Adeladius Makwega-MWANZA
“Katika tasinia hii sasa inaajiri watu wengi maana haina watendaji wa kutosha kwa hatua zote, nyie mashuhuda, makocha wengi wa kilabu zetu kubwa wenye sifa si wazawa, wazawa ni wachache mno, hata mashuleni kuna walimu wangapi wa michezo wenye sifa ? Mathalani katika shule za msingi 21,000 za Tanzania na hata shule 6,000 za sekondari kuna walimu wangapi wa michezo wenye sifa hizo? Katika idara yetu ya michezo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu idara hiyo ianze imetoa wataalamu 1700 tu na Chuo chetu cha MCSD tangu kianze wahitimu wake hawazidi 2000, jamani mpira upo uwanjani kwetu jukumu letu ni kucheza tu, wazungu wanasema The ball is in your coat jukumu lako ni kuutoa kotoni na kucheza hapo tutafanikiwa. Hii tasnia inatoa mshahara mkubwa mathalani kocha katika timu zetu analipwa kati ya dola 2500-4000 kwa mwezi, hii ni pesa nyingi kwa Mtanzania na bila kodi, huo ni mshahara mkubwa tena sana. Hii Tasnia kama ukiamua kuitumikia hauwezi kupata shida ya vitu vidogo vidogo hapa dunia.”
Msomaji wangu haya ni maelezo ya Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya Dkt Jonas Tiboroha wakati akizungumza katika ufunguzi wa juma la utambulisho kwa wanachuo wapya wa taasisi hii ya umma mapema Novemba 11, 2024 hapa Malya Kwimba Mkoani Mwanza.
Hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa Dkt. Tiboroha aliyehamishiwa hapa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuja MCSD kuongeza nguvu katika taasisi hii ya umma ambayo sasa ina miradi mkubwa kadhaa inayokaribia Bilioni 40 za Kitanzania chini ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiendelea kuongea katika hadhara hii iliyokusanya wakufunzi kadhaa, watumishi kadhaa na wanachuo wa kozi za astashahda na stashahada za michezo karibu 350 Dkt. Tiboroha alisema,
“Chuo Cha MCSD wanafunzi wake wanafanya vizuri sana katika michezo na hilo nimelibaini nilipokuwa mhadhri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na sasa nawaombeni nyote mliopo hapa muilinde hilo kwa manufaa ya taasisi yetu.”
Akizungumza katika shughuli hii awali Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha Mkufunzi Denisi Kayombo alisisitiza malipo ya ada kwa wanachuo wote maana hilo litawasaidia mno kuweza kuondoa usumbufu wakati wa mitihani.
Kwa hakika mtayarishaji wa makala haya anatambua kuwa kwa sasa serikali imewekeza nguvu zake za rasilimali fedha na ujio wa Dkt. Tiboroha unaipiga kengele ya uwekezaji mwingine wa serikali kwa MCSD na huo ni uwekezaji wa rasilimali watu na kwa kumleta Daktari wa Falsafa katika tasnia ya michezo. Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kumleta mtaalamu wa michezo wa ngazi hiyo, kwa nafasi hii.
Mtayarishaji wa makala haya anaona wazi kuwa shabaha ni serikali ni nzuri na inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja wetu anayehusudu mafanikio ya michezo kwa taiafa letu, jukumu lililo mbele yetu ni kwa mtaalamu huyu wa michezo kupewa ushirikiano kwa MCSD yenyewe, kupewa ushirikiano na wadau wa michezo na kupewa pia ushirikiano kutoka serikalini hususani wizara husika hasa upatikanaji wa fedha za uendeshaji wa taasisi kwa wakati kufanikisha majukumu yote yaliyo mbele MCSD. Kwa Hakika mpira upo katika koti la kila mdau wa michezo jukumu ni kutoa mpira huo kotini na kuucheza ili kuyafikia mafanikio ya michezo.
Kandoni mwa haya kwa juma zima tangu Novemba 11-15 , 2024 MCSD ni juma la maelekezo kwa wanachuo wapya waliojiunga na chuo hiki kwa ngazi ya astashahada na stashahada ya michezo.
0717649257
Post a Comment