Adeladius Makwega-Musoma MARA.
Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi yanayokuchagulia katuni nne , kila moja ikielezewa na kufanyiwa uchambuzi kwa jicho la mtayarishaji wetu.
Kuyaanza makala haya ninaikamata katuni namba moja iliyochorwa na Masoud Kipanya ambapo kunaonekana watu wawili katika mazingira mawili tofauti; mkono wa kulia yupo mama mmoja anaongea na bintiye;
“Binti yangu, Mwanaume asikusumbue.”
Upande mwingine yupo baba na kijana wake;
“Kijana wangu Mwanamke asikusumbue.”
Kwa hakika katuni hii kila mzazi anavutia upande wa jinsia yake, huo ndiyo ubinadamu. Kikubwa Mwanakwetu anachoweza kusema ili watu wakae pamoja lazima kila upande uwe makini ili kufanikisha maisha ya pande mbili , yaweze kusonga kwa amani, maisha ya binadamu yanahitaji uwepo wa wengine.
Mwanakwetu katuni hii inambeba hadi mwaka 2009 alipomtembelea Mchungaji Dkt Eberhardt Ngugi ambaye alikuwa Mchungaji wa Usharika wa Makolola Tanga KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambaye baadaye msomi huyu wa Teolojia aliwahi kuwa Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi hii enzi za Askofu Dkt Stephern Munga, katika ibada ya jumapili hii ya mwaka huo aliyosali Mwanakwetu akiwa na rafiki yake na Mwanafunzi wa Uchungaji wakati huo ambaye sasa ni Mchungaji Paulo Diu , Dkt Ngugi siku hii alinukuu kitabu cha Waefeso 5:22-33.
“Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana. Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake. Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote.
Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake. Alifanya hivyo ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji, kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safi kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo. Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.
(Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa, maana sisi ni viungo vya mwili wake).
'Kwa sababu hiyo, mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja.” Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake. Lakini yanawahusu nyinyi pia: Kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.'
”
Kwa hakika Mwanakwetu anasema kama hautaki hilo, basi uamue kukaa mwenyewe na uwe mtawa hadi kifo, kwa haya Mwanakwetu hana la kuongeza maana Dkt Ngugi kutoka Usambaani ambaye ana PHD ya Teolojia yeye amemaliza kila kitu.
Dkt E Ngugi.
Mwananakwetu anaikamata katuni ya pili ambayo imechorwa na Saidi wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW KISWAHILI hapa kunaoneka Guta likiwa limebeba magogo yaliyovumwa msituni huku nyani na kima wakiwa juu ya magogo haya. Sasa hapa juu ya guta yupo kima akisema kwa namna mnavyoharibu mazingira yetu na ndiyo na sisi tunavyoweza kuhamia huku mlipo.
Katuni hii inazungumzia juu ya uharibifu wa mazingira huku mamlaka zikikumbushwa kutimiza wajibu wao.
Mwanakwetu anaikamata katuni ya tatu iliyochorwa na King Kinya.jamaa wawili wamekaa katika sofa LOVE SEAT, hii kochi la watu wawili maana sofa zipo za aina tatu, la mtu mmoja mmoja, la watu watatu watatu na pia la watu wawili waili hii ndiyo LOVE SEAT, haya mambo ya Keko Furniture.
“Mmoja mmoja, watatu watatu au LOVE SEAT maana yake wawili wawili.”
Watu watatu , jamaa wa Love Seat na jamaa mmoja aliyesimama aliyevaa shati la kijani wanaangalia runinga,kinachoonekana ni mpambano wa kura, nadhani nafasi ya uchaguzi wa mweneyekiti wa CHADEMA Taifa kati ya Mbowe na Lissu . huku vikisikika vishindo. Huyu jamaa aliyesimama akiwa amevaa shati la kijani yaani CCM anashangilia mno.Kwa hakika katuni hii hakuna haja ya kuieleza haya ni mambo ya siasa za Tanzania baina ya CHADEMA na CCM kuelekea CHADEMA kumpata mwenyekiti wao mpya.
Mwanakwetu anaikamata katuni ya nne hii imechorwa na Gado ni katuni ya mwaka wa 2021 ikimuonesha mama mmoja yupo kwa tabibu wa macho akisoma maandishi ambayo yamebandikwa Katiba Mpya. Mama huyu anayasoma kwa tabu maandishi hayo maana yake haoni vizuri, gafla mama huyu anasema tafadhali Daktari naomba unipe muda.
Kwa uhakika mchoraji wa katuni hii alikuwa anamkumbusha mama huyu mwenywe wajihi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania juu mahitaji la Katiba Mpya nchini Tanzania.
Kutokana na katuni hii Mwanakwetu amekumbulka hoja hii.
“Je, ni hali gani ya sasa ya nafasi ya kiraia - uhuru wa kujumuika, kukusanyika kwa amani, na kujieleza nchini Tanzania?”
Hilo ni swali lililopo katika makala iliyoandikwa na Maria Sarungi ambaye ni mwanahabari Mtanzania, ambapo Mwanakwetu akiwa mwanafunzi wa Tambaza enzi hizo anakumbuka jina la Maria Sarungi alikuwa Dada Mkuu pale Zanaki Sekondari ambapo simulizi za huyu dada mkuu iko siku Mwanakwetu atazismulia.
Maria Sarungi alijibu swali hili kupitia-mtandao wenye anuani hii-
https://www.civicus.org/index.php/media-resources/news/interviews/5269-tanzania-what-is-needed-is-a-new-constitution-reflecting-the-will-of-the-people
Mwanakwetu huu ni utangulizi wa jibu la swali hilo kutoka kwa Dada Mkuu wa zamani wa Zanaki Sekondari.
“Nafasi ya kiraia inaendelea kuwekewa vikwazo, kwani mfumo wa kisheria haujabadilika. Marekebisho yamependekezwa kwenye Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) za 2020, ambayo yamesababisha vikwazo vikali vya uhuru wa kujieleza mtandaoni na uhuru wa vyombo vya habari vya dijitali. Hata hivyo, marekebisho haya ni habari njema chache, kwa vile masuala muhimu kama vile kuharamishwa kwa kile kinachochukuliwa kuwa 'habari bandia' au habari potofu bado yamesalia na mamlaka imebaki na uwezo wa kiholela wa kuchukua hatua na kuondoa kile kinachoitwa 'maudhui yaliyokatazwa' ndani. saa mbili.
Orodha ya maudhui yaliyokatazwa, ambayo ni wazi kwa tafsiri na ambayo yamekuwa yakitumika kuzuia uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza hapo awali, imesalia.Kuhusu uhuru wa kukusanyika kwa amani, vikwazo vimekuwa vikali zaidi kiasi kwamba mikutano ya ndani ya vyama vya siasa sasa imepigwa marufuku(ilipigwa marufuku) na hata kuvurugwa na polisi wa kuzuia fujo.”
Kwa hakika matakwa ya katiba mpya yapo mengi, Maria Sarungi yeye amejaliwa uwezo wa kuandika na ameyaandika hayo lakini vipi wale wanaohitaji Katiba Mpya lakini hawana uwezo wa kuandika?
Kwa hakika msomaji wangu naomba kwa hisani yako nikuache na swali hilo.
Mwanakwetu upo?
Basi msomaji wnagu hadi hapo ndiyo natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo, nlikuwa na katuni nne ile ya asikutishe mwanaume na asikuitishe mwanamke, katuni ya pili ni juu ya uharibifu wa mazingira na nyani na kima kuhamia mjini, katuni ya tatu ni juu ya vita katika uchaguzi wa mwenyekiti wa CHADEMA baina ya Mbowe na Lissu na shangwe ya jamaa wenye mashati ya kijani, katuni ya nne ni hii ya Dokta Naomba Unipe Muda.
Kwa katuni hizonne ndiyo na mimi naufunga ukurasa huu wa makala ya katuni siku leo
Kumbuka
“Naomba Unipe Muda”
Nakutakia Mwaka Mpya Mwema.
0717649257
Post a Comment