WEMA WANENEWE MEMA WABAYA WALAANIWE.

 


Samson Richard – Mwanza.

Februari 14, 2025, ulimwengu wa Katoliki ulitaharuki baada ya Vatican kutoa taarifa rasmi kuhusu hali ya afya ya Baba Mtakatifu Papa Francis kulazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli, Roma, kwa ajili ya vipimo na matibabu ya ugonjwa wa mkamba (bronchitis). Hali yake ilibadilika kuwa nimonia pande zote za mapafu, na Vatican ilitoa taarifa rasmi kuhusu hali yake ya afya tarehe 23 Februari 2025.

Kiongozi huyu wa Kanisa Katoliki duniani, ambaye amehubiri amani, mshikamano, na huruma kwa zaidi ya muongo mmoja, amekuwa akikabiliwa na changamoto za kiafya zinazoibua mijadala na maombi kutoka kwa waumini kote ulimwenguni.

Mwanakwetu, unaposoma haya, fikiria macho ya waumini yaliyoinuka kwa shauku kuelekea Vatican, wakisubiri taarifa kuhusu mtu aliyewagusa wengi kwa uongozi wake wa kipekee.

Katika kutafakari nafasi yake katika historia, kuna matukio mawili yaliyonigusa kuhusu Baba Mtakatifu huyu ambayo lazima nikushirikishe msomaji wangu wa Mwanakwetu.



Tukio la Kwanza ni Julai 2022, Papa Francis alifanya safari ya kihistoria nchini Canada, akikutana na jamii za asili zilizoteswa na mifumo ya zamani ya shule za misionari. Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya Vatican, alisema:

"Tunapaswa kukiri makosa yetu. Kanisa halipaswi kuwa ngome ya upendeleo bali nyumbani kwa wote."



Hotuba hiyo iliashiria moyo wa toba na uadilifu wa kiongozi huyu ambaye alitumia miaka yake madarakani kuleta mageuzi makubwa ndani ya Kanisa Katoliki. Alisimama kama sauti ya maskini, mhamasishaji wa amani na mpiganiaji wa haki za kijamii.


Tukio la Pili ni Disemba 2024, Papa Francis alilazwa kwa mara nyingine katika hospitali ya Gemelli, Roma, akisumbuliwa na matatizo ya kupumua. Hali yake iliwatia hofu wengi, huku ripoti zikionesha kuwa umri wake wa miaka 88 ulikuwa unamletea changamoto zaidi za kiafya.

Pamoja na matatizo hayo, aliendelea kuzungumza kwa njia ya video na waumini, akihimiza mshikamano wa kimataifa katika kusaidia wahanga wa vita vya Gaza na Ukraine.

Katika hotuba yake moja, aliuliza swali lililogusa wengi:

"Je, binadamu tumesahau maana ya upendo? Kwa nini mateso ya wengine hayaumizi mioyo yetu?"



Mwanakwetu, kumbuka, haya ni maneno ya mtu aliye na mwili dhaifu lakini moyo thabiti.


Mwanakwetu anasema nini siku ya Leo?


Kama ambavyo jamii hupuuza wema wa viongozi bora hadi wanapokosekana, hali ya afya ya Papa Francis imewafanya wengi kutafakari urithi wake. Hili linatufundisha kuwa tukiwapokea viongozi wenye nia njema, tuwathamini mapema na sio tuwasifu baada ya kupotea.

Wananchi wa Vatican na dunia kwa ujumla wanamshuhudia Papa Francis kama kiongozi aliyebadilisha mwelekeo wa Kanisa Katoliki na kupaza sauti kwa wanyonge. Hata wale waliompinga, sasa wanakubali kuwa ni mtu aliyeleta mageuzi yenye maana.



Katika mwanga wa haya, tunapaswa kujiuliza: Je, tutaendelea kumnenea mema mtu huyu akiwa nasi, au tutangoja historia ituandikie kumbukumbu zake?


Papa Francis, safari yako ya imani na uadilifu itaendelea kuwa mwanga kwa wengi, bila kujali dhoruba zinazokukumba.


Mwanakwetu upo?

Kumbuka tu:
"Wema Wanenewe Mema, Wabaya Walaaniwe."

Nakutakia siku njema.











0/Post a Comment/Comments