Adeladius Makwega-Musoma MARA.
Majira ya asubuhi ya Januari 22, 2025 Kompyuta ya Mwanakwetu imeharibika, hivyo hawezi kuendelea na kazi yake aliyokuwa anaifanya, hilo likamnyanyua hadi kuwatafuta mafundi mahiri wa kompyuta ili kukipa tiba kifaa chake hicho.
Safari haikuwa ndefu, akafika kwa wataalamu hao ambapo alipoitazama ofisi hii ilikuwa kama haina watu lakini alipepesa zaidi na kuita aliitikiwa kuwa tupo, Mwanakwetu aliingia na kuwaeleza jamaa hawa shida yake. Mandhari ya ofisi hii ilikuwa ya utulivu kiasai kiyoyozi asilimia zote na sauti za mashine zikilisindikiza baridi lenye mzizimo mkali.
Kwa mbali sauti kama hotuba inayotoka katika simu ya mkononi ikikata mawimbi, huku ndugu hawa wawili walikuwa wameiinamia simu hiyo iliyokuwa mezani kwao. Mwanakwetu akawa akasikiliza kwa umakini mkubwa, Mwanakwetu akajiuliza hawa jamaa wanasikilizi nini?
“…Mwenyekiti mpya atoe neno kwa ufupi lakini neno la urefu atasema baadaye kama analo lakini katika hatua hii naomba yeye amkaribishe Mwenyekiti anayemaliza muda wake. People s Power ! Peoples Powers ! Stronger Together!, Stronger Together...! Wanasema wewe ni Mwenyekiti Mstaafu, Wewe ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya Chama, Mwenyekiti haukimbii namna hiyo wewe bado ni kiongozi, hiki kitabu unachokibeba kinakubeba bado, wajumbe wa Mkutano Mkuu naomba nimshukuru mwenyekiti wetu …”
Hapo Mwanakwetu sasa anasikia sauti kadhaa ya kiyoyozi ndani ya chumba hiki, vifaa vya kompyuta, hotuba katika simu. Hotuba hii Mwanakwetu alifuatilia alibaini sauti ya John Mnyika Katibu Mkuu CHADEMA na baadaye ya sauti ya Tundu Lissu Mwenyekiti mpya wa CHADEMA, hapo hapo Mwanakwetu akabaini kuwa jamaa hawa wawili wanasikiliza Mkutano Mkuu wa CHADEMA.Mafundi hawa huku mmoja akimrekebishia Mwanakwetu kompyuta yake.
Kuna jambo likamstajabisha mno Mwanakwetu,
“Jamaa hawa walikuwa na TV kubwa inafanya kazi lakini hakuwasha TV yao wauone mkutano wa CHADEMA bali TV ilikuwa inaonesha mambo mengine kabisa, kwanini hawakuwasha runinga yao ?Bosi anawachagulia hadi chaneli.”
Mwanakwetu akawaambia hawa jamaa ahaa kumbe nyinyi siyo wenzetu eeeh, hawa jamaa wakacheka wakawa wanakataa hapana tunasikiliza tu mkutano wa CHADEMA bali sisi siyo CHADEMA sisi ni wenzako kaka.
Maneno haya ya Mwanakwetu ya kumbe nyinyi siyo wenzetu yakawanyima raha hawa jamaa wakapunguza zaidi sauti ya hotuba kutoka katika simu janja. Jamaa mmoja katika chumba hiki akasema daa Tundu Lissu kapitia magumu mno, jamaa wa pili akasema hee wamepitia magumu mno , chama hiki kama una roho nyepesi hauwezi kuendelea na siasa maana wapo waliokufa na wapo wapo waliopata vilema vya kudumu.
“Yaani mtu unamuwa mwenzako hivi hivi, ati una roho gani? Huo sio ubinadamu, sasa kama wewe uliyefanya hivyo upo hai unawezaje kumtazama uliyemfanyia ubaya akiwa hai ?”
Jamaa kando akasema, hawa jamaa wana roho mbaya hiyo na hata kumfanyia mnyama inahitaji ukatili mkubwa, ngojeni niwasimulie kisa hiki.
“Nyumbani kwetu tulikuwa na mazizi makubwa sana ya ngombe zaidi 3500 mbuzi kondoo mbwa tete na kuku wengi maana kinyesi cha ngo’mbe kinasaidia kuzalisha wadudu ambao kuku wanakula sana , kwa hiyo makundi ya kuku yalikuwa mengi na zisizohesabika. Siku moja ninataka kuingia ndani wanapolala kuku ambapo na binadamu walikuwa wakiishi humo humo nakutana na mbwa wangu anatoka ameyabeba mayai mdomoni ya kuku mmoja ambaye alikuwa anataga sana huku akitotoa anatotoa vifaranga karibu vyote na kuvilea vizuri hadi vinakuwa vikubwa salama.”
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu hapo anasubiria kompyuta yake inawekwa sawa na simulizi inaendelea.
“Nikasema shabashi! Kumbe huyu mshenzi ndiye anayekula mayai ya kuku wangu! Nikamfukuza na kumkamata hapo hapo nikaanza kumuadhibu kweli kweli, Mbwa anapiga kelele, hali ya adhabu ya mbwa ilivyo kuwa tete akachomoka na kukimbia mwendo hivi nyuma ya nyumba yetu. Kwa kuwa mimi ni baba wa mji nikaagiza mfukuzeni mbwa huyu mshenzi anayekula mayai ya kuku wetu.
Vijana wangu wakaitikia kauli ya baba kwa nguvu moja wakawajibika kumkimbiza huku na kule huku na kule wakampata na kuendelea kumuadhibu na kumsogeza nilipo mimi, baba wa mji. Kumbe mbwa /mnyama anavyopewa mateso huwa kuna hatua za vilio huku sauti ya mbwa ikibadilika kulingana na hatua hizo. Tukampiga yule mbwa hadi akafa, nikaagiza vijana mbebebeni mkamtupe mbali. Vijana wakafanya hivyo na kufanyia usafi eneo tulilomuadhibu mbwa jirani na nyumba yangu huyu, lakini cha kushangaza hata baada ya usafi nzi kadhaa walizunguka eneo hilo la tukio . Tukamaliza zoezi lile na kuendelea na kazi zetu.
Usiku sikulala, akilini mwangu inanijia sauti ya kilio cha mbwa yule hatua kwa hatua huku ikiwa kama filamu tangu namuona mbwa na mayai mdomo, namkamata nampiga mbwa, anakikimbia hadi mbwa anafukuzwa na vijana hadi anapigwa na kufa na mwisho naona mandhari ya inzi wengi baada ya zoezi hili. Usiku huo sikulala hadi kunakucha mwendo ulikuwa Mawazo Bini Mang’amung’amu.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo anatengeneza kompyuta yake. Hapo sasa Kompyuta ya Mwanakwetu imepona akakabidhiwa akakaa huku akizituma stori zake mtandaoni, jamaa kando akawa anaendelea kusimulia huki huyu Tundu Lissu anaendelea hotuba yake ikiwa kwa sauti ya chini. Jamaa anayesimulia kisa cha mbwa akasema,
“Sasa nikawa najiuliza hivi sisi tuna ng’ombe zaidi ya 3500, mbuzi na kondoo wasiohesabika nimemuuwa mbwa wangu kisa mayai ya kuku, hata kama mbwa huyu angemla kuku mwenyewe kweli hili ni haki? Nimemuuwa mbwa wangu, usiku sikulala, hivi hawa wanaopanga na kuwauwa wanadamu wenzao wanakuwa roho ya namna gani?
Unajua mimi mshituko huo nilioupata wakati ambao sikuwa na hata na dini maana Ukristo ulikuja baadaye. Hilo liliniumiza mno moyoni. je vipi huko kwa Mwenyeezi Mungu jamani Atakuacha Salama Kweli.”
Mwanakwetu alipomaliza kutuma Stori zake aliwaaga hawa jamaa huku wakiendelea kuusikiliza mkutano wao na yeye kwenda zake.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Msomaji wangu nakuomba leo hii tafakari kisa hiki kwa kukisoma mara tatu juu ya huyu Mpagani Aliyeuwa Mbwa Wake kisha simulia watu watatu tu.
Mwanakwetu upo?
Makala haya niyaitaje?
Leo
Nisiseme Neno, Mpagani Aliyeuwa Mbwa Wake,Mbwa wa Mpagani, Bosi Anayechagua Hadi Chaneli Au Mawazo Bini Mang’amung’amu
Mwanakwetu anachagua Bosi Anayechagua hadi Chaneli
Nakutakia Siku Njema.
0717649257.
Post a Comment