na viongozi wa Serikali ya Wanachuo wakiongoza na Rais wa Serikali ya Wanachuo mwalimu George Mkinga.









 



 

0/Post a Comment/Comments