MUDA WA KUTAMBIKA WENYEWE TUNAUJUA


 



Adeladius Makwega-Musoma MARA

Nikiwa Wilayani Lushoto kati ya mwaka 2016-2018 Rais wa Awamu ya tatu Benjamin Mkapa alikuwa na makazi yake ambayo yalikuwa nje kidogo na mji huu kama unakwenda Mlola. Eneo la makazi ya Mzee Mkapa palikuwa na bonde zuri kwa kilimo cha bustani.Kama yalivyo maeneo mengi ya wilaya ya Lushoto wanalima sana mabondeni mboga mboga kama kabichi, viazi mviringo, karoti, nyanya, vitunguu, pilipili hoho, nyanya chungu, bamia, bilinganya, maharage mabichi na hata brukolini.

 

Nakumbuka hata hii brukolini nilikuwa siifahamu mie mtoto wa Mbagala, kufika Lushoto nilitambua maana ilikuwa inasafirisha hadi Ujerumani na inaipatia Halmashauri ya Lushoto pesa nzuri. Hata msaada ya ujenzi wa sehemu yenye majokofu ya kuhifadhia mbogamboga hizo Lushoto walijengewa kwa mkopo kwa sababu ya Kilimo Brukolini.

Kilimo cha bustani cha Lushoto kinashangaza maana kinafanyika mno kipindi cha kiangazi tu. Kipindi cha masika inakuwa ngumu kuyadhibiti maji na mafuriko yanayosomba mbegu, mbolea na mazao milimani kuyatupa mithili ya zimwi na takataka mabondeni.


Mzee Mkapa kwake palikuwa panalimwa sana na alikuwa analitumia vizuri bonde hilo mithili na yeye alikuwa mzaliwa wa Lushoto. Kwa hiyo bonde hilo walilima viazi na mboga mboga zingine tele. Huku wakivuna, zinapakiwa katika mafuso na kusafirishwa kwenda Dar es Salaam au Arusha.

 

Wakifika pale geti la Halmashauri ya Lushoto-Nyasa, viroba vinahesabiwa kimoja baada ya kingine wanalipa na kuondoka zao kwa amani kabisa.Wakiwa  na mavuno mengi Vijana wa Benjamin Mkapa walipomaliza kuvuna walimuita mtendaji wa kijiji  na kukatiwa ushuru shambani kisha mazao kupakiwa naye Mwanakwetu kuyakagua malori hayo moja baada ya linguine kituo cha ushuru Nyasa kilichopo mpakani mwa Lushoto na Bumbuli.

 

Unaweza kutambua kuwa ni viazi vilivyolimwa mbele ya nyumba ya Mzee Mkapa kama mtendaji wa kata husika alipita katika shamba hilo na akavihesabu wakalipa ushuru na kuwapa lisiti. Mafuso hayo yakipita Nyasa wanakaguliwa tena ndiyo utatambua hii lisiti namba kadhaa wa kadhaa ni ya mashine ya kata ambapo makazi ya Mzee Mkapa yao.

 

“Shamba gani hili mmepata viazi vingi hivi?”

 

Shamba mbele na makazi ya Mzee Mkapa wanajibu madereva wa fuso. Hii inasaidia kujua hata uzalishaji wa kila kata wa mazao. Mzee Mkapa alikuwa anafika kwenye makazi yake, muda mwingine yupo mwenyewe, muda mwingine anakuja na mama Anna Mkapa

 

Mara zote kiongozi mkubwa kama yeye anapofika kwenye wilaya kwa utaratibu anapokelewa kwa heshima zote na viongozi wa wilaya hasa hasa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na waalikwa wa kamati hiyo ambao ni Afisa TAKUKURU na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika pia hata CCM wenye serikali yao anakuwepo Mwenyekiti wa Wilaya na Katibu wake.

 


Anapokuja kiongozi aliyeshika nyadhifa kubwa, ukiwa imongoni mwa niliowataja hapo juu lazima ujitahidi sana unakuwepo. Hapo anaweza kuuliza au kupatiwa ripoti ya hali ya wilaya ilivyo. Akiwa nyumbani kwake anaweza kumtembelea mzee mwenzake au wazee wenzake wanaweza kwenda kumtembelea kiongozi huyu, kama ana makazi hapo anao majirani, marafiki na hata jumuiya za dini. Kama umebahatika kukaa jirani na wazee wengi kama huyu huwa ni wakweli na hawapendi kuficha jambo. Huwa hawapendi mtu aharibikiwe kupitia mkono au kauli yake. Kwa hakika Mwanakwetu jambo hili nilijifunza Wilayani Lushoto na hasa kwa Mzee Ben Mkapa.

 

Kwa hakika nakumbuka tukio hili,

 

“Kuna siku alikuja Mzee Mkapa, akapokelewa vizuri, mimi na wezangu tukashiriki kwa karibu sana, tukapanga foleni akianza mkuu wa wilaya na katibu tawala na siye wengine wa mwisho mwisho.
 

Mzee Mkapa alipofika tukamsalimia kwa kumpa mikono na shikamoo yake na kisha tukaingia hadi sebuleni kwake. Kwa umri ambaye kidogo alikuwa analingana na Mzee Mkapa nadhani alikuwa Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Lushoto wakati huo Balozi Mstaafu Abdi Mshangama (mzee mmoja mrefu mweupe) sidhani yeye kama shikamoo ilimtoka walikuwa nadhani wanalingana.
 

Tukiwa tunaingia sebuleni kwake. Mzee Mkapa akasema.‘Mkurugenzi Kazimbaya upo? Nikajibu nipo shikamoo.’ Mzee Mkapa akajibu marahaba huku akicheka, wajumbe halali wa kamati ya ulinzi wanastajabu inakuwaje Mzee Mkapa anamtaja Mwanakwetu ambaye mara nyingi nakuwa nyuma nyuma? Mzee Mkapa akanishika mkono kisha akauliza ‘Kwanini umeukata mti wa matambiko?’ Akasema kwa kunong’ona.Nikajibu kweli tulitaka kuukata maana ulikuwa unaharibu nyumba ya serikali. Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga (wakati huo)Injinia Zena Said aliwasiliana na sisi tukawa tumeupunguza matawi tu, lakini tumesitisha zoezi hilo mheshimiwa.Mzee Mkapa akauliza,

 

‘Unataka shemeji zako wakatambike wapi?’Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi wanasikiliza na Watu wengine tuliombatana nao wakawa wanacheka maana maneno mengine walikuwa wanayasikia. Hapo hapo tunaingia sebuleni nyumbani kwa Mzee Mkapa-Lushoto, viongozi wote ewakubwa wanajiandaa kumsomea taarifa ya wilaya. Kisha Mzee Mkapa akasema,’Jamani mimi nimechoka sana, sasa naombeni mniache nikapumzike.’ Basi kila mmoja wetu tukatoka ndani na kuwasha magari yetu na kurudi nyumbani maana ilikuwa siku ya mapumziko.”

 

Jambo hilo lilinipa tafakari mno huku nikitafuta majibu, huku nitambua kuwa Mzee Mkapa wilayani Lushoto alikuwa na marafiki zake wakubwa watatu, wa kwanza Brigedia Mstaafu Hassan Ngwilizi,wa pili ni Diwani Lukozi wa wakati huo Marehemu Karim Mahanyu na wa tatu ni Baba Askofu Mstaafu Stephern Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumbuka wakati huo Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania alikuwa John Pombe Magufuli na Jamii ya Watanzania walikuwa wakiamini kuwa aliyekuwa anamuweza Magufuli vizuri ni Ben Mkapa peke yake.


 

 

Nikasema moyoni kama zengwe la Mti wa Matambiko lipo kwa Mkapa maana yake Magufuli analo, binafsi sikuwa na amani siku hiyo nikawa najua kuwa hapo siku za kutumbulia zinahesabika tu na wale jamaa na barua zao wako stand by lakini je ukweli unajulikana kwa Rais John Pombe Magufuli? Nikajiuliza jambo hili kwa kina na namna kuweza kulipata vizuri, nikasema hawa rafiki zake watatu mmoja kati hao lazima atakuwa na majibu. Basi nikamfuata Karim Mahanyu alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Uongozi na Fedha ya Halmashauri hii pia alikuwa kiumri hajazinidi sana, nikajua tu tutaelewana vizuri.


 

 

Siku hii Karim Mahanyu kaja Halmashauri katika Kikao cha Kamati ya Fedha kikafanyika vizuri kisha nikamuita ofisi, kumuuliza kulikoni mbona Ben Mkapa kaniuliza juu ya Habari ya Mti wa Matambiko kuwa nimeukata na mimi sikufanya hivyo bali Mtendaji wa Kata ya Lushoto.mheshimiwa Mahanyu akaijibu,

 

“Kweli kuna wazee wa kimila walikwenda kwa Mzee Mkapa wanalalamikia kuwa mti wao wa kutambika Pale SECUP umekatwa na Mkurugenzi Mtendaji na huo mti haupo Tanga nzima ulikuwa mti mmoja tu.”

 

Nikamuuliza Mzee Mkapa akasemaje? Karim Mahanyu akajibu

 

“Mzee akauliza vyombo vya ulinzi na usalama, walipompa jibu ndiyo salama yako akaliachia jambo hili hapo hapo.”

 

Karim Mahanyu akaniuliza kwani kumetokea nini? Nikamueleza Karim Mahayu vile alivyoniambia Mzee Mkapa siku tuliyompokea na simu ya Injini Zena Said Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga wakati huo. Huyu Karim Mahanyu sasa marehemu alikuwa mtu mmoja siyo msemaji, mkimya mno, tajiri hakuwa fukara na alikuwa ndiyo mara nyingi mazao yakivumwa katika makazi ya Mzee Mkapa anasimamia zoezi hilo mwanzo mwisho maana yake alikuwa mtu muaminifu alisimamia kutayarisha shamba, kupanda kuyatunza mazao hadi kuvuna. Hapo hapo tupo na Karim Mahanyu ofisini nikasema sasa mheshimiwa, mbona pale pana ua wa wavu, geti la chuma na mlinzi mwenye bunduki mchana na usiku?Mnatambika muda gani kwenye jengo la serikali? Maana kwa Maelezo ya Mtendaji wa Kata ya Lushoto ndugu Karanga waliomba kibali cha kuukata mti huo shabaha walikuwa wanaokoa jengo na mabati yanaoza kutokana na matawi na majani ya mti ule.

Mheshimiwa Karim Mahanyu akasema.

 

“Hayo mambo, wewe achana nayo, ili mradi mti upo. Muda wetu wa kutambika Wasambaa tunaujua Wenyewe.”

Majibu haya yalimfanya Mwanakwetu kuwa mpole na mti huo upo hadi leo hii na pengine Shemeji za Mwanakwetu Wasambaa wanaendelea kutambika hadi kesho.


 

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Makala haya yametayarishwa kwa  heshima ya marehemu Ben Mkapa ambaye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana siku ya leo nimemkumbuka mzee wetu huyu.

 

“Raha ya Milele Uumpe Ee Bwana na Mwanga wa Milele Mwangazie Apumzike kwa Amani Amina.”

Kumbuka,

 

“Muda wa Kutambika Tunaujua Wenyewe.”

 

Nakutakia Siku Njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 






 

0/Post a Comment/Comments