Adeladius Makwega Musoma MARA
Napokea simu na aliyenipigia akijitambulisha kisha kusema kuwa unahitajika kutoa Ushahidi katika Shauri Moja la Jamhuri, maana wewe ni Shahidi wa Jamhuri. Mwanakwetu akauliza Shahidi wa Jamhuri? Jamaa akajibu ndiyo. Mara baada ya simu hii Mwanakwetu, Shahidi wa Jamhuri alikumbuka kuwa siku kadhaa nyuma alishafanyiwa mahojiano na taasisi moja iliyokuwa inachunguza shauri fulani. Katika simu hii pia alielezwa tarehe ya kufika mahakamani kutoa ushahidi wake. Mpiga simu alieleza kuwa Mwanakwetu afike siku moja kabla ya shauri ili kumuongoza kutoa ushahidi kabla ya kesi, Mwanakwetu aliuliza nani atalipia gharaza za kumtoa hapo alipo hadi huku Mahakamani? Majibu yalikuwa ni gharama ya Jamhuri. Simu ilipokata Mwanakwetu akawa anajindaa na baadaye alipigiwa simu tena,
“Gharama ni kubwa karibu milioni mbili na ushehe, hivyo imeamuliwa utoe ushahidi kwa simu ya video.”
Mwanakwetu akasema acheni ubahili, sasa imeshakuwa Jamhuri ya Mkono wa Birika? Ebu toeni pesa, nije nitoe Ushahidi wa Jamhuri. Daa udenda uliokuwa unamtoka Mwanakwetu sasa ukakata maana anakosa kitita cha Jamhuri maana kama ingekuwa Januari Mwanakwetu angekuwa amejaa machungu ya kulipa karo za watoto wake maana Mwanakwetu ni Baba Makusanya aka Hondo hondo Mlezi wa Wana.
“Utaelekezwa Mahakama Kuu ilipo kisha tutakuongoza hadi hapo kuutoa ushahidi huo.”
Lo salale bin lahaula la kwata, Mwanakwetu amekosa kitita sasa anakwenda kutoa ushahidi kwa kutumia Simu ya Video. Kweli siku moja kabla ya shauri kuwa mbele jaji/hakimu Mwanakwetu alifika katika taasisi husika jirani na kuongozwa namna ya kuutoa ushahidi kukiwa na mambo ya kadhaa ikiwamo utambuzi wa nyaraka za Serikali. Kumbuka Msomaji Mwanakwetu Shahidi wa Jamhuri. Siku ya kutoa ushahidi kwa Simu ya Video ilifika na kuelekea katika taasisi hii mapema kabisa na kufika hapa mawasiliano na wakili wa serikali yalifanyika, alisema kuwa watafika mahakamani kama jaji/hakimu atakavyowaongoza wataomba Mwanakwetu awe shahidi wa mwisho. Kumbuka msomaji wangu shahidi wa Jamhuri ni Mwanakwetu, saa nne kamili wakili wa Jamhuri alipiga simu tena na kumuuliza upo wapi nakujibu kuwa yupo karibu na ofisi yenu, mama huyu akauliza umesoma ujumbe wangu? Mwanakwetu akajibu hapana, mama wakili akamuomba Mwanakwetu asome ujumbe huu.
“Shahidi wa Serikali aende Mahakama Kuu jirani amtafute mwenye namba hii 000000000 anaitwa H….y ajitambulishe atapewa ushirikiano, Asante.”
Mwanakwetu aliposoma ujumbe huu akamijibu huyu wakili wa Jamhuri kuwa nimesoma ujumbe wako Mama Wakili lakini umbali kutoka hapa nilipo hadi Mahakama Kuu ni mbali lakini pia usalama wangu, naomba hili mama wakili nyinyi wenyewe tengenezi utaratibu mlisimamie nifike mahakamani nitoe ushahidi huu wa Jamhuri pia Mwanakwetu akaongeza na haya,
“Dada Wakili kwa uzoefu wangu mazingira ya mahakama tangu za Mwanzo hadi Mahakama Kuu mwenye kuheshimiwa ni Jaji/Hakimu si mtu mwingine, unaweza kuambiwa neno ukafanywa kama na wewe mharifu wakati wewe ni siyo mharifu, sasa hilo mimi binafsi silipendi na ndiyo maana naomba mniongoze nifike Mahakamani Kuu kwa usafiri wenu na ulinzi wenu , nitoe ushahidi na kurudi nyumbani kwangu salama.”
Kwa bahati nzuri wakili huyu wa serikali mama mmoja kwenye simu alionesha muungwana sana anapendeza kuwa mke wa mtu, akamuelewa Mwanakwetu na kwa muda wa dakika tano gari ikafika na jamaa kumuongoza Mahakama Kuu. Mwanakwetu akashangaa anakwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi, akauliza mbona mnanileta hapa ?
Alijibiwa kuwa hapa ni jirani na wanavyo Vifaa Vyote vya Simu ya Video, Mwanakwetu akasema naam sasa Mahakama zetu nyingi zina vifaa vya Simu za Video. Kweli hapo Mwanakwetu alipokelewa na karani mmoja siyo yule H…y wa Mahakama Kuu, Karani aliomba Kiunganishi(link) na Shauri hilo ambalo linaendelea Mahakamani wakati huo Mwanakwetu shahidi wa mwisho. Akiwa hapa kwa karani mahakamani kulikuwa na jamaa wawili wote inaonekana wa walikuwa wamefika kwa karani kuhakiki kukamilika kwa nyaraka hizo za mirathi.
“Kaka nyaraka ya kuzihamishia fedha kutoka akaunti ya marehemu kwenda akaunti ya mahakama hazipo nakuomba uende benki ukachukue sasa hivi ili zikamilike na muda unakwenda.”
Jamaa kando anayeambiwa akajibu,
“Nadhani hii nyaraka, mama atakuwa nayo, jana alikwenda msibani hivyo ngoja arudi, kesho nitakuja nayo hapa utahakiki.”
Karani wa mahakama akasema wewe ndiye msimamizi nyaraka zote kaa nazo wewe,
“Msimamizi ni mimi lakini si unajua huyu aliyekufa alikuwa mumewe, huyu ni mama yangu nina hakika atakuwa anazo tu .”
Mara karani wa mahakama akapokea simu, akawa anaongea huku akijibu kwa maneno haya,
“Ehh kazi zenyewe hamna, watu wakistaafu wanachoka zaidi, eeeh nipo kazini Affidavite ni shilingi 5000 /- ya stakabadhi hii, toa 5000 upate affidavite(kiapo)…”
Karani anaongea na simu huku hawa jamaa wawili ofisini wanaofuatilia uhakiki wa nyaraka za mirathi wanamuongelesha na anajibu. Gafla akaingia mama mmoja kabeba chupa ya chai na vitafunio anauza, nyuma yake akaja dada mweusi mrembo naye anauza chai akaomba cheji ya shilingi 1000/-, hakupata, kisha akaomba shilingi 200/- hakupata, jamaa mmoja mwili mkubwa mfuatilia mirathi akanunua chai na vitafunio viwili.Gafla karani akakata simu akisema baba link imefika twende ukatoe ushahidi.
Mwanakwetu akamfuata mama karani hadi chumba kimoja kikubwa chenye makarani wawili, akaambia kaa hapa na huyu karani aliyekwenda naye. Naye karani huyu kuingia chumbani, gafla karani baba akasema kwa lugha ya ukali, huku karani mama mwenyeji katika chumba hii kakaa kimya tu.
“Haya wewe mzee amkaa hapo, kakae pale.”
Maneno haya ya shuruti, anaambiwa Mwanakwetu kweli Mwanakwetu akaamka na kukaa kiti cha chuma vilivyounganisha. Hapa hapa akakumbuka maneno yake kwa Mama Wakili wa Serikali,
“…Wakili kwa uzoefu wangu mazingira ya mahakama tangu za Mwanzo hadi Mahakama Kuu mwenye kuheshimiwa ni Jaji/Hakimu si mtu mwingine…”
Kweli mama karani alitoka chumbani alifika hapo alipo Mwanakwetu alitoka nae akiwa na kompyuta mpakato na kutafuta chumba tupu ili atoe ushahidi wake.Wakielekea chumba cha kutoa ushahidi kwa simu ya Video, walipita eneo moja Mwanakwetu alikutana na mti mkubwa mkongwe akaupiga picha kisha kuelekea kutoa ushahidi. Akiwa katika chumba hicho akafika Afandemwenye v kama tatu, akauliza eti kuna shauri moja la ubakaji limesajiliwa, karani akauliza lipi?
Askari akajibu la Msukuma aliyebaka, karani akjiabu limeshasajiliwa. Afande akaondoka zake. Mwanakwetu akatoa ushahidi kwanza kwa wakiliwa serikali akiongozwa wakili wa serikalia na baadaye wakili wa utetezi. Ushahidi ulipokamilika Mwanakwetu alimueleza Jaji/Hakimu aliyekuwa anasikiliza shauri husika maneno haya,
“Hongereni sana mahakama kwa kuboresha namna ya kuendesha kesi kwa kutumia simu ya video na hizi pongezi zangu zifike kwa uongozi wa Mahakama Tanzania.”
Pongezi zikapokelewa baada hakimu kusema sawa, Mwanakwetu atafuatilia kama pongezi hizo zitafika kwa wahusika. Mwanakwetu akawa anatoka zake kurudi kwake madongo poromoka.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
HIvi sasa mahakama zetu zimeboreshwa sana lakini yapo mambo lazima yafanyiwe kazi na mahakama yenyewe na mengine ni ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwanza ni hoja ya watumishi wa mahakama wasidhani kila anayekwenda mahakamani ni mharifu wawe na lugha ya staha hata kwa waharifu maana tunapaswa kuyachukia makosa waliyotenda kama mahakama imewatia hatiani lakini utu wao lazima uheshimiwe na kila mmoja wetu , lugha iwe ya staha.
“Tunatakiwa kumuheshimu mtu kwa umri wake, cheo chake na hata mwenendo wake. Kwa hiyo hata mdogo apewe heshima yake pia.”
Shida kubwa ya Mahakama ya Tanzania ni suala la Jaji Mkuu ambaye ndiye Kiongozi wa mahakama kuongezwa muda , ni vizuri Mahakama Kuu ingepata Jaji Mkuu Mpya hii itasaidia sana kutoa nafasi kwa mawazo mapya kuboresha mahakama yetu, nguvu mpya na fikra mpya kutoa mchango mpya katika mahakama, kinyume chake ni kuendekea kuacha fikra zile zile kuendelera kuiongoza mahakama yetu.
“Hizi ni fikra za zamani fikra za Kaka, Hamisi, Daudi, Muuza, Duka, Sokoni, Mwanza. Fikra za latili tunataka fikra mpya.”
Katika taifa la watu milioni 60 kumuongea muda mtu siyo sahihi, Tanzania kuna wakati ilikuwa inaazima majaji kutoka mataifa mengine mathalani kesi ile ya Jamhuri dhidi ya Said Abdallah Mwawindi , Jaji hakuwa Mtanzania lakini sasa taaluma ya sheria inayo wasomi wengi wenye uwezo mkubwa na jambo hili ni la pande mbili anayechagua apime jamii inalitazamaje maana hii ni nafasi ya watu na pili kwa anayechaguliwa mwenyewe na Mungu wake kupima kuwa jamii inakuonaje? Vijana wanahaha kutafuta kazi, hiyo nafasi yako moja ukitoka anasogea mtu na wengine wanapata kazi na wengine wanapanda ngazi. Hata kama tumewekeza katika tekinolojia, tumewekeza katika majengo ya mahakama na miundombinu kuna umuhimu kuitazama rasilimali watu inavyopokezana vijiti kwa wakati na huko ni kuwekrza katika rasilimali watu. Jambo la tatu na la mwisho Serikali ijitahidi kushugulikia suala la usalama wa raia, hoja za watu wasiojulikana linaweza kusababisha mashahidi mahakamani hasa mashahidi wa Jamhuri kutokutoa ushahidi kwa amani na hilo kusababisha serikali kuingia hasara kubwa , maana mahakamani hakutakuwa na haki tena maana kinachoanza ni usalama wa raia kisha haki ndiyo inakuja.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka,
“Shahidi wa Jamhuri.”
Nakutakia Siku njema.
0717649257
Post a Comment