Adeladius Makwega Musoma MARA.
Jioni ya Januari 28, 2025 Mwanakwetu alipigiwa simu na Afisa Habari wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara Mafulu Mjalifu akiuliza,
“Kaka Makwega Upo?”
Mwanakwetu akajibu,
“Nipo.”
Mjalifu akasema,
“Leo, Katibu Tawala Mkoa ndugu Gerald Kusaya alikuwepo Manispaa yetu, mbona sijakuona?”
Mwanakwetu alijibu,
“Kweli sikuwepo, sikufahamu hilo lakini pia nilikuwa katika Kikao cha Mkuu wa Mkoa Mara alichokuwa akifanya na NGOs za Mkoa Mara katika ukumbi mkubwa tangu asubuhi ya Januari 29, 2025.”
Mafulu Mjalifu ambaye ni ndugu anayefahamiana na Mwanakwetu kwa miaka mingi yaani tangu mwaka 2005/2006 akajibu,
“Sawa kaka.”
Baada ya maswali ya Mjalifu kwisha katika simu hii Mwanakwetu akataka kujua katika kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Kusaya alisema nini katika kikao huko Manispaa ya Musoma ambayo ipo hatua chache na zilipo Ofisi ya Mkoa wa Mara?
Mafulu Mjalifu akajibu haya,
“Alizungumzia masuala yote ya nidhamu kwa watumishi wa umma,mavazi na kujibu hoja za ukaguzi kwa wakati, kutembelea miradi kwa wakati, kuwajali watumishi wa hali chini na kutodokoa mali ya umma.”
Mwanakwetu katika hoja hizo zilimvutia sana na hivyo kutaka kuyatarisha makala juu ya kikao hicho maana Afisa Tehama Mkoa wa Mara alimdokeza Mwanakwetu mapema juu ya kikao chao na Katibu Tawala ili Mwanakwetu ashiriki kama mwanahabari .
Mwanakwetu katika haya mawasiliano na huyu huyu muungwana Mafulu Mjalifu ambaye ni kijana mwenye akili nyingi hata alipokuwa Chuo Kikuu Cha Tumaini Iringa wakati akisoma Shahada yake ya Sanaa na Habari wakaagana na Mwanakwetu akimwambia Mjalifu kuwa hivi sasa nakwenda katika kikao cha Katibu Tawala ndugu Gerald Kusaya anafanya na Maafisa Tehama kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara. Kikao chenyewe kipo katika ukumbi mdogo hapa hapa mkoani.
Kwa faida ya Msomaji wa Mwanakwetu hapa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mara kulikuwa na vikao kadhaa, kikao kikubwa kilifanyika ukumbi mkubwa ambapo huko alikuwepo Kanali Evans Alfred Mtambi Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bi Mwatumu Mahiza na wadau kadhaa kutoka NGOs zote za Mkoa wa Mara na huko ukumbi mdogo wapo jamaa wa TEHAMA na Katibu Tawala ndugu Katibu Tawala ndugu Gerald Kusaya. Mwanakwetu akatoka ukumbi Mkubwa huku kikao kinaendelea na kuelekea ukumbi mdogo maana ukumbi mkubwa mambo yalikuwa yanakaribia kumalizika.Mwanakwetu kigulu na njia hadi ukumbi mdogo akashika kitasa na kufungua mlango huu.
Mwanakwetu akafungua mlango wa ukumbi mdogo pole pole na masikio yake yakakaribisha na maneno haya,
“Ni vizruri tukaangalia namna ya kuongeza watumishi, kuna halmashauri zipo katika hali mbaya sana, pale mnapoona mmezidiwa naomba muwatafute wataalamu wangu wa mkoani watakuja kutoa msaada, najua inawezekana mkoa wetu umefanya vizuri katika mfumo huo wa kwa sababu kila halmashauri tuna mtu wa TEHAMA na anatimiza majukumu yake, ukiwa umekwama tujulishe tutume mtu wa kuokoa jahazi maana binadamu unaweza kuwa mgonjwa, upo likizo au mambo mengine ya kifamilia.”
Hapa Mwanakwetu anaingia, siyo kwamba amechelewa hapana bali anajitahidi kila kikao kuweza kuripotiwa katika vyombo vya habari na ndugu Gerald Kusaya Katibu Tawala akizungumza na wataalamu hawa wa TEHAMA. Mwanakwetu alipotazama ukumbi huu ulikuwa umejazwa na dazeni moja na robo ya watu yaani watu karibu 15 wanaume 14 na mwanamke mmoja tu, kikao kinaendelea naye Katibu Tawala Mkoa wa Mara anaunguruma, cha kusikitisha mkubwa huyu ni Shabiki wa Yanga timu ile ya Jangwani Dar es Salaam. Mabingwa wa kupambana na mafuriko ya kila mara jijini Dar es Salaam timu yenye mashaka mengi nchini Tanzania.
“Suala la Usafiri kwa maafisa TEHAMA ni jambo la msingi maana nyinyi ndiye mnaofanikisha hata hili la ukusanyaji wa mapato, bila mfumo madhubuti hatuwezi kukusanya mapato vizuri angalau muwe na gari moja ya kusaidia nyinyi kuweza kufanya kazi zetu vizuri na kwa wakati na uhakika, ninatoa ahadi kwenu nitafanya kikao na Wakurugenzi Watendaji wenu ili niwaeleze hili ninalolisema kwenu nyinyi.”
Msomaji wangu kikao kinaendelea Mwanakwetu ananukuu neno kwa neno na Katibu Tawala akiongea na dazeni hii unusu ya jamaa kutokea Vitengo cha Tehama vya Halmashauri zote za mkoa wa MARA.
“Mnapopata laki tatu, mpo wawili huyu anachukua laki unusu na mwezako laki unusu mpendane, maisha yenyewe ndiyo haya haya, mimi nakumbuka nimefanya kazi kule Rukwa kama Katibu Tawala, hapo hapo Rukwa ipo Halmashauri ya Wilaya inaitwa Nkasiwakati huo hili siyo la sasa hawa jamaa walikuwa na maafisa Tehama wawili lakini walikuwa hawaelewani kabisa na wala hawaongei, hili jambo nimelisimulia hata pale Manispaa ya Musoma asubuhi ya Januari 29, 2025 kila mmoja yupo bize na begi mgongoni kimya kimya, mtu aachi hata chupa ya maji mezani kuogopa kuwekewa sumu, jamani mpo wawili pendaneni.
Mkubwa akiondoka safari hamuachii mwezake hata funguo, sasa hapa kazi mnafanyaje? Uamuzi wangu kama Katibu Tawala nikamchukua huyu mdogo na kumuhamishia mkoani, nilipofanya hivyo tu yule jamaa mkubwa wa ICT kule Nkasi aliyebaki alichanganyikiwa kabisa, akarukwa na kichaa hadi nikajilaumu kwa nini nilifanya uhamisho wa yule kijana, hadi ninaondoka hali ilikuwa hivyo. Jamani ujumbe wangu mnapofanya kazi pamoja pendaneni.”
Kikao kinaendelea na sasa majira ya jioni, Katibu Tawala alitoa nafasi ya wataalamu hao wa TEHAMA kuuliza maswali na hata kushauri katika jambo moja na lingine, kikaoni uwanja ukawa wazi. Baadaye Katibu Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Kusaya alitoa majibu ya hoja kadhaa na hoja zingine kuzipokea ili kutoa muda wa utekelezaji kwa kuwaelekeza Wakurugenzi Watendaji wote wa Mkoa wa Mara.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika huyu ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara ndugu Gerald Kusaya akizungumza na watumishi wake wa umma na kujibu hoja kadhaa, je wewe unayesoma haya makala kwenu huku hali ikoje? Iwe mkoani, Wizarani au Taasisi yoyote ya umma mnapata nafasi hiyo? Kama mambo yanafanyika hivyo ni vizuri na jambo la heri na kama mambo yanakwenda mrama makala haya shabaha yake wewe unayeyasoma ujifunze kutoka Mkoa wa Mara uwe mkubwa namna gani na hata uwe mdogo namna gani.
Kwa hakika changamoto za watumsihi hawa wa Vitengo vya TEHAMA zinaweza kuwa ni changamoto sampuli za Maafisa TEHAMA nchi nzima mathalani wanapewa bajeti geresha kila mwaka wa bajeti lakini hawaruhusiwi kabisa kutumia fedha hizo, hawana vitendea kazi kama vile usafiri wa uhakika , hawashirikishwi katika shughuli kadhaa za kitendaji mathalani ukaguzi wa miradi.
Mnaofanya hivyo mnakosea mnasahau kuwa sasa ulimwengu wetu umeshahama kutoka analojia na upo katika ulimwengu mwingine wa digitali ambapo TEHAMA ndiyo mpango mzima.
Ndiyo kusema kutowathamini wataalamu wa TEHAMA ni kuendelea kupanda Gari la Analojia ambalo Mwanakwetu anasema ni gari lisilo na magurudumu na haliwezi kutufikisha popote maana gari la digitali ndilo linaloweza kutufikisha sehemu sahihi likiwa na magurudumu salama.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Kutowathamini Wataalamu TEHAMA Kuendelea Kupanda Gari Lisilo Magurudumu.”
Nakutakia siku Njema.
makwadeladius @ gmail.com
0717649257
MB-Makala haya yametayarishwa na MwAnAkWeTu kwa heshima na Mafulu Mjalifu, Afisa Habari wa Manispaa ya Musoma ambaye alipokuwa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa mwaka 2006-2009 alifahamika kama mwanachuo bora mwenye akili nyingi.
Post a Comment