AKIUNYEA MKONO MSIUKATE

 



Adeladius Makwega-Musoma MARA

FEBRUARI 2022 Kamishina wa Elimu Tanzania alitoa Mwongozo wa kuwarejesha Shuleni Wanafunzi waliokatiza Masomo kwa Sababu Mbalimbali, shabaha ikiwa kukamilisha elimu yao walipokomea kwa ngazi husika.

Kwa hakika nyaraka hii ya elimu ina kurasa saba zenye maandishi nia kwa kila mdau wa elimu, kwa watoto na wanafunzi wetu waliyokatiza masomo waweze kufikia ndoto zao ambazo pengine zilisimamishwa kwa changamoto kadhaa ikiwa utoto, ujana, jinsia , maumbile au makundi rika.

Kwa hakika jamii ya Watanzania naomba ifahamu kuwa zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kusababisha mtoto/ mwanafunzi kukatishwa masomo, zikiwamo hata hoja ya nidhamu ya mwanafunzi, hapa kikubwa zinabebwa na basi la jinsia yake, utoto wake, ujana wake , rika lake , mihemuko na makundi rika ambacho hiki ni kipindi kigumu sana kwa malezi ambacho kina upepeo mbaya na kinaweza kikawabeba na kuwakumba wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari huku baadaye wakiwa watu wazima wakajilaumu kwa kilichotokea..

Nakuomba msomaji wangu ufahamu mambo kadhaa dhidi ya ninayeandika makala haya kwanza ni mwalimu, pili ni mwanahabari , tatu nimefanya kazi ngazi ya maamuzi katika Serikali za Mitaa lakini pia nimepitia changamoto za elimu ya Tanzania. Hapa ninaandika juu ya jambo ninalolifahamu kwa kina.

Kwa uzoefu wangu utaratibu wa awali ulikuwa na madhaifu makubwa ambapo majibu yake ndiyo ujio wa huu mwongozo unaojadiliwa leo hii. Swali la kujiuluza je utaratibu wa awali ulifunga milango katika hilo 100 kwa 100 ?

Jibu lake hapana, wengi wanadhani jibu lake ni ndiyo. Jibu lake ni hapana kwa kuwa utarataibu wa awali katika kila mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikuwa na nafasi ya majadiliano baina ya wazazi na viongozi wa elimu.

Naomba nitolee mfano wa Mkoa wa Dar es Salaam watu wa Mzizima walikuwa na Bodi ya Rufaa ya Mkoa  ambayo iliundwa na wajumbe kadhaa akiwamo Mkuu wa Mkoa ambaye alikuwa mwenyekiti, Afisa Elimu Mkoa(Jiji) wa Dar es Salaam akiwa Katibu na wajumbe wengine watatu ambapo kabla ya vyama vingi walikuwa wanatoka UWT, WAZAZI na UVCCM).”

Kwa utafiti wa Mwanakwetu anatambua hili halifahamiki na wengi na ndiyo maana liliwanufaisha watoto/wanafunzi wachache mno hasa wale wazazi/walezi na koo zilizotambua hilo maana ulikuwa utaratibu kama kimahakama. Baada ya Mzazi /Mlezi kupokea barua ya kufukuzwa mwanawe iwe kwa hoja ya nidhamu (Mimba, utoro, fujo nk) barua hiyo kutoka Bodi ya Shule ilimuelekeza Mzazi/ Mlezi kuwa anaweza kukata rufaa kwa Bodi Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam, ndani siku 45 baada ya uamuzi wa Bodi ya Shule kufanyika. Kumbuka Bodi ya Shule inaundwa na Wazazi/ Walezi na katibu wao ambaye ni Mkuu wa Shule.

Bodi ya Rufaa Mkoa iIipofanya maamuzi baada ya kupokea rufaa ya utetezi wa maandishi kwa kosa alilotuhumiwa mwanafunzi husika kwa kujadili hoja moja baada nyingine kasha kukata shauri husika, aliyeshindwa na hata alishinda yaani Mtoto/Mwanafunzi au Bodi ya Shule ilikuwa na haki ya kukata Rufaa kwa Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya siku 45 baada ya kupokea barua ya maamuzi. 


 

Suala hilo muhusika kama angeshindwa kwa Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa na haki ya kwenda mahakamani lakini kwa utafiti wa Mwanakwetu mashauri mengi yaliishia ngazi ya Bodi ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo iliongozwa na watu makini na waliokuwa  na uchungu na Dar es Salaam yao.

Nakuomba msomaji wangu kwa rejea nakupatia mashauri manne ya mfano ambayo yaliamuliwa na Bodi ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam Aprili 1994 kwa maamuzi ya Bodi za Shule kwa mwaka 1993 mashauri matatu wanafunzi walirejeshwa shuleni na shauri moja mwanafunzi hakurejeshwa shuleni.

“Aron Sifuni (KATISI), Mohammed Said (Mzukizi) na Adeladius Makwega Vs Bodi ya Shule ya Sekondari Tambaza. Maamuzi ya Bodi ya Rufaa ya Elimu ya Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Ditopile Ukiwaona Ramadhari Mzuzuri (RC Dar es Salaam), wanafunzi hao watatu walirejeshwa masomoni kama ifuatavyo Aron Sifuni na Mohammed Said walipangiwa Kibaha Sekondari PWANI huku Adeladius Makwega alipangiwa Same Sekondari KILIMANJARO”

Tangu kukatwa kwa Rufaa hadi maamuzi yalitumia miezi karibu saba ambapo Shauri ambalo mwandishi wetu anakumbuka mwanafunzi alishindwa hili;

“Lukas Mganga Vs Bodi ya Shule ya sekondari ya Tambaza, maamuzi ya Bodi ya Rufaa Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Ditopile Ukiwaona Ramadhani Mzuzuri (RC Dar es Salaam) yalikubaliana na uamuzi wa kumfukuza Lukas Mganga shule moja kwa moja huku akipewa haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Elimu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania wakati huo akiwa Profesa Philemon Sarungi.

Lukas Mganga akiwa mwanafunzi wa kidato cha nne Tambaza Sekondari mapema mwaka 1993, alikamatwa na polisi mkoani Dar es Salaam na kukutwa na majani yaliyodhaniwa kuwa na Bangi, majani hayo yalipelekwa na Mkemia wa Serikali na baadaye Bodi ya Shule na Polisi Dar es Salaam kujulishwa kuwa Lukas Mganga alikuwa na madawa ya kulevya aina ya Bangi siku aliyokamatwa.”

Mwanakwetu anakumbuka utaratibu huu wa kukata rufaa wapo hata mabinti waliokuwa na ujauzito ambapo pengine ujauzito ulitoka walirejeshwa masomoni, nakumbuka mwaka 1994 binti mmoja wa Shule ya Sekondari Kisutu alikuwepo katika kikao hicho juu.

“Tulikaa naye katika benchi moja, alivaa blauzi nyeupe na chini alivaa sketi ya Kisutu na maamuzi kwa shauri lake kikaoni alisomewa kuwa arejeshwa shuleni na kukariri kidato cha tatu kwa kupangiwa shule nyingine, kwa bahati mbaya jina lake silikumbuki lakini kikao hiki kilifanyika  katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam juu huku kila mwanafunzi aliambatana na mzazi wake.”

Mwanakwetu hana hakika kwa mikoa mingine hali ilikuwaje lakini ninachoweza kukisema nilipokuwa Ndanda Sekondari mwaka 1996-1998 nilishuhudia wanafunzi wawili wa kiume walifukuzwa shule na walipopewa barua zao, waliondoka tu na hata barua hizo hazikuwapa nafasi ya kukata Rufaa kwa Bodi yoyote ile, hawa jamaa wapo hai hadi leo hii na nadhani makala haya watayasoma, walimalizia ndoto zao za elimu shule binafsi, hii ni kwa mkoa wa Mtwara..


 

Mwanakwetu anaandika makala haya kwa jamii ya Kitanzania, inatakiwa kutumia fursa hii vizuri ya mwongozo huu wa kurejeshwa masomoni katika kipindi kati ya siku moja hadi miezi 24 mwanafuniz/ mtoto alipokatisha masomo yake kwa sababu mbalimbali.

Mwanakwetu anatumia wakati huu wa kufunguliwa kwa hasa kwa shule hasa za umma  wazazi / walezi wale watoto /wanafunzi wetu waliyopata changamto mbalimbali mwaka jana na juzi, jamii ya Watanzania msidhani ruhusa hii ni kwa waliyopata ujauzito tu,mwongozo unasema sababu mbalimbali, nendeni mashuleni, tumieni haki hii ili watoto /wanafunzi wetu wakamilishe ndoto zao.


 

Wazazi/walezi wanaweza kutembelea Ofisi za Elimu Kata, Ofisi za Elimu Halmashuari za Wilaya , Ofisi za Elimu Mikoa na hata shule husika za umma mtapewa mwongozo wa cha la kufanya .

Msomaji wangu naomba nikurejeshi nyuma kidogo Aprili 1994 ndipo Bodi ya Rufaa Mkoa wa Dar es Salaam ilikaa chini ya Mwenyekiti Ditopile Mzuzuri, Katibu alikuwa Mwalimu Abdalla Mbegu–Afisa Elimu Jiji Dar es Salaam na kukiwa na wajumbe watatu ; mama mmoja, kijana mmoja baba mmoja. Huyu baba mmoja, mjumbe alikuwa ni Ibrahimu Raha mwenyekiti Wazazi Dar es Salaam, ambaye alikuwa muigizaji wa michezo Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) a.k.a Mzee Jongo.

Wakati maamuzi yanasomwa Ibrahimu Raha akasema,

Wazazi / walezi,

“Mtoto akiunyea Mkono Msiukate.”

Mwanakwetu anasema nini?

Kikubwa na ukweli wa Mungu kwa utekelezaji wa huu Mwongozi wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatiza Masomo Katika Elimu ya Msingi na Sekondari Kwa sababu Mbalimbali una changamoto kwa mabinti waliopata ujauzito  hoja NI IPI?;

“Kiumbe yoyote hai aliyejifungua/kuzaa mtoto yu hai akili zake zote ni kwa kiumbe chake alichokileta dunia, je  mwanangu amekula?, Sijui mwanangu analia? Sijui saizi binti wa kazi anampiga? 

 Kiumbe hiki unapokirejesha kwenye what is Biology? What is  History ? Tunakosea sana, kiumbe hiki kilitakiwa kitengenezewe mazingira ya kujifunza kazi za mikono ili zikamsaidia kupambana na maisha na malezi ya kiumbe chake, kwa hakikik mabinti hawa walio wengi kusoma ni changamoto lakini wale wenye shida zingine kusoma elimu hii haikwepeki.”

Watanzania tutambue hii ni nchi ni yetu sote na hawa watoto/wanafunzi ni wakwetu hata kama haujawazaa wewe, jamii inatabia ya kutegemeana, mwanao ataolewa au kuoa katika hiyo jamii, binadamu  tunategemeana, dunia imejengwa katika kila mmoja kumuhitaji mwezake.Watu wengi wenye elimu na nafasi wanao kuwa kama jambo hili halimuhusu.Hoa hao vijana wa bodaboda , hawa hawa mabinti wanaofanya kaiz za ndani watazaa na familia yako, lazima tuwape elimu tutake tusitake.


 

Mwanakwetu Upo?

Nasema

“Mtoto Akiunyea Mkono Msiukate.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

NB PICHA ZOTE NI ZA MAKTABA ISIPOKUWA NAKALA YA  MWONGOZO











0/Post a Comment/Comments