Adeladius Makwega- Musoma MARA
Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi wa katuni mbalimbali kama zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji wa katuni hizo kutoka vyanzo mbalimbali.
Kuanza kulipiga kasia la makala haya Mwanakwetu anaivuta kwa heshima na taadhima katuni yake ya kwanza iliyochorwa na Said Mikaeli na kuchapishwa na Shirika la Utangazaji la Ujerumani ambayo inamuonesha jamaa aliyevaa sare kama za Jeshi la Polisi Tanzania huku akiwa na V mbili begani lakini zimecheza tiki taka.
Kwa Jeshi la Polisi Tanzania msomaji wnagu askari mwenye V mbili ni Kopro wa Polisi huku mwenye V tatu ni Sajenti wa Polisi naye mwenye V tatu na Bibi na Bwana huyu ni Stafu Sajenti wa Polisi, hili Mwanakwetu analieleza kwa faida ya msomaji wake tu.
Huyu Sajenti wa Polisi anapiga picha kwa kamera yake, alafu anasema mbona sioni mtu bali nasikia sauti tu? Haiba ya huyu Polisi anakitambi kikubwa huku kitambi hicho kinasababisha kutoona kinachoendelea mbele yake huku chini ya kitambi chake kuna jamaa mwenye jina la wakosoaji anapata kichapo cha uhakika kutoka kwa watu wasiojulikana, jamaa huyu asiyejulikana akinadi wewe unasema nini inatia doa!
Mchoraji wa hii katuni amejenga dhana ya Polisi kuwa na kitambi kikubwa na kutoshughulikia kabisa suala la watu wasiojulikana, nadhalia ya kitambi inajengwa tu na siyo kweli kwamba polisi wetu wote wana vitambi namna hiyo, japokuwa wapo wachache wenye miili kama hii, katuni hii inapaza sauti kwa polisi wetu kutimiza wajibu wao wa kumlinda raia na mali zake.
Mwanakwetu anatambua vijana wengi wa IGP Kamilius Wambura wako vizuri lakini kinachoshangaza kila siku inavyokwenda kwa Mungu watu wasiojulika wanatamalaki kwa kiburi bila aibu.
Mchoraji wa katuni hiii anatumia dhana ya kitambi ili kuwakumbusha wajibu wao Polisi wetu katika hilo na kama mambo ni magumu wakubwa wa Jeshi hilo wanayo nafasi nzuri ya kuachia ngazi kama alivyosema mzee Joseph Butiku. Katika hoja hii Mzee Joseph Butiku aliweka wazi kuwa kama mambo haya yanaendelea na wapo watu kwenye nyadhifa hizo wanao wajibu kuwajibika na wasibaki kufichama katika vyeo hivyo.
“Jamani eeh, mimi ninaona nimejitahidi kupambana na suala la watu wasiojulikana sasa ninaamua kuachia ngazi, niwapishe Watanzania wengine waje kulitafuta fupa hili.”
Hapo hapo atakuja kiongozi mwingine na yeye akikaa mwezi hali ikiendelea na yeye anang’atuliwa hapo hapo hadi mwisho tutamfahamu huyo anayevaa joho la watu wasiojulikana,Je ni nani na katumwa na nani?
Mwanakwwetu sasa anaikamata katuni ya pili ambayo inawaonesha nyumbu /Nyati wanataka kuvuka mto, nyumbu hawa wako wengi na huku mto huu ukiwa na mamba kadhaa. Nyumbu wako njia panda je wanaweza kuvuka mto huo wenye mamba tele? na wote kuvuka salama?
Nyumbu mmoja anasema hao mamba wako sita tuvuke wataliwa sita na wengine watabaki salama ili tuendelee na safari. Nyumbu wa pili anauliza ee bwana unahakika wapo mamba sita na nyumbu wa tatu anasema nani aanze?
Maswali hayo matatu tuvuke wataliwa sita , unahakika wapo sita na nani aanze? ndiyo kikwazo cha nyumbu hao kuvuka mto huo.
Kwa hoja hizo nyumbu hawa hawawezi kuvuka mto huo huku watabakia hapo hapo wakipiga maki time tu. Kibaya zaidi linaweza kutokea kundi la simba na mwitu na kuwavamia na kuliwa nyumbu kadhaa. Nyumbu hawa wanasahau kuwa adui yupo pahala popote, ni heri ya adui unayemuona kuliko adui sirini.
Mwanakwetu anaendelea kupiga kasia la makala ya katuni kwa kuikamata katuni ya nne ambayo inaonesha Kivuko kinavuka upande mmoja kwenda upande wa pili kwa hakika upande mmoja ni Magogoni na ule upande wa pili ni Kigamboni Dar es Salaam.
Hapa panaonekana Kivuko kimejaza watu wengi, kwa kando kipaya na mwanae wapo baharini wanaogelea mtoto wa kipanya anauliza eti baba Kigamboni nayo Tanzania?
Kipanya anamjibu mwanawe kuwa hana hakika kama Kigamboni nayo ni Tanzania. Mwanakwetu anaomba amsaidie mtoto wa Kipanya lakini sharti amchagulie mji na Mji wenyewe lazima uwe Wete Pemba.
Swali hilo lingenoga kama lingeulizwa, Kigamboni nayo Tanganyika?
Jibu lake ni kuwa Kigamboni, sehemu kubwa ya Dar es Salam zile KM 14 za tangu usawa wa bahari kwa asili ilikuwa mali ya Zanzibar ya Sultani lakini baadaye maeneno haya Sutani aliyauza kwa watawala wa Tanganyika ikiwamo Kisiwa cha Mafia.
Haya ilikuwa kabla ya Mkutano wa Berlini.
Nikuchekeshe msomaji wangu,
Mwanakwetu anaye rafiki yake Mzanzibari anaitwa Hafsa Omari Binti Jumaa ambaye Baba yake alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna wakati Mwanakwetu alikuwa anataniwa na Bi Hafsa Omari Jumaa, binti huyu akamwambia Mwanakwetu maneno haya ;
“Watanganyika mkisema kuuvunja muungano ninawakumbuka KM 14 kutoka usawa wa Bahari, upande wa Tanganyika, hii Posta yote, Oystebay yote, Ikulu yote ya Magogoni, Kariakoo yote na lle kurasini na Kigamboni yote ni Zanzibar, Watanganyika mko tayari?”
Mwanakweu akajibu Sultan alishakula pesa, kwa hiyo sasa ni Tanganyika, huku Zanzibar haina chake.
Sasa Mwanakwetu anaikamata katuni ya mwisho ambayo imechorwa na King Kinya inamuonesha jamaa mwenye nembo ya 2019 akiingia katika chumba cha Novemba 27, 2024 ikimaanisha chumba cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao umemalizika hivi karibuni.
Mchoraji wa katuni hii anampinga dongo Waziri wa TAMISEMI wa sasa kuwa hali ya uchaguzi huo haitofautiani na uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019. Unapotupia jicho juu ya takwimu za matokeo haya kwa hakika hazina tofauti kubwa.
Kikubwa haya ni mambo ya watu kama yapo madhaifu yafanyiwe kazi mapema ili kuepusha malalamiko yasiyo na maana na tija kwa Watanzania wengi.
Basi hadi hapo ndiyo na mimi natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo, mikononi mwangu nilikuwa na katuni nne ; ile ya askari mwenye kitambi, ya pili ni ile ya nyumbu wakitaka kuvuka mto wenye mamba sita, ya tatu ni ile ya Kigambini nayo kama ni Tanzania? Nayo katuni ya nne ni hii ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“2024 Kama 2019”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment