TATU MOJA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

 


Adeladius Makwega-Musoma MARA.

Nakualika tena katika Makala ya Katuni hakika haya yakiwa makala ya uchambuzi wa katuni kadhaa namna zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji mbalimbali. Kumbuka makala haya uchagua katuni nne katika kapu ya katuni tele, kisha kuzielezea namna zilivyochorwa alafu zinachambuliwa kwa jicho la mtayarishaji wetu.

Kuyaanza makala haya Mwanakwetu anaikamata katuni ya kwanza ambayo ndiyo inafungua ukurasa wa makala haya, katuni hii imechorwa na ndugu Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW Kiswahili ambapo inaonesha wahamiaji haramu wakikata baharini kutoa Bara la Afrika kwenda Ulaya. Jamaa hawa wamejazana botini wakikimbia Afrika kutokana na ukosefu wa ajira na huko Ughaibuni wakiwakataa. Kwa kando kuna jamaa wanaokwenda kuwaokoa hawa ndugu wakiwa na jamaa wa msalaba mwekundu, hawa waokozi wakisema jamani heshimuni haki za wahamiaji haramu na haki za binadamu

Katuni hii inaonesha hali ya changamoto za maisha za watu wanaokimbia mataifa yao kutokana na ugumu wa maisha huku ikisisitizwa haki ya kufanya kazi katika mataifa wanayokimbia na hata huko wanapokimbilia wasiwatendee vibaya hawa wahamiaji haramu na wao ni binadamu.


 

Sasa Mwanakwetu anaikamata katuni ya pili ambayo imechorwa na Alwatan Masoud Bini Kipanya ambapo kunaonekana jamaa kiganja chake kinaonesha kidole kimoja, ambapo kwa desturi kiganga kinachonesha vidole viwili huwa kinatumiwa na CHADEMA kama alama yao kwa muda mrefu. Kwa kuitazama katuni hii Mwanakwetu amekumbuka picha yake aliyopiga na dada yake Ahaliya wa Mbagala Sabasaba Novemba 5, 2012 ambapo alama ya vidole viwili na idole kimoja zilitumika kwa pamoja, Ahaliya alikuwa akiunga mkono CHADEMA huku Mwanakwetu akiunga mkono CCM. Katuni hii ya Masoud Kipanya inabua dhana kuwa je CHADEMA kwa sasa kinakwenda kupotea na alama zake na kuwa CCM B? Je Tanzania inarudi kuwa taifa la chama kimoja?

Hili ni swali ambalo majibu yake yatapatikana hivi punde. 


 

Mwanakwetu anaikamata katuni ya tatu ambapo kunaonekana jamaa alikuwa anakipaka rangi chumba chake, huku kitanda cha huyu jamaa kimetandikwa vizuri na kina mto ambao unaonekana kuwa na rangi za bendera za CHADEMA yaani nyekundu, bluu , nyeupe na nyeusi kwa hiyo huyu jamaa anawajibu wa kukipamba chumba hiki kiwe na rangi hizo lakini huyu jamaa  amebakia kiwiwili tu, hana kichwa, hivyo kukosa kichwa kunafanya jamaa kushindwa kuendelea na kazi ya kukipaka chumba chake rangi.Jamaa amekiti kitandani Je kichwa chake kimekwenda wapi?

Kwa jicho la mtayarishaji wetu anapoutazama mchoro huu unadokeza kuwa hali ya CHADEMA hivi sasa suala la kupatikana kwa mwenyekiti wake kitaifa limekuwa kizungumkuti, hivyo  mchoraji wa katuni hii anaamini kuwa kama huyu jamaa akipata kichwa chake ndipo kazi ya kukipamba chumba hicho itafanyika vizuri, vinginevyo hali itakuwa mbaya na pengine huo ndiyo mwisho wa CHADEMA maana binadamu hawezi kuishi kama kichwa na kiwiliwili vimetenganishwa. Swali ni Je kati ya Mbowe na Lissu nani ni kichwa halisi kwa mustakabali wa CHADEMA? Kikubwa tusiandikie mate wakati wino upo, tungoje muda ukifika wenye CHADEMA yao watakapo fanya maamuzi.


 

Mwanakwetu anaikamata katuni ya mwisho , hii imechorwa na King Kinya na ya mwaka 2020 ambapo anaonekana marehemu Bernad Membe akiwa amekali kiti chake maridadi, kiti chenyewe kina rangi ya ACT Wazalendo. Katuni hii imekumbusha Mwanakwetu mambo matatu; Kwanza picha moja ambayo Bernad Membe alipiga na mwanahabari maarufu Tanzania Yotham Ndembeka siku chache kabla ya kufariki ambapo Mwanakwetu aliandika makala mbili ya kwanza Aprili 29, 2023 iliyopewa jina Samehe Haraka Wala Usichelewe https://www.mwanakwetu.co.tz/2023/04/samehe-haraka-wala-usichelewe.html na makala ya pili iliandikwa Mei 13, 2023 baada ya kufariki ikisema Tunakwenda Kumzika Membe https://www.mwanakwetu.co.tz/2023/05/tunakwenda-kumzika-membe.html


 

Katika haya yote matatu yaani makala mbili na picha ya Membe ya Yule mwanahabari, Mwanakwetu amekumbuka namna Bernad Membe alivyokuwa akiomba kura katika mkutano wake wa Uzinduizi wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 pale Lindi ambapo aliomba kura vizuri sana.

“Sisi katika chama cha ACT tuna wateja Wazuri ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM). Kwa sababu na wenyewe wamechoka na kuna makundi mawili ndani ya CCM; Wale waliyochoka kabisa na kuachana nao na wale wanaotuunga mkono wakisema tuacheni tubaki na kadi zetu.”

Kwa hakika hoja za Membe katika kampeni ya ufunguzi wa ACT mwaka 2020 alizijenga vizuri sana na zinatoa wazo moja jipya kuwa mtu anapokuwepo CCM haina maana kuwa anakubaliana na kila kinachofanywa na CCM na Serikali yake na ndiyo maana Membe alisema mengi ambayo mengine alishiriki katika vikao vya maamuzi vya CCM ngazi za juu na Bungeni na kwenye Baraza la Mawaziri.

“Ndugu zangu wa Lindi mkitaka tuingie Ikulu tunatakiwa kufanya mambo mawili tu;, la kwanza tuondoe woga na pili kupiga kura.”

Maneno haya ya Bernad Membe ambaye mwili wake umelala kaburi mwaka unusu sasa yanatoa fikra ya umuhimu wa vyama vyote vya siasa hasa vya upinzani kufanya shuguli zake bila usumbufu wowote kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya kila mara inavyonadi katika Sura ya Kwanza, Sehemu ya Kwanza ibara ya tatu moja

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya Kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kwa hakika Bernad Membe amefariki dunia.

“Tuingie tusiingie –Ingia. Nimtoe Nisimtoe –Mtoe.La tatu linaloniuma , Kiongozi anasema jamani nakuja kuomba kura, hodi nataka mniruhusu niendele miradi niliyoianzisha, haondoki mpaka mpaka tumtoe. Je akianzisha miradi 2024 aje akianzisha mradi mwaka 2024 alafu anaomba miaka mitano tena mtakubali? Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaturuhusu kutumia katika sanduku la kura kumtoa mtu madarakani.”

Swali la kujiuliza wale waliyokuwa wakimuitikia Bernad Membe wote wamelala makaburini ?Jibu lake wako hai na kiitikio chao ni ndiyo ya ile ibara ya 3(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Jamani asanteni sana, endeleeni kufuatilia vyombo vya habari, muone namna tunavyoitembelea Tanzania tukifanya kampeni,kazi inavyofanyika, mkapige kura kisha tusibiri matokeo Oktoba 25,”

Mwanakwetu upo?


 

Basi hadi hapo ndiyo na mimi natia nanga katika makala ya katuni siku ya leo, nilikuwa na katuni nne; Ile ya wahamiaji haramu na changamto zao, ya pili ni ya kupotea kidole kimoja cha CHADEMA na ya tatu ni ile ya jamaa wa CHADEMA mpaka rangi chumba ambaye amekatwa kichwa na katuni ya nne na ya mwisho ni ya huyu  marehemu Bernad Membe, hii ni ya mwaka 2020.

Kwa katuni zote nne ndiyo Mwanakwetu anatia nanga ya makala ya katuni siku ya leo. 


 

 

Kumbuka

“Ibara Tatu Moja ya Katiba ya Jaahuri ya Muungano wa Tanzania”

Nakutakia Krisimasi Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 


 


0/Post a Comment/Comments