MUNGU ATAKASIRIKA



Adeladius Makwega- Kwa Omari KIjana-MOROGORO

“Mpaka sasa taarifa zinazojitokeza hazivutii, kwa matokeo yale, uchaguzi haukuwa mzuri, kwanza katika usimamizi na kutendeka kwa haki. Mathalani watu walivyolazimishwa kuandika karatasi za uchaguzi kwa ajili ya kuwapa kura watu wa chama tawala, hata watu mbalimbali hawakupiga kura, watu wameteswa.

Uchaguzi huu unatupa viongozi ambao hawakutokana na ridhaa ya wananchi, matarajio ilikuwa ni kuona mabadililko ya kisiasa na kutendeka haki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hii ni fikra ya watu wengi kutokana na  yale yalitokea huko nyuma, hakuna mabadiliko yalitokea.”

Msomaji wangu haya ni maelezo ya Sheikh Issa Ponda Kiongozi wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania ambaye ni miongoni wa viongozi wa dini ambao mara nyingi hutoa fatua ya mambo mbalimbali ya kitaifa bila ya kutafuna maneno, msimamo wake mara zote umekuwa ukijikita katika kweli.

Kumbuka hapa akitoa maelezo yake siku moja baada ya uchaguzi wa Serikali ya Mtaa kufanyika na matokeo yake kutangazwa. Maelezo ya Sheikh Issa Ponda yako wazi na amesema matokeo yaliyotangazwa hayavutii.


 

Swali ni je matokeo yenyewe yalikuwaje?

Kwa mujibu wa waziri wa Tanzania mwenye dhamana na uchaguzi huu kwa mwaka 2024 alinadi mbele ya vyombo vya habari kuwa CCM ilishinda karibu 99% huku CHADEMA ikiambulia nafasi ya pili kwa kuwa na viti visivyozidi 100, yaani CCM imeshinda makumi elfu , aliyefuta hakupata makumi elfu, hakupata maelefu hakupata mamia amepata viti katika makumi na vyama vingine vimeokotaokota tu katika makumi na mamoja.

Shekhe Issa Ponda katuambia pia hali ya matokep haya hairidhishi kama matokeo ya chaguzi zilizotangulia yaani wa mwaka 2019 na 2020 na hii ina tafsiri kwa uchaguzi Mkuu wa 2025 ambao mpishi wake anatambulika kama Tume Huru ya Uchaguzi ya Tanzania.


 

Swali lengine je hali ya Uchaguzi huo mwaka 2019 ilikuwaje?

Waziri mwenye dhamani na TAMISEMI wakati huo Mh Seleiman Jafo alinadi kuwa CCM ilishinda kwa 100% huku wajumbe ndani ya vijiji na mitaa vyama vya upinzani viliokotaokota kidogo.Kwa  hakika nakisi ya chaguzi huo inaonekana ni ile tu ya muwa wa uchaguzi pekee huu wa 2024 na ule ni wa 2019 lakini matokeo yake nakisi yake ni hafifu na iliyochujuka.

Mtayarishaji wa makala haya analo swali kwako wewe msomaji wake, je Sheikh Issa Ponda anavyosema matokeo hayaridhishi, kiongozi huyu wa kiroho anapiga fitna au anasimama katika kweli ya mzani ya haki?

Kwa hakika msomaji wangu jibu unalo. Hizo ndizo siasa za Tanzania na namna chaguzi zake zinavyofanyika.


 

Mwanakwetu katika kukupatia jibu sahihi la hili swali la mwisho, swali kitenda mimba la makala haya,  amemkumbuka kaka yake marehemo Richard Tambwe Hizza (Mbagala walipenda kumuita Baba Tulo/ Baba Agness wakati akiwa hai) 

Katika mojawapo ya mikutano yake akiwa katika jukwaa la CHADEMA aliwahi kutoa elimu ya urai kwa Watanzania  wenzake kwa kusema maneno haya.

“Wapo watu wachache ambao hawafahamu kwanini tuna fanya chaguzi, wakidhani uchaguzi ni wakati wa kutukanana na kubishana kijinga jinga, tuendelee kuwaelimsha waelewe.

Unapochagua kiongozi wa hovyo au unachagua chama cha hovyo umkomoi mtu, bali unajikomoa wewe mwenyewe.

Mimi sikumchagua Magufuli, Je Magufuli Rais wangu au siyo Rais wangu? Magufuli Rais wangu.

Sasa wanaposema wameshinda, eee wamemshinda nani ? Magufuli ni Rais wetu sote.Hapo ndiyo unatakiwa kutumia akili yako, mnarukaruka ohhh tumeshinda tumeshinda, umeshinda nani?Umemshinda nani?

Kibaya unasema tumeshinda huku viatu vya kuvaa miguuni hauna,hauna. Maisha yetu ya kimasikini, angalia nyumba zetu, mnajua nyumba moja wanakaa watu zaidi 40. Mnakaaje nyumba moja zaidi ya watu 40 !Na hiyo miaka zaidi 55 baada ya uhuru, tunaishi nyumba moja watu 40? Choo chenyewe kimoja , hali ngumu, ndiyo siyo (watu wanajibu ndiyooo?)

Kabla hajaingia Rais Magufuli Hospitalini ilikuwa bure, sasa hadi uwe na kadi, CCM awe na Kadi na CHADEMA awe kadi. Jamani tumieni akili, Mwenyeenzi Mungu atakasirika.”

Mwanakwetu Upo?


 


Kwa leo inatosha. Ngoja nimeze mate.

Kumbuka,

“Mwenyeenzi Mungu Atakasirika.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 



0/Post a Comment/Comments