Jina La Yesu,Salamu
All Hail the Power
1. Jina la Yesu, salamu! lisujudieni,
Ninyi mbinguni, hukumu, Na enzi mpeni.
Ninyi mbinguni, hukumu, Na enzi mpeni.
2. Enzi na apewe kwenu, watetea dini;
Mtukuzeni Bwana wenu, Na enzi mpeni.
Mtukuzeni Bwana wenu, Na enzi mpeni.
3. Enyi mbegu za rehema nanyi msifuni;
Mmeponywa kwa neema, Na enzi mpeni.
Mmeponywa kwa neema, Na enzi mpeni.
Hayo ni baadhi tu mashairi na kiitikio cha wimbo maarufu kama na ENZI MPENI ukiimbwa katika Kanisa la Mtakatifu Peter hapa Rorya mkoani Mara, mbele ya Mungu , mbele ya madhabau yake na mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Dkt. Isidori Mpango katika Harambee ya kuchangia maendeleo ya Dayosisi ya Rorya ya Kanisa la Angilikana Tanzania huku akiwaomba waamini wa kanisa hilo kuliombea taifa la Tanzania na kuendelea kuwalea waamini wake katika maadili.
Wimbo huo jina lake halisi ni Jina la Yesu Salaam ukimgusa kila anayeshiriki harambee hii mara baada ya kuanza kuimbwa kanisani hapo. Haya yakifanyika Februari 28, 2025 katika Kanisa hilo Mwanakwetu akishuhudia na Serikali ikisisitiza
“Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu na itaendelea kuwa bega kwa bega na taasisi zote za dini nchini Tanzania na serikali inatambua waamini wenye kufuata miongozi miema ya dini zao hawawezi kuwa na tabia mbaya kwa taifa lao.”
Kanali Mtambi akinukuu neno kwa neno kutoka hatuba ya Makamu wa Rais pia aliwaomba waamini hao wakumbuke kushiriki katika masuala kadhaa ya kitaifa ikiwamo uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 2025.
“Serikali inatambua mchango wa kanisa kwa miaka tele katika masuala kadhaa ya maendeleo, ikiwamo elimu na tiba, endeleeni na moyo huo kushiriki katika shughuli zenu za maendeleo na mambo yote ya taifa letu,”
Awali akimkaribisha mkuu wa Mkoa wa Mara , Mkuu wa Wlaya ya Rorya Dkt. Khalifani Haule alisema kuwa anachangia mifuko 100 ya saruji na anatambua mchango mkubwa wa Kanisa la Anglikhana Wilayani Rorya na viongozi wa kanisa hilo ni wa kupigiwa mfano kwani katika kila kikao vya kiserikali wanavyopewa mialiko wanashiriki.
Awali lilisomwa neno la utangulizi katika Harambee hiyo kutoka kitabu cha Wakoritho wa 2 sura ile ya 9 mstari wa 1 hadi wa 7,
“Hakuna sababu ya kuwaandikia kuhusu msaada unaotolewa kwa ajili ya watu wa Mungu, kwa kuwa ninajua mlivyo tayari kutoa, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili yenu kwa watu wa Makedonia, nikiwaambia kuwa ninyi wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana. Ari yenu imewachochea wengi wao kuanza kutoa. Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusije kukawa ni maneno matupu, bali muwe tayari kama nilivyosema mko tayari. Isije ikawa nitakapokuja na watu wa Makedonia nikute hamko tayari niaibike, na ninyi zaidi, kwa kuwa nilishasema mko tayari. Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kabla yangu, wafanye mipango yote ya matoleo ya zawadi mliyoahidi ili iwe tayari, si kama mchango wa kulazim ishwa bali kama zawadi ya hiari. Kumbukeni kwamba, mtu anayepanda mbegu chache, atavuna mazao machache; na mtu anayepanda mbegu nyingi atavuna mazao mengi. 7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa kusita au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu anapenda mtu anayetoa kwa moyo.”
Baba Askofu wa Dayosisi ya Rorya mchungaji Moses Yamo Masala kusoma neno hili alifafanua neno hili akisema;
“Sura hii ya tisa kutoka kitabu cha Wakoritho, Paulo Mtume anaagiza mambo kadhaa kwa Wakristo ikiwamo kutoa sadaka kwa furaha maana katika kutoa kuna kupanda na anayetoa haba hupanda haba na mwisho huvuna haba.”
Harambee hiyo iliwakutanisha Maaskofu kadhaa wa Kanisa la Anglikana Tanzania viongozi kadhaa wa madhehebu na dini nyingine huku waaamini wa Kanisa hilo wakijumuika na wakazi kadhaa wa Rorya na mkoa mzima wa Mara katika kufanikisha shughuli hii ya kiroho.
Harambee hii kwa hakika imefanyika kwa kufana mno, huku Makamu wa Rais ndugu yetu Dkt Isidori Mpango amechangia shilingi milioni 10, Mkuu wa Mkoa mara amechangia mifuko 300 ya saruji huku waamini hao kutoka kila kaya na kila kanisa walitoa michango yao hiyo ikiwa safari ya kupatikana milioni 250.
Katika Harambee hii jambo la kufurahisha sana lilikuwa ni Baba Askofu mmoja alianzisha Harambee ya kushindana baina ya Simba na Yanga., Kiongozi wa Kapu la Yanga alikuwa Kanali Evans Alfred Mtambi lilikuwa na watu wengi. Kapu la Simba lilikuwa tupu halikuwa na watu wengi, huku Yanga ikipata michango mingi . Msomaji wnagu kumbuka Mwanakwetu Simba Damu, alichuku mchango wake na kuuweka katika kapu la Simba kwa siri maana bosi mkubwa Kanali Mtambi ni Yanga hauwezi kwenda tofauti na mkubwa wazi wazi na kwa bahati mbaya Smba ikalala dolo katika Harambee hii Yangu kuibuka kidedea.
Hayo yote yakifanyika kwa amani nayo hali ya hewa ya eneo la Kowak hapa Nyathorongo Rorya jua lilikuwa la kadil,i huku hakukuwa na wingu lolote tangu Mkuu wa Mkoa wa Mara anafika hadi zoezi hili linakamilika.
4. Wenye dhambi kumbukeni ya msalabani.
Kwa furaha msifuni, Na enzi mpeni.
Kwa furaha msifuni, Na enzi mpeni.
5. Kila mtu Duniani msujudieni,
Kote-kote msifuni, Na enzi mpeni.
Kote-kote msifuni, Na enzi mpeni.
6. Sisi na wao pamoja tu mumo sifani.
Milele sifa ni moja, ni "enzi mpeni".
Milele sifa ni moja, ni "enzi mpeni".
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Endeleeni Kuwalea Waamini Kimaadili.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
NB Makala haya yametayarishwa kwa heshima zote kwa Kanisa la Anglikana Tanzania.

Post a Comment