NDIYE MTEGUZI WA HIKI KIGUGUMIZI

 


Adeladius Makwega Musoma-MARA

 

“Leo mwalimu wetu kacheka mara nne, jana mwalimu kacheka mara tano na juzi kacheka mara saba. Mbona leo kacheka kidogo? ”

 

Hayo yalikuwa maneno ya kawaida mno ya wanafunzi darasani kwetu.Mawazo yangu ya utoto nilidhani kuwa huko Marangu wanawake wote ni warembo, lakini sijapata sijawahi kufika huko pengineni kweli na hata tulipokuwa tunacheza michezo ya kujipikilisha nyumbani, kijana mmoja aliyekuwa na pacha wake alikula kiapo hadharani kuwa ataenda kuoa huko Marangu. na mie Mwanakwetu nililiunga mkono hilo mia kwa mia kwa kuwa mwalimu wetu wa darasa alikuwa mfano na mwakilishi wa wanawake wote wa Kichaga. Kama ilikuwa taasisi basi ilikuwa imekamilika kila idara.Jambo la kushangaza wale pacha, pacha wa kike kaka yake alipokuwa akifanya kosa darasani akichapwa na mwalimu huyu hakukasilika hata kidogo. Mwanakwetu na hawa pacha wako darasa la tano mkondo A.Darasa la letu lilikuwa na wanafunzi 100, huku kukiwa na mikondo miwili ya A na B. Mwalimu wa darasa letu alikuwa binti wa Kichaga ambaye alikuwa akijipenda sana huku wanafunzi wengi wa kike wakiwa na mawazo ya kuwa kama mwalimu wao wakimaliza shule.

 

Mwalimu huyu alikuwa mrefu, mwenye mwili uliojengeka huku akiwa si mwembamba au mnene, rangi yake ni maji ya kunde, alikuwa na mwanya ambao ulionekana vizuri pale alipocheka, huku kicheko chake kilikuwa kikisubiriwa sana na wanafunzi wa darasa letu pale aingiapo darasani. Darasa letu lilijaliwa kuwa na wanafunzi wa aina zote, wapole, watulivu na watundu. Nao wanafunzi watundu akina Mwanakwetu walikuwa wakiweza kuhesabu vicheko vya mwalimuhuyo kila aingiako darasani.Mwalimu wetu mrembo akisimama mstarini tuliwaringishia wanafunzi wenzetu kuwa mnamuona mwalimu wetu ! Huku wanafunzi wengine wakitamani kufundishwa na mwalimu huyu wa Kichaga. Siku moja tukiwa tumeshamaliza mitihani ya mwisho wa mwaka tukisubiri shule yetu kufungwa na huku walimu wa madarasa wakiwa bize wakitayarisha ripoti zetu. Walimu wengine wakitugawia mitihani yetu.


 

 

Basi tulijulishwa kuwa darasa la tano A twendeni darasani tukagawiwe mitihani hiyo. Kweli tuligawiwa mitihani hiyo vizuri. Mwalimu wa kwanza alienda zake nasisi tukibaki kusubiri, mwalimu mwingine aje kutugawia mitahani mingine.Tukiwa tunacheza darasani mara binti mmoja, ilishanga kumuona kuwa sketi yake imetapakaa damu. Binti yule pacha aliibuka nakupiga kelele,

 

“Jamani njoni mumuone.”

 

Kweli jambo hilo lilikuwa la hatari wanafunzi wote wakajaa, wakishangaa hilo huku wengine wakilia kuwa mwezetu anaweza kupoteza uhai muda wowote ule wengine walichukua kanga kutoka nje kwa akina mama wnaofanya biashara na kumpatia na kisha alifika mwalimu wetu wa darasa na sote kutolewa nje.

Sisi tulikalishwa katika mwembe huku akija mwalimu mwingine na kutugawia mitihani na binti Yule tukaambiwa alipelekwa nyumbani kwao na mwalimu mmoja wa kike. Baada ya muda, tukiwa katika mwembe huo aliitwa nabinti pacha na mwalimu huyu wa darasa katika ofisi ya walimu kadhaa wa kike, kumbuka mwalimu wa darasa ni Binti wa Kichaga.

 Kilichoendelea huko ofisini binti pacha alisimulia hiki,

 

“Nilikaribishwa na mwalimu darasa Mchaga ninayempenda kwa bakora kadhaa ambazo sikuelewa kuwa ninachapiwa nini? Jambo hilo liliniuma sana na sana, mimi nilidhani nimefanya jambo la utu na la kiungwana kwa mwezangu aliyeumia kuwajulisha waje kumuokoa, kumbe nimefanya kosa? Nilirudi nyumbani huku nikiwa nimekasirika mno. Tulipofika nyumbani. Baba yangu mzazi aliniuliza binti yangu mbona leo umekasirika sana kulikoni? Nilijaribu kumueleza lakini hakunielewa kwa kuwa nilikuwa na kaka yangu pacha yeye alilieleza tukio lililotokea darasani na namna wanafunzi wenzangu walivyomwaambia walimu na nilivyocharaza bakora.Baba alisema sawa akasema kuwa anagemfuata mwalimu huyo na kumueleza juu ya tukio hilo lililotokea, hapo kidogo hasira zilipungua. Kweli baba alimueleza mwalimu huyu ambaye nilikuwa nampenda sana lakini sasa mimi nilishamchukia mno na roho yangu ilishaingia nyongo naye, hata kaka yangu pacha nikimwambia kuwa ukiwa mkubwa usiwaoe Wachaga kwa kuwa wanawachapa wanafunzi bila kosa.”

 

Mazungumzo ya baba na mwalimu yalifanyika huku na kweli tulipofungua shule tuliingia darasa la sita na walikuja walimu maalumu kutufundisha juu ya Barehe na Kuvunja Ungo. Hapo ndipo tulipoelewa kuwa lile tukio la binti pacha kuwaita wenzatu kuja kushangaa lilikuwa ni kosa.Masomo yalimalizika huku hata yule dada ambaye tukio hilo lilimkuta alikuwa rafiki mno yetu mno na cha kushangaza miaka michache baada ya kumaliza shule alikuja kuolewa na binamu ya huyu dada pacha na hivi sasa wana watoto watatu na wajukuu

 Binti Pacha alisema,

 

“Hata ile chuki yangu ya kucharazwa viboko na Mwalimu wangu wa Kichaga ikapotea baada ya kugundua kile kilichotokea. Mwalimu huyu alizungumza na mama kuwa huyu mwezatu aliwahi kupevuka mapema, kwa hiyo mimi nilikuwa mdogo na sikufahamu kilichotokea na tulimchapa ili tukio kama hilo likitokea tena lisijirudie tena na kumuelekeza kwa wakati ule haukuwa wakati sahihi.Kweli chuki na Wachaga ikaondoka na hata kaka yangu(pacha wangu) alimuoa mama wa Kichaga huko Marangu sasa ni mke na mume na wana watoto wawili.”

 

Mwananakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Shule hii haikuwa na chochote cha kujihifadhi kwa binti huyu. Kwa hakika suala la kupatikana kwa sodo mashuleni ni jambo la msingi nchini Tanzania, hoja siyo sodo za dharura tu bali sodo kwa kila binti aliyepevuka wote waliopevuka wapewe sodo bure mashuleni. Hoja hii kwa Tanzania inaonekna kama kutotiliwa maanani lakini Tanzania inatakiwa kuitilia maanani haraka maana Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanamke. Wenzetu Serikali ya Kenya imeanza kutoa sodo bure mashuleni kwa mabinti wote waliyopevuka  tangu enzi za Rais Mwai Kibaki hoja ya Kenya ni juu yasodokutoka nje zisitozwe kodi ili kuwapa nafuu wote wa Kenya.

Tanzania bado jambo hili litimeshikwa na kigugumizi, kwa hakika Mteguzi wa Kigugumizi Hiki ni Rais Samia.Suala la kufanyiwa hisani na walimu kutoa khanga na wanawake wengi wenye makazi jirani na shule kuwasaidia mabinti zetu linakuwa jambo la aibu maana sodo katika sanduku la huduma ya kwanza ni chache sawa na utani ukilinganisha na idadi kubwa ya mabinti waliyopevuka mashuleni.Sasa ni wakati sahihi jambo hili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Panapokuwepo na uhakika wa sodo salama inampa nafasi binti mwanafunzi kusoma kwa amani na huku elimu juu ya sodo kutolewa vizuri kukiwa na mazingira sahihi ya kutatua dharura kama hii mashuleni na siyo kutegemea hisani .


 

Swali ni je matukio kama haya yanatokea mangapi katika shule zetu?

 

Binti huyu alikimbizwa nyumbani kwa mwalimu, walimu wakijitolea khanga zao kuokoa jahazi hilo la binti wa kike aliyepevuka ambaye anakuja kumzaa raia wa Tanzania ambaye anaweza kuwa mwenye manufaa makubwa kwa taifa hili. Mwanakwetu alitarajia katika bajeti ya elimu ya mwaka wa 2021/2022 sodo bure mashuleni ilikuwa imepatiwa jawabu, ikapita 2021/2022, 2022/2023, 2023/2024 na tunakwenda na 2024/2025 huko kote limegonga mwamba.Mawaziri wanawake kibao na Spika juu yake,aaaa jamani,aaaa jamani washikeni mkono binti zetu.

 


Mwanakwetu anasema wazi,

Rais Samia Hili ni Deni Unalodaiwa mama, fumba macho fumbua kisha tamka sodo bure kwa shule za msingi na sekondari alafu twende kwenye Uchaguzi Mkuu na hili Baraka hata kwa Mola wako.Inashauriwa zitafutwe mashine za kutengeneza sodo ziwekwe hata jeshini na tena Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni mwanamke Stigomena Tax, zitengenezwe na kusambazwa sodo mashuleni nchi nzima bure.”

 

Kwa leo naweka kalamu yangu chini nakulikabidhi jambo hili kwa leo nasema kwa  mara ya mwisho kwa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika 2025.

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Mteguzi wa Kigugumizi Hiki Rais Samia.”

TANU walituambia,

 

“Inawezekana Kikubwa ni Kutimiza wajibu.”

 

makwadeladius@gmail.com
0717649257



 

0/Post a Comment/Comments