PENDA NA UA LAKE

 

 



Adeladius Makwega-MBAGALA

Jumatano ya septemba 14, 2022 nilipokuwa katika shughuli zangu nilikutana na mama mmoja shabiki mkubwa wa Yanga akiwa amevalia kilemba chekundu, blauzi nyekundu suruali nyeusi na viatu vyekundu.

Kwa hakika bila ya kuingiza unazi wa Simba na Yanga, mama huyu alikuwa amependeza mno, kama unavyofahamu msomaji wangu rangi nyekundu inavutia sana na kuonekana hata ukiwa umbali gani, bahati hiyo siyo kwa rangi ya kijani au njano.

“Kwa kumtazama bi mkubwa huyu alipendeza zaidi kwani alikuwa na mweusi wa asili unaong’ara huku rangi ya blauzi nyekundu ikiwakawaka katika sura yake iliyopambwa na mafuta yanayonukia vizuri sana mithili ya tausi aliyepo katika bustani ya mfalme.”

 

Kama  ujuavyo msomaji wangu Mwanakwetu si mwingi wa uchoyo, nimejaliwa ukarimu, nilimsogelea ndugu yangu huyu kwanza na kumpa mkono wa hongera uliojaa pongezi tele za kupendeza huko, nayeye alijibu kwa neno asante. Nikauliza mambo haya ya kupendeza ni ya lini au siku zote? Nilijibiwa kuwa hizo ni habari za siku zote.Nilipomdodosa nilibaini kuwa kupendeza huko kote mama huyu alikuwa mzaliwa wa Mtaa wa Twiga wa Jangwani Dar es Salaam huku akishabikia timu ya mtaa huo ya Yanga African Sports Club .

Kwa kuwa Mwanakwetu ni shabiki wa Simba niliomba ruhusa ya kupiga picha na mama huyu huku nikiwa na langu la moyoni, nilijibiwa sawa.


“Lakini unataka kupiga picha je mume wake akiuliza huyu uliyepiga naye picha ni nani je akatoe majibu gani?”

 

Niliulizwanikamwambia hilo tu, kabla sijasema neno akaniambia unataka nipewe talaka? Nikamwambia,

 

“Unaogopa talaka, talaka ni karatasi tu, akitoa talaka ninakuhamishia Chamwino Ikulu, utakuja kupigwa na upepo wa Ikulu ya Chamwino ambao kwa sasa marashi ya Zanzibar yananukia.”

 

Akasema thubutu, nikamwambia ndiyo nakwambia.Shabiki huyu wa Yanga akaniambia sawa lakini mtu mwenyewe wa kanisani kila jumapili mambo ya mitala utayaweza? Nikamjibu nitamshirikisha Padri wangu, akanijibu mpaka ukamshirikishe. Wewe nihakikishie hapa hapa mimi nikiachika nije Chamwino Ikulu, alisema.




Kumbe mama huyu kwa chonjo walikuwepo vijana wake kadhaa ambao pia ni mashabiki wa Yanga wakinitazama kwa jicho kali, mmoja wapo akauliza,

 

“Sasa mzee mama yetu unamuhamishia Chamwino Ikulu kwenye marashi ya Zanzibar.”

 

Nikamjibu naam, Je mustakabali wa sisi watoto wake utakuwaje?Mama mtu alisema hapo wanangu umemuuliza swali sahihi kabisa, huyo baba yenu mtarajiwa

 

“Wewe tumekusikia ukipanga mikakati ya mama peke yake sisi wana je, tupe mustakabali wetu.”

 

Niliulizwa, Niliwaambia hawa watoto wajitahidi kuwa na heshima na mie baba yao kwanza ili nimalizane na mama yeo.Mama huyu akasema

 

 “Kama unataka picha basi kwanza tumalizane na mkataba wa wanangu  ili likitokea la kutokea na kama ulivyowasikia wanangu wameshasikia mimi na wanangu tutayafuata marashi ya Zanzibar yaliyopo Chamwino Ikulu, pumzi unayo?”

 

Niliulizwa Mwanakwetu sikupata bahati ya kupiga picha hiyo.Siku zikasonga Septemba 15, 2022 nilikutana na mama huyu kavaa nguo zake za rangi ya kijani na njano nilimtazama kwa jicho pembe lakini nilibaini hakupendeza kabisa, hata ile habari ya kumuhamishia Chamwino Ikulu nimeighairi.





 

Yeye akininanga kuwa nitaendelea kula wa chuya kwani nimeshindwa masharti nanikipenda boga nipende na maua yake.

Mwanakwetu Upo?

 

“Ukipenda Boga,Penda na Ua Lake.”

Nasema

“Ahlan Wa Sahlan.”

 

makwadeladius @gmail.com

 

0717649257


 



0/Post a Comment/Comments