ULIKUWA HAUNA NIDHAMU

 




 

Adeladius Makwega-MBAGALA

 

Siku moja nilitembelewa na ndugu yangu mmoja ambaye ni kapteni mstaafu, alifika nyumbani kwangu yeye na mkewe, nilifurahi mno maana ni mtu muwazi, mkweli , mshika dini yake na mwenye hadithi nyingi zenye mafunzo. Tukaongea mengi sana, tulipoyamaliza mazungumzo haya ndugu yangu huyu akaniaga. Kwa kuwa nyumbani kwangu nina miwa mingi, nikamkatia miwa kadhaa na kuifunga kama kuni, nikajitwika begani huku nikiwasindikiza wao mbele mie nyuma.

Tukiwa njiani, tulipita njia yenye makaburi kama matano ya ndugu wa familia moja ambayo yalikuwa yamejengewa vizuri sana, yakionesha ni makaburi ya Wakristo na ya Waisilamu. Ndugu yangu huyu akaniambia unayaona haya makaburi, nikamjibu nimeyaona kaka na kila siku ninayaona. Ndugu yangu huyu, akasema sawa Makwega unayaona lakini umeshawahi kufikiri mabingwa waliolala katika makaburi haya? Na simulizi za maisha yao?Zikoje? Mke wa huyu Kapteni Mstaafu anacheka. Nikamjibu hapana, ndugu yangu huyu akasema wewe ni mwandishi wa habari tena mkongwe, jaribu kufanya hivyo huku akiongeza haya;

 

“Kama kila kaburi lingekuwa linasimulia maisha ya marehemu aliyefariki duniani na kulala humo, basi duniani pangekuwa sehemu nzuri sana na salama kuliko ilivyo sasa.Pale kaburini pawe kioo kinasimulia, hapa duniani pangekuwa peponi.”

Safari inaendelea naye Mwanakwetu anacheka na mke wa jamaa anacheka.Jamaa huyu Msabato na mkewe wako mbele wamevaa saresare maua na simulizi hizi za makaburi zinaendelea. Nikamuuliza huyu bingwa kwanini umesema haya ? Jamaa akajibu akisema,

“Makwega, leo tumeongea mambo mengi sana, lakini ngoja nikusimulie kisa hiki cha mwisho.”

 

Kuna siku nilimpigia simu mheshimiwa mmoja, alipopokea simu yangu nikajitambulisha vizuri, nikimwambia mimi ni fulani bini fulani na tulifanya nawe kazi Tanga, kutokana na maelezo yangu mheshimiwa yule alinikumbuka, anasimulia ndugu yangu huyu. Wakawa wanawasiliana sana huku wakibadilishana mawazo na hali ya kisiasa ya Tanzania.

Kumbuka Mwanakwetu kabeba mzigo wa miwa anawasindikiz a jamaa na mkewe. Kwa kuwa ndugu aliyemtembelea Mwanakwetu kwao Butiama, kuna siku  akiwa huko alimtembelea mheshimiwa huyo ofisini kwake kumjulia hali katika mkoa mmoja wapo wa Tanzania Bara. Kweli alipofika hapo alimkuta mheshimiwa huyu akitekeleza majukumu yake ya kisiasa vizuri tu kama Mkuu wa Mkoa, wakaongea mengi. Ndugu yangu huyu akampongeza kwa kazi, akimwambia hongera sana mheshimiwa kwa kazi nzuri, naona unachapa kazi. Mheshimiwa huyu akajibu, -Asante, ehee ninachapa kazi vizuri sana na kazi hii inahitaji discipline (nidhamu), usipokuwa na discipline unafeli mapena sana.


 

Mheshimiwa huyu akamwambiwa ndugu huyu (kapteni mstaafu) hata wewe uliondolewa katika nafasi uliyokuwa nayo kwa kuwa haukuwa na nidhamu, kama ungejaliwa nidhamu hata kidogo mpaka sasa tungekuwa sote. Kapteni mstaafu anasikiliza kwa umakini mkubwa maelezo haya ya mheshimiwa alafu akasema ahaa kumbe nilikosa discipline! Ndiyo maana jamaa wakaniondoa? Kapteni mstaafu akasikitika mno huku akiwaza moyoni

Sikuwa na nidhamu?

Mazungumzo hayo yalipokwisha tu ndugu huyu akatoka ofisini kwa mheshimiwa na kurudi zake Butiama ambapo anajishugulisha na kilimo, akawa anaendelea na maisha yake. Mawasiliano yaliendelea vizuri sana, katika hali ya maisha msimu wa kilimo uliwadia, naye ndugu yangu huyu kapteni mstaafu hakuwa na mbegu bora za mahindi, akasema ngoja nimpigie mheshimiwa maana nilifanya naye kazi vizuri labda anaweza akaokoa jahazi.

Mheshimiwa kwema? Za huko? Naomba unisaidie laki mbili, nimekwama sana na msimu wa kilimo umefika ili ninue mbegu, nisikose kupanda msimu huu hata ukinichukulia mbegu katika duka la mbegu za kilimo utakuwa umenisaidia sana

Jamaa akajibiwa kuwa hiyo pesa ni nyingi sana sina na haiwezekani na hata duka la kupata mbegu hiyo halipo. Jamaa akamwambia mheshimiwa naomba hata unidhamini nikivuna mahindi nitakurudishia ! Mheshimiwa alijibu hawezi kufanya hivyo. Hadi mwisho Kapteni mstaafu hakupata laki mbili wala mbegu hizo kutoka kwa mheshimiwa huyu huku akipambana na maisha yake ya shambani. Maisha hayarudi nyuma, yaliendelea kama kawaida.

Baadaye mheshimiwa yule jahazi lake likazama, “tubwiiiiiiiii.” Kwa kuwa kapteni mstaafu ni mtu muwazi sana akachukua simu yake akampigia simu mheshimiwa huyu na kumpa pole.

Mheshimiwa kwema? Habari za siku? Mheshimiwa akajibu nzuri maisha yanaendelea kivingine na ni kama ulivyosikia jahazi lilizama. Ndugu yangu huyu akasema maneno haya,

“Si unakumbuka, mimi nilikwambia, mimi nilikuwa nimekwama, nikakuomba msaada haukunisaidia hata kidogo na wewe ukisema kuwa mtu akiondolewa huko huwa amekosa discipline, Je wewe hiyo nidhamu yako uliihamishia wapi? Sasa Ile discipline iko wapi?.”

Mwanakwetu mheshimwa huyu alikaa kimya kabisa hakujibu neno lolote, akakata simu na yeye kapteni mstaafu akaifuta namba ya mheshimiwa huyu saa hiyo hiyo.

 Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anamsindikiza kapteni huyu kupanda gari na miwa yangu begani. Kapteni akasema kama kila mmoja wetu aliyekufa kwa vipindi tofauti na kaburi lake likisimulia aliyoyapitia, kwa hakika dunia ingekuwa sehemu salama sana.

 


Kweli tulifika stendi naye kapteni mstaafu na mkewe wakapata basi na kuondoka zao na tita la miwa yao kutoka kwa Mwanakwetu. Na mie Mwanakwetu nilipokuwa narudi kwangu nikawa nakumbuka kisa hiki cha ndugu huyu na mheshimiwa, nikasema mtu aliye katika nafasi yoyote ile atambue kuwa yupo hapo kwa sababu ya Mungu kapenda awepo hapo kwa wakati huo katika nafasi hiyo siyo nidhamu, siyo kufanya kazi bidii au chochote kile, japokuwa kwa binadamu muugwana aliyelelewa na wazazi inahitajika sana kuwa na sifa hizo lakini siyo kibali cha wewe kudumu hapo ulipo.

 

Mwanakwetu Upo?

 

Kumbuka

“Ulikuwa Hauna Nidhamu”

 

makwadeladius @gmail.com

0717649257


 

0/Post a Comment/Comments