Adeladius Makwega-Musoma MARA
Msomaji wangu nakualika kwa mara nyingine katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi wa katuni mbalimbali mara baada ya kuziteua katuni nne miongoni mwa katuni kadhaa kutoka kwa wachoraji mbalimbali. Awali ya yote katuni hizo moja moja, kwanza inaelezewa namna ilivyo kisha kufanyiwa uchambuzi wake makini kwa jicho la mtayarishari wetu.
Kuanza kuukwea mnazi huu mrefu kuliko wote wa makala haya ya katuni siku ya leo , huku nikipanda ngazi yake ya kwanza, nakutana na katuni moja iliyochorwa na King Kinya , huyu ni miongoni mwa wachoraji maarufu wa vikaragosi hapa Tanzania. Katuni hii inamuonesha mtu kama mhe Januari Makamba, Mbunge wa Bumbuli huko Lushoto Mkoani Tanga.
“Bwaaa Shehe…. Bwaa shemeji.”
Hapa mheshimwa Makamba anaonekana kama amebeba vibatari kadhaa akivitoa kutoka eneo moja na kuvipeleka eneo lingine. Vibatari hivyo na pasi ya mkaa juu yake vimepachikwa katika kapu mithili ya pakacha, cha kustajabisha vibatari vinadondoka chini kimoja baada ya kingine.
Msomaji wangu tambua kuwa juu ya hii katuni mchoraji wake King Kinya kapachika maneno POWER CUT yaani ule MKATIKO WA UMEME. Katuni hii ilichorwa kitambo wakati mh Januari Makamba alipokuwa Waziri wa Stima wa Tanzania, hadi sasa mkatiko huo wa stima hapa Tanzania bado upo pale ple, huku baadhi ya watu tuliyokuwa tunaamini kuwa shida ya mkatiko wa stima ni mh Makamba sasa tunaamini vinginevyo , kumbe tulikuwa tunakosea.
Mwanakwetu anapoitazama katuni hii kwa umakini mkubwa anajiuliza hivi vibatari vine vilivyochora vikiporomoka kutoka katika kapu la mh Makamba vinamaanisha nini kwa hivi sasa?
Kwa hakika jibu lake ni hili
“Mh Januari Makamba, Mtanganyika anayezaliwa na baba Msambaa na mama Mhaya ni miongoni mwa wabunge wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyerejeshwa Uwazirini mara baada ya kifo cha Rais Magufuli mwaka ule wa 2021, alikaa katika uwaziri huo tangu 2021, 2022,2023 na 2024 ndipo akapigwa mkasi.
Vibatari hivyo vinne ni miaka 2021, 2022, 2023 na 2024 ambapo badaye Rais Samia Suluhu akampiga mkasi na hivyo hivyo Rais John Magufuli alifanya kazi na Januari Makamba kwa vipindi hicho hicho cha miaka minne. Ndiyo kusema Mtanganyika huyu yeye ni mzee wa miaka mine mine tu.”
Kwa jicho la Mwanakwetu,
“Katuni hii ya Kingi Kinya inabainisha wazi kuwa mh Makamba japokuwa vibatari vyake vine vimelamba sakafu ardhini, mafuta yamemwagika, huku waliyo kando wanapoliwa na kupiga chafya kwa harufu ya Keresene Mungu bahati kapu la mh Makamba limejaa vibatari tele ambavyo vitatumika kutoa mwanga hapo mbeleni hasa kwa makabwela maana sisi ndiyo watumiaji wa vibatari.”
Safari ya kuukwea mnazi huu mrefu wa makala ya katuni inaendelea na sasa ninakutana na katuni ya pili ambayo imechorwa tena na King Kinya , kunaoneka jamaa aliyevalia koti jeusi na tai juu yake, huku akipewa kibandiko kama TUME HURU hii ni ya uchaguzi nchini Tanzania. Jamaa huyu wa tume huru mfukoni kwake kabeba katiba ya CCM huku akimkamata jamaa mwenye sare za CHADEMA akimning’iniza hadi juu na huyu jamaa wa CHADEMA wajihi wake ni mithili ya Tundu Lissu- Makamu Mwneyekiti wa CHADEMA taifa.
Jamaa wa tume huru anavyoonekana ati akitoa elimu ya namna ya kuomba kura huku akiorodhesha mambo kadhaa anayotaka wapinzani kuzingatia. Akitumia namba za kiarabu yaani moja, mbili na tatu.
Mtayarishaji wa makala haya anapoitazama katuni hii kwa umakni anaibua hoja kuwa ,
“Ebooo Tume Huru ya Uchaguzi, haiwezi kuwaelekeza namna bora ya kuomba kura vyama vya siasa. Kikubwa kwao ni kusisitiza kufuatwa sheria na kanuni zake tu. Nayo ile katiba ya CCM mfukoni inapaswa kuondolewa kwa ndugu huyu wa tume huru maana hawapaswi kuwa na upande.”
Mwanakwetu anaendelea kuupanda mnazi huu mrefu na sasa ameshafika robo tatu yake, hapa anakutana na katuni ya tatu iliyochorwa na King Kinya tena , mandhari ya jamaa yu kaburini akitoa mchozi mzito, kaburi hilo lenye marumaru nyeusi limepewa jina CHATO na huku anayelia kando ya kaburini hili ni jamaa mwenye shati la kijani na suruali nyeusi , akilia machozi mazito mazito huku akinadi ,
“Tunakukumbuka Mwalimu Nyerere. Tunakukumbuka Mwalimu Nyerere., Tunakukumbuka Mwalimu Nyerere.”
Kwa jicho la mtayarishaji wa makala haya anasema haya,
“Matumizi ya neno CHATO katika kaburi hilo inamaanisha kuwa kaburi hilo ni la Rais wa Awamu ya Tano John Magufuli lakini mchoraji anazuga kwa kutoa maneno kuwa analia kwa sauti anamtaja mwalimu Nyerere mithili yu Butiama.
Hiyo ni geresha na ni dangnya toto kula kunde mbichi., akifanya hivyo kuficha umma usitambue kuwa kama anayemlilia ni John Pombe Magufuli.”
Swali ambalo Mwanakwetu anajiuliza akiwa juu mnazi wake kuwa inakuwaje huyu jamaa analia kwa mficho? Kwanini kumlilia Nyerere hadharani hakuna madhara na kwa nini kumlilia hadharani John Pombe Magufuli kuwe na madhara?
Makala ya katuni yana majibu haya,
“Kwa hakika ndani ya CCM ziko kambi kadhaa mojawapo ni ile iliyo benchi ambayo inayakumbuka mema na mazuri ya John Pombe Magufuli, huku wakijipa upofu wa mabaya ya Mzee Magufuli. Kwa kufanya hivyo siyo kosa kwani hata rais wa sasa atakapotoka madarani jamii itayakumbuka mazuri yake.
Watanzania tusiwe waoga kulia wazi wazi, iwe kwa makaburi ya somo wetu, makabauri ya wazazi wetu , makaburi ya ndugu zetu na hata katika makaburi ya viongozi wetu kama vlle mwalimu Julius Nyerere, Sheikh Abeid Karume, Ali Hassan Mwinyi, Edward Sokoine, Benjamin Mkapa na hata kwa John Pombe Magufuli.”
Mwanakwetu sasa amefika kileleni mwa mnazi wake, huku mkono wake wa shoto umekamata katuni yake ya mwisho iiyochorwa na alwaatani Masoud Kipanya, ikionesha Kipanya aliyevalia viatu vyeusi, surualli nyeusi na shati mithili ya kijani, ameketi chini, amechoka huku akiegemea ukuta, mguu wa kulia akiunyoosha chini na mguu wa shoto kaukunja juu, yupo hoi bini taabani kama katoka safari ya mbali
Akilini mwake Kipanya anajliuza swali hili,
“Je huu ni mwanzo wa mwisho?”
Mtayarishaji wa makala haya alitumia muda kidogo kupata tafsiri mficho ya katuni hii lakini muda iliyochorwa inatoa taswira kuwa mchoraji wake anayatazama na kuyatilia maanani mambo kadhaa ya Tanzania, huku akipuliza tarumbeta lake kwa sauti kubwa hususani hali ya mazingira ya Tanzania ya mwaka wa 2024 kuelekea 2025 na changamoto kadhaa zinazilikabili taifa hili, huku akiibua hoja kwa swali kuwa chama tawala huo ni mwanzo wa mwisho wake?
Mwanakwetu kwa katuni hii anaamini haya,
“Kwanza chama tawala kujiuliza ni sahihi, maana inaweza kusaidia kupatikana majibu ya baadhi ya mambo kwa wakati ikiwamo suala la watu wasiojulikana ambalo ni habari ya mjini.
Hapa kuna matumaini yaliyochujuka, je swali hili kama chama hiki kinajiuliza? Kwa hakika majibu yatapatikana na mambo yanaweza kuwa mazuri.
Hoja ya msingi je kama hawajiulizi inakuwaje?
Jibu lake ni kuwa katuni hii ya Masoud Kipanya inakumbusha hilo na hata makala Mwanakwetu haya ni sehemu ya kuwakumbusha hilo.”
Mwanakwetu kumbuka yu kileleni akaangua nazi zake kadhaa na kushuka nazo chini , akazifua kisha kurudi nazo kwake.
Mwanakwetu Upo?
Hadi hapo ndiyo nayafunga makala haya ya katuni, siku ya leo nilikuwa na katuni nne ya kwanza ni ile ya Mbunge wa Bumbuli na kapu la vibatari vyake, katuni ya pili ni ile ya tume huru ya uchaguzi na namna ya kuvifundisha vyama vya siasa kuomba kura, katuni ya tatu ni ile ya Kilio Kaburini kule CHATO na katuni ya mwisho ni hii ya swali la Kipanya .
Kumbuka,
“Ni Mwanzo Wa Mwisho.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment