Adeladius Makwega BUNDA
“Tulienda kwa jamaa wanaouza vyuma chakavu, tukampa shilingi 10,000/= ya Tanzania, akapekua kwa nusu saa kisha akaja na vyama viwili chakavu; kimoja ni ringi la gari dogo na kimoja kipande cha nondo, akavigongesha mara nne na kutoa mlio wa kengele, tuliridhiswa nao, nikasema naam hivi vyuma vinafaa na tumepata kengele.
Tukabeba kwa bodaboda hadi hapa shuleni, tukaifunga na sasa ndiyo kengele yetu, imeshakaa katika mti huu wa mwembe uliokauka kwa mwaka mmoja .”
Hayo yalikuwa majibu ya swali kutoka kwa Mwanakwetu kwa mwalimu mmoja aliyekutana naye Wilayani Bunda ambaye Disemba 29, 2024 alikuwa katika usimamizi wa ujenzi wa shule yake, akijiandaa kupokea wanafunzi wa Kidato cha kwanza mapema Januari 2025.
“Mwalimu hii kengele mliitoa wapi?”
Majibu ya swali hilo yalimpa tafakari mno Mwanakwetu juu ya umuhimu wa kengele shuleni lakini pia na namna inavyopatikana na sasa ndiyo swali hilo linayajenga makala haya.
Swali la kujiuliza ni je kengele shuleni inafanya kazi gani?
“Mlio wa kengele ya shuleni ni ishara ya kutangaza na kuujulisha umma nyakati muhimu kwa wanafunzi na wafanyakazi wa shule, kama vile kuashiria mwanzo na mwisho wa siku ya shule, vipindi vya darasa, mapumziko na hata dharura na hata ugeni.”
Katika baadhi ya shule kengele inaweza kuchukua umbo la kengele halisi kama ile kengele ya ringi la gari aliyokutana nayo Mwanakwetu hapa Bunda, kwa maeneo mengine zipo kengele zinazoendeshwa kwa umeme. Katika shule nyingine inaweza kuwa inatoa tu toni, king'ora, sauti ya kengele ya kielektroniki, mfululizo wa kengele, au muziki unaochezwa kupitia mfumo wa mawasiliano PA na hata wengine hutumia miruzi na makofi yanayopigwa na binadamu, haya matumizi ya makofi kama kiashiria cha matukio shuleni kinatumika nchini Somalia.
“Katika shule za walemavu wa kusikia, wao hutumia mbinu mbadala za kuashiria mlio wa kengele, kwa mfano lugha ya ishara kutoka kwa mwalimu na taa zinazomulika wakati anwani ya umma/kengele inapigwa.”
Kwa tulio wengi tumsomea shule kadhaa mathalani Mwanakwetu amesoma shule za Msingi Kimanzichana na Mkuranga mkoni Pwani , pia amesoma Mnazi Mmoja na Mtoni Kijichi mkoni Dar es Salaam na kwa hakika mfumo wetu wa kusoma kengele zilizotumia kujulisha muda zilipatika kutoka katika vyuma chakavu-kengele za kuokota .
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Swali ni je yupo hata mmoja miongoni mwetu, miongoni mwetu amewahi kukumbuka maboresho ya kengele ya shule yake iliyomsadia tangu wakati ule herufi zinapiga tiki taka, herufi zinapiga tiki taka na hadi leo hii mwandiko umekaa vizuri na anaonekana ni msomi mkubwa?
“Kwa hakika sasa shule ndiyo zinafunguliwa, hivi punde na kwa hakika serikali inafanya maboresho makubwa ya elimu lakini suala la kuhama kutoka kengele za kuokota na kwenda kengele za kietroniki bado tutumie muda huu kukumbuka maboresho ya kengele za shule zetu nchi nzima ili tuondokane na kutumia vyuma chakavu.”
Kumbuka kwa sasa jamii na Serikali nchini Tanzania inawekeza mno katika majengo ya taasisi zetu zote za elimu lakini suala la kengele bado halijatazamwa, bado hatujajaliwa kufanyia maboresho na Mwanakwetu kwa makala haya anayatumia kuikumbusha jamii juu ya maboresho ya kengele zetu, huku Mwanakwetu akiipiga mbiu ya mgambo ya safari ya kuhama kutoka vyuma chakafu, kengele za analojia na kwenda kengele za digitali.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Mwalimu Hii Kengele Wapi Mliitoa?”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
NB Makala haya yametayarishwa na MwAnAkWeTu wa heshima ya Shule za Msingi Kimanzichana na Mkuranga, Mkoani Pwani pia Shule za Msingi Mnazi Mmoja na Mtoni Kijichi Dar es Salaam ambapo zote alisoma tangu darasa la awali hadi darasa la saba kati ya mwaka1983-1990
.
Post a Comment