TUIGE TABIA ZA MFALME YESU

 


Adeladius Makwega-DODOMA

Wakristo wameambiwa kuwa wanaposherehekea Sikukuu ya Kristo Mfalme wakumbuke tabia za Mfalme Yesu kuwa ni upole, upendo huruma,unyenyekevu,amani, msamaha na umasikini. Hayo yamesemwa na Padri Gidion Msigala katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata Parokia ya Chamwino Ikulu Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Novemba 24, 2024.

Akihubiri katika Ibada ya misa ya kwanza iliyoanza saa 12.30 ya asubuhi, Padri Msigala aliongeza ,

“Kristo Mfalme tangu anazaliwa alitambulishwa kama Mfalme katika Vitabu kadhaa mfano Ezekiel , Zakari , Injili na hata Malaika walinadi hilo. Swali ni Je Mfalme ni nani ? Mfalme ni mtawala wa watu wa eneo fulani. Hapa duniani tangu enzi za dola ya Rumi hadi sasa mataifa kadhaa yanahusudu kuitawala dunia kwa nguvu ya chuma lakini yameshindwa lakini jamani Kristo ndiye Mtawala wa Ulimwengu mzima.”

Padri Msigala aliongeza kuwa Sherehe ya Kristo Mfalme ilianzishwa na Baba Mtakatifu Pius wa XI kwa tamko maalumu liitwalo PALE PALIPO NA UPENDO mwaka 1925.

Akimalizia kwa kuupigilia msumari wa mahubiri yake Padri Msigala alisema kuwa katika dunia hii wapo Wakristo Mfalme wao ni Simu za mikononi, mwingine Mfalme fedha lakini akaambia Mfalme wa Kweli ni Yesu Kristo.

“Tiisheni vitu vyote kwa Yesu maana kumbukumbu zinaonesha hata wale wanasiasa dunia waliyokuwa wakimpinga na kumtenga Baba Mtakatifu Pius XI walikufa vibaya na ndiyo maana sasa hata Urusi Rais Putin anasali Kanisa la Oxhodox japokuwa ni Mkomunisti. Jamani katika kuadhimisha sikukuu ya leo katika mambo yote mkumbatieni Mungu.”

Awali akianza mahubiri ya Sherehe hii  Padri Msigala alikuwa mkali kidogo akiwaambia waamini wake kuwa anapotoa maelekezo ni vizuri wale wanaolekezwa kuyafuata, hakuna haja ya yeye kila mara kuyatoa maelekezo hayo hadharani. Kwa hakika nje ya Parokia hii hali ilikuwa ya utulivu, miti ikiendelea kuchanua chanua, wakulima wakitayarisha mashamba yao ambapo Wagogo wanaita Kubelega.


 

Mwandishi wa makala haya wakati anatoka Kanisani alikutana na ndugu Mengi Yoram jamaa mmoja mzaliwa wa Mpwawa alikuwa akiuza miiko ya kupikia chakula ambapo alisema biashara yake ni nzuri kwa siku anauza kati ya shilingi 15,000-25,000 lakini anakumbana na changamoto tatu; kutembea umbali mrefu kusaka wateja kwa miguu, kuwa mbali na familia na mwisho kudharauliwa na wanawake nakumuona yeye kama punguani akinadi kuwa yeye yupo timamu na ndiyo maana anakumbuka kusali kila alipo, akinadi kuwa wapo binadamu mfalme wao ni dharau.Mwandishi wa makala haya alipomuuliza ndugu Yoram yeye mfalme weke ni fedha ? Alijibu hapana anatafuta fedha ya kula tu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 








 

0/Post a Comment/Comments