JAMBAKOTI KUTOKA ARABUNI

 



Fredrick Mfugale &mkewe

 

Adeladius Makwega-Barabara ya Lobinaa Dodoma.

 

Nilipokuwa mdogo nilikuwa rafiki yangu mmoja anayefahamika kama Fredrick Robert Mfugale huyu n mtoto wa Profesa Robert Mfugale ambaye ni mjuzi wa lugha ya Kiingereza na Kifaransa. Rafiki yangu huyu anazaliwa na Baba Mhehe/Mbena na Mama yake ni Mpogolo.

 

“Kwa hakika Wahehe/Wabena wa Iringa Mjini, Kilolo, Ilula, Kalenga hawa ni Wahehe ambao wapo jirani sana na Morogoro na ndiyo maana mahusiano ya Wahehe hao kuoleana na watu wa Morogoro ni jambo la kawaida tangu enzi.”

 

Tulipokuwa wadogo Fredrick Mfugale tulimpa jina la utani la Black Fish, ndugu huyu ndiyo kusema, rafiki yangu huyu wa utotoni ananifahamu vizuri na mimi namfahamu yeye vizuri sana. Nyumba kwao ni Mbagala Kwa Mangaya, nakumbuka wakati huo watu waliohamishwa kutoka Azimio, Temeke na Tandika kupisha barabara walipewa viwanja eneo la Mangaya wakahamia hapo, ndipo ninmakakutana na ndugu yangu huyu kwa mara ya kwanza. Wao walikuwa wanaishi Tandika Magorofani, hamisha hamisha hiyo walipata kiwanja wakajenga nyumba yao Mbagala Mangaya, hapo Fredrick alikuwa na kaka zake wengi, ugomvi wa watoto ilikuwa ngumu sana kupambana nao maana ukoo mzima ungeweza kukufuata ulipo. Jamaa hawa hawakuwa wagomvi, walikuwa watu wema, wakarimu na wanyenyekevu.

 


Nyumba ya akina Mfugale ilikuwa mkabala na nyumba ya familia moja ya Mzee Bofu, hii familia ya Bofu ilikuwa ni familia inayoisihi maisha ya Uisilamu sana huku familia ya Mfugale wakatoliki Kindakindaki huku Profesa Robert Mfugale alikuwa anaimba Kwaya Kanisani Mbaga;a Zakhem. Kwa hakika Ukristo wa akina Mfugale na Usilamu wa akina Bofu ulionekana katika maisha ya kila siku.

 

Kwa wale majirani waliyokuwa wakiitazama hizi familia kwa mbali na hata kwa karibu hawakuhitaji kuambiwa maisha wanayoishi.

 

“Mzee Bofu alikuwa na wake wawili mkubwa na mdogo, wale kina mama walikuwa wanapendena sana. Sikujaliwa kuona familia kama ile tena yenye upendo mkubwa miongoni mwao na ndiyo maana leo naisimulia. Chakula anapika mke mkubwa kesho yake anapika mke mdogo na watoto wa familia hii chakula walikula kwa pamoja iwe chai , cha mchana na hata chajioni, kila siku kwa pamoja Mwanakwetu. Kikipikwa, kinapakuliwa na kutengwa pamoja, familia nzima watoto kiume upande wao na mabinti upande mwingine huku Mzee Bofu anakaa na wake ze wanakula kwa amani kabisa.”

 

Kama wanakwenda sokoni mara nyingi akina mama hawa walikuwa wanaongozana pamoja mke mkubwa na mdogo, suala la mavazi kwa mujibu wa dini yao hilo kwao lilikuwa siyo jambo la kulisimulia maana lilizingatiwa mno.

 

Nakumbuka Wakati tukiwa tunacheza mara nyingi niliona mke mkubwa/mke mdogo anafika kuwaita watoto wote kwa chakula kula pamoja kama nilivyosimulia.

 

Mzee huyu yeye na wake zake walikuwa Wandengereko wa Rufiji na nyumba yao ilikuwa inapakana na Barabara ya Mangaya na kando yake ulikuwepo Masjidi(Msikiti) Sinina, msikiti huu wakati huo ulikuwa ndiyo unajengwa. Familia ya Mzee Bofu ndiyo waliokuwa wanasimamia msikiti huo kwa masuala hasa ya kupiga azana na kufanya usafi.

 



Kando ya Msikiti huo kulikuwa na Madrasat Sinina kwa hiyo watoto Wakiislamu wote walisoma shule hii ya dini hapo hapo. Mandhari kando ya msikiti zikisikika sauti konsonati na Irabu za Kiarabu.

“'alif, Bā', Tā', Thā'… Wāw, Yā', Hamza, Fathah , Dammah, Kasrah.”

 

 

Ijumaa ikifika wake wa Mzee Bofu kwa pamoja walivalia nguo zao nadhifu wanakwenda kusali Msikiti wa Ijumaa Masjidi Salama(Mbagala Kizuiani) kwa sababu Masjidi Sinina wakati huo haukuwa Msikiti wa hadhi ya Ijumaa. Wake wa Mzee Bofu walipendana sana hakuna mtu mtaani hapo ambaye alipata ushahidi wa wakati huo kuwa hawa akina mama mmoja wao amewahi kumpandishia sauti mwenzake na hata watoto na ndugu wa familia hiyo hawakuwa na ushahidi wa tukio kama hilo.

 

Kumbuka Mwanakwetu na rafiki yangu Fredrick wako jirani nah ii familia na pia jirani na Masjid Sinina, tangu wakati msikiti unajengwa tulikuwa tukishuhudia wageni mbalimbali na hata wale waliotokea Arabuni kufuatilia ujenzi wake. Ujenzi uliendelea huku kukiwa na Msikiti Mdogo ukitumika kusali zile sala tano za siku yaani; Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi, na Ishaa huku wale akina Hamsa Salawati familia ya Mzee Bovu ikiwajibika ipasavyo, baadaye hii Madrasa ilikamilika na kubakia ujenzi wa Msikiti kama kuna taasisi ya dini ya ikiwa wafadhili huwa lazima wawe wanatembelea taasisi wanayohifadhili.

 

“Kuna siku walifika wageni kutoka Arabuni wakakagua ujenzi huo wa Msikiti na Madrasa vizuri sana wakazungumza na kutoka nje na kutukuta watoto tunacheza. Wale Waarabu wakazungumza na watoto wa madrasa huku mkalimani akitafsiri kutoka Kiarabu kwenda Kiswahili. Gafla likatolewa robota za nguo nyingi akakabidhiwa Shekhe Waziri (mwalimu wa madrasa) akaambiwa atugawie watoto wote tuliokuwapo hapo.

Kweli watoto wote tulipata nguo hizo mimi na ndugu yangu Fredrick Mfugale tukapata vizibao(jambokoti) na nadhani kwa kumbukumbu zangu mimi na Fredrick hivyo vizibao vilikuwa vya kwanza kuvivaa tangu kuzaliwa.

 

Vizibao hivyo Mwanakwetu vilikuwa vizuri sana, vina nakshi ya maua maua yaliyokozwa rangi ya dhahabu kwa mbele na vifungo vyake rangi ya dhahabu. Siku hiyo kila mtoto pale mtaani waliokuwa wanasoma shule hii ya dini ya Kiisilamu walirudi nyumbani na nguo mpya mkononi. Shekhe Waziri alitambua fika kuwa Mwanakwetu na Fredrick Mfugale tumepata nguo hizo na ni Wakristo na siyo wanafunzi wake.

 

Shekhe Waziri alikuwa anatambua fika sisi tulikuwa tunashinda kando ya Madrasat Sinina tukiwangoja wenzetu tukacheza nao, akituambia njoni msome, tukimjibu sisi Wakristo. Eneo hilo lilikuwa na miembe mikubwa na palikuwa kivuli cha kutosha na palikuwa na uwazi mkubwa wa kuweza kucheza mpira wa miguu wa magoli madogo au mchezo wa one touch. Tuliporudi nyumbani na vizibao kutoka Arabuni, vizibao vya gharama, vizibao hivyo hata mashekhe wakubwa pale mtaani hawakuwa navyo, Mwanakwetu maswali yalikuwa mengi, haya bwana Fredrick umebadilisha dini?

 

‘Ahaa jamani hapana wamekuja Waarabu wa Oman wametoa nguo kwa watoto wa Madrasat Sinina wengi, siyo mimi peke yangu.’

 

Haya wewe unasoma hapo madrasa? ‘Hapana mimi nilikuwa nawangoja wenzangu tukacheze, ndiyo nikapewa Kizibao, siyo mimi peke yangu na hata Adeladius kapewa Kizibao.’ Fredrick Mfugale mtumikiaji wa kanisani alitoa majibu hayo. Haya sasa haya muite na huyu Mwanakwetu haraka.

 

Nikatafutwa kwenda kwa akina Fredrick kutoa maelezo ya kina na mama yake Fredrick ambaye alikuwa mwalimu mahiri wa Darasa la Kwanza Shule ya Msingi Gerezani Ilala Dar es Salaam wakati huo.”

 

Mwanakwetu nikaulizwa huko kulikuwa na nini? Maana hizi habari za Vizibao hatuzielewi.

 

Mwanakwetu ambaye nayeye ni mtumikiaji wa Kanisani alipoulizwa akajibu,

“Hatujabadilisha dini, sisi walitukuta uwanjani tu na huo mgao tukapata.”

 

Mke wa Shekhe Waziri alifuta nyumbani kwake nay eye alipoulizwa alieleza kwa kina kilichotokea, kwamba mumewe alifanya jambo la kiungwana kwamba hata kama Adeladius na Fredrick ni Wakristo kuwamyima nguo hizo isingekuwa haki maana Waarabu wenyewe wapewe watoto wote waliokuwapo hapo na wao walikuwepo.

 

Profesa Robert Mfugale akiwa na mkewe ,mwalimu wetu aliyetupa changamoto ya jambakoti

Msomaji wnagu hapo kidogo ndiyo pona pona na kuruhusiwa kuvivaa vizibao hivyo.

Kwa hiyo hivyo vizibao vyenye nakshi ndiyo tukapata vibali vya kuvivaa. Hapo msomaji wangu hapo vizibao vilishakuwa mikononi mwa wazazi,

 

“Kizibao kilishawekwa mezani kikimngoja Mzee Mfugale, Huyu mama Mwalimu wa Darasa la Kwanza alipotoka kwa Mke wa Shekhe Waziri ndipo tukakabidhiwa vizibao vyetu.”

 

Sasa hata jumapili tulivivaa na kuingia navyo kanisani vilikuwa vigumu sana, havipauki wala kuchujuka rangi zake. Tulipokuwa tunavivaa kanisani tukitumikia ukivaa kanzu za waministranti Kizibao kilikuwa kinamulikamulika yale maua yake ya rangi ya dhahabu, kwa hiyo kinavuliwa kinabaki Sakaristia unabaki na fulana unavaa kanzu unatumikia misa, ikiisha misa unakivaa Kizibao chako unarudi zako nyumbani.

 

Sasa wakati tunarudi nyumbani tukawa tunazungumza na Fredrick, huko pale mbele kanisani unatumikia umeshika maji ya Baraka umevaa kanzu yako vizuri alafu Kizibao kinamulika mulika ndani ya kanzu, waamini wanaimba,

 

“Uninyunyizie maji Ee Bwana, Ee Bwana unioshe nitakase, Ee Bwana unioshe ni nitakase.”

Waamini wanaweza kushangazwa huyu mmnistranti mbona anawakawaka kwenye kanzu yake ukaleta taharuki kanisani kwa hiyo kukivua Kizibao hicho kabla ya Misa lilikuwa jambo la muhimu sana.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Kikubwa Mwanakwetu amemkumbuka rafiki yake Fredrick Robert Mfugale aka Black Fish ambaye ni Afisa huko TANAPA, Kaka Fredrick nakukumbusha tu simulizi hii ya Jambakoto Kutoka Arabuni. Nawe Fredrick ukiisoma simulizi hii uwasilimue wanao na wajukuu zako hali ya maisha ya enzi zetu hasa mahusiano baina ya familia za Kikristo na Kiisilamu mtaani huko Mbagala Dar es Salaam.

 

Nawewe unayeyasoma makala haya kama lipo la kujifunza basi jifunze kutoka makala haya ambalo ni tukio la mwaka 1987.

 

Mwanakwetu upo?

 

Kumbuka ,

“Jambakoti Kutoka Arabuni.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

 

0717649257 

 
















 

 

0/Post a Comment/Comments