Adeladius Makwega-Manyoni SINGIDA
“Eee Mungu Mwenyezi, utujalie tuzidi kulifahamu Fumbo la Kristo , kwa njia ya mazoezi ya kipindi cha Kwaresma tunachojaliwa kila mwaka, na kwa njia hiyo tuyafuata yale yanayotokana na kwa fumbo hili kwa mienendo inayostahili, kwa njia ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mwanao, Katika Umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu milele na milele ...”
Haya ni maneno yanayotamkwa na Padri Enhart Mpete wa Kanisa Katoliki katika mojawapo ya Ibada ya dominika, hatua za mwanzo kabla ya kusomwa masomo ya jumapili hii ambayo Mwaanakweu alisali Machi 2025.
“Bwana awe nanyi … Awabariki na kuwalinda Mungu Mwenyezi, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu … Nendeni na amani…..”
Hapa pia ni Padri Enhart Mpete kutoka Shirika la Rosimini Jimbo Katolikil la Tanga akihitimisha ibada ya Misa ya Dominika Takatifu na hapo akitoa Baraka ya Mwishoni kwa misa hii ambapo pia Mwanakwetu alisali. Swali ambalo lipo ubaoni ni je jamii yetu inatambua hatua ambazo Padri anapitia hadi kuwa Padri? Hili kuufikia Upadri huo vijana wadogo wa kiume Wakatoliki huanza masomo kwa elimu ya msingi, kisha elimu ya sekondari alafu ndipo hujiunga na Seminari Kuu na hujifunza hadi kufikia UPADRI.
Msomaji wangu unaweza kujiuliza leo vipi Mwanakwetu anaandika juu ya nini?Jibu lake ni hili;
“Hii ilikuwa ni siku ya Jumamosi, huku Mwanakwetu na wenzake watatu walikubaliana kuwa kesho yake watafanya kazi fulani pamoja lakini mmoja miongoni mwao alisema yeye atadamkia kanisani kusali Jumapili, hivyo aliomba kwa hisani ya wana kundi hili kazi hii ifanyike baada ya misa ya kwanza.”
Saa mbili kamili ya jumapili husika wakakutana na kuanza kazi hii na kuifanya hadi muda wa chai, wakanywa chai na kurudi kazini, huku mchana wakisema wamuombe mama ntilie alete chakula hapo hapo walipo, kweli mchana waliletewa chakula hicho na kutupa mawe pangoni. Wakiwa katika kazi hiyo kukawa na mjadala juu ya Padri Sawala ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano pale Baraza la Maaskofu Katoliki(TEC), kama walivyokuwa akina Padri Paul Haule zamani wakirusha vipindi vyao katika vyombo vya utangazaji vya serikali katika Vipindi vya Inueni Mioyo,Tumsifu Mungu Tumshukuru Mungu, Tumuabudu Mungu, Kumekucha, Kumkuchwawa na hata Kipindi cha Hii ni Kwaresma, nazo sauti zao Mapadri hawa zikijulikana kwa jamii ya Watanzania. Mjadala ulikuwa mkubwa sana huku jamaa mmojawapo akisema Padri Sawala sasa yupo Shinyanga katika mojawapo ya Parokia.
Ndugu mmoja miongoni mwetu ambaye alikuwa mdogo kiumri akasema jamani tena niwambie jambo, mmenikumusha kitu, wiki iliyopita kuna mwezake mmoja amepata upadri ambaye walisoma wote kidato cha kwanza hadi cha pili seminari.Maelezo haya yalimgusa Mwanakwetu akitaka kujua inakuwaje rafiki wa huyu ndugu amepata Upadri na kwanini ndugu huyu hakuweza kulifikia daraja hili? Mjadala ukanoga huku kazi hii inafanyika vizuri. kuhakikisha kazi inakamilika maana kazi hii kutokamilika ilikuwa ni kuongeza gharama zaidi ya muda na fedha.
“Mimi nilimaliza darasa la saba kutoka katika shule zetu hizi za kawaida, nikaomba kujiunga na seminari vizuri tu nikitamani kweli niwe Padri, nilipojiunga na mojawapo ya seminari nilipewa sharti nikae mwaka mmoja shuleni kujifunza baadhi ya mambo ikiwamo maadili na taaluma kabla ya kuanza kidato cha kwanza mwaka 2007 na 2008 nikajiunga kidato cha kwanza na mwaka mmoja baadaye yaani 2009 ndiyo nikawa kidato cha pili.
Nikiwa kidato cha pili mwaka huo huo kulikuwa na msimu wa mashindano ya UEFA, Mimi na wezangu tukiwa tunatoroka seminari kisha tunakwenda kutazama mechi hizo, nilikuwa mpenzi mkubwa wa mchezo wa Mpira wa Miguu.
Siku moja tulikwenda kutazama mpira wakati tunarudi tukashikwa na kisha kuandika barua, nakupewa onyo mimi na rafiki yangu tuliyekuwa naye, yeye analala kitanda cha juu na mimi kitanda cha chini. Siku nyingine kulikuwa na mechi nzuri sana baina ya Manchester United na Bacelona FC, mimi nilibakia bwenini kwa kuwa nilikuwa mgonjwa tu lakini wezangu wawili wakaenda kutazama mechi hiyo katika vibanda uumiza, Mechi ilipokwisha wakaanza safari ya kurudi Seminari.Walinzi wakashtuka hivyo wakawazuia kuingia kupitia eneo ambalo lilikuwa rahisi kupenya, hivyo jamaa wakakata shauri na kuruka senyenge na kuingia shuleni kulala. Sie bwenini hakuna mtu anayetambua kilichotokea zaidi ya kujua tu matokeo ya UEFA yalikuwaje kupitia wao.
Kulipokucha ikapingwa kengele ya dharura tukafika mstarini na kuambiwa sote tukavae fulana zetu za shule na turudi mstarini, kweli kila mmoja alifanya hivyo.
Mimi bwenini naisaka fulana yangu siioni, tafuta tafuta na wewe, huyu mwezangu baadaye akaniambia unajua fulana yako jana niliivaa nilipokwenda kutazama mpira lakini nilianguka katika matope, hivyo nimeifua usiitafute. Basi kweli tukarudi mstarini na mimi kumueleza Padri kama alivyoniambia mwezangu kuwa fulana yangu nimeifua nikisema nimeifua.
Padri huyu akaachana na wote kisha kuambatana na mimi hadi bwenini, ile tunafika bwenini fulana yangu naikuta ipo kitandani kwangu ni chafu huku imenyofoka kipande chake kwa nyuma ambacho kilikuwa na ufito(mstari) wa rangi rangi. Padri akasema wewe ndio tulikuwa tunakutafuta, unaona hichi kipande cha fulana yako kilinasa katika senyenge mlipokuwa mnaruka senyenge kutoka kutembea usiku mitaani.
Mliporuka senyenge kilinasa , walinzi waliniletea sasa twende ofisini, twende ofisini. Kweli tulienda ofisini nikapewa barua ya kufukuzwa shule hapo hapo. Nikarudi nikafunga vitu vyangu , wakati nafunga vitu vyangu, jamaa mwenzangu wa kitanda cha juu amechanganyikiwa haamini kinachotokea lakini ndiyo hivyo, huku akisema yaani samahani sana yaani unafukuzwa kwa sababu yangu! lakini yaani hili tukio kama ningefukuzwa mimi baba yangu angeniua.
Akilini mwangu nasema huyu jamaa maana yake anasema afadhali ya mimi kufukuzwa! Nikarudi nyumba, nikamueleza baba kama ilivyokuwa akaenda shuleni kuelezea ilivyokuwa lakini hawakuelewana na Padri na hakuna mtu mwingine aliyeelewa. Nikatafutiwa shule nyingine na kufanya mtihani wa kidato cha pili na kuendelea na masomo, hivyo ndivyo Ndoto Yangu ya Upadri ilivyopotea.
Nilifukuzwa kwa kosa la kudanganya kuwa fulana yangu nimefua na kosa na kutoka nje ya shule usiku huku Makosa Yote Haya Hayakuwa Yangu.”
Msomaji wangu kumbuka jamaa hawa na Mwanakwetu wanafanya kazi hiyo, huku huyu kijana kando akisimulia tukio hilo hatua kwa hatua.
“Baadaye huyu kijana aliyesababisha nifukuzwe aliwaambia shule kuwa yeye ndiye aliyefanya kosa hili kwa inavyosemekana lakini hawakulielewa hilo kabisa, jamaa akabaki na kusoma na Juma Lililopita Kawa Padri.”
Msomaji wangu kumbuka katika kundi hili lkuna watu watatu, Mwanakwetu ananukuu neno kwa neno kisa chote na hii ilikuwa mwaka wa 2023.Mwanakwetu alimuuliza huyu ndugu je katika kisa hiki huyu msimuliaji anapata funzo gani? Jamaa huyu alijibu haya;
“Huyu rafiki yangu ambaye sasa ni Padri kama akiwa mwalimu au kiongozi wa taasisi pahala popote kama ni mtu anayeweza kujitafakari moyoni hawezi kufanya maamuzi kwa kukurupuka, kwa kuwa anajua moyoni mwake fulani bini fulani alitolewa sadaka, mimi nikapona hadi leo hii Padri.
Pili, siyo watu wote wanaohukumiwa, wapo sehemu mbaya leo hii kwa makosa waliyoyafanya, wengine wameonewa tu. Jambo la mwisho tutambue kuna watu wengine wanakuwa sehemu fulani kuwa madaraja kwa ajili ya mafanikio ya wengine.
Mwisho wewe unayefanikiwa kwa namna hiyo jitahidi mno kuwa mfano mwema kwa wengine, maana upo hapo kwa neema za Mungu tu, wapo watu wameharibikiwa kwa sababu yako, wapo wamekuwa sadaka kwa sababu yako.”
Tulifanya kazi ile vizuri na kuimaliza, tukala chakula cha jioni, Mwanakwetu akakabidhiwa na kisha kila mmoja kuchukua njia yake. Naye Mwanakwetu akikumbuka Mathayo 25, 35-40 Yesu mwenyewe ananadi haya;
“Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.’ Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme ‘Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji? Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika? Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?’ Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.”
………………………………………………………………………………………………….
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kisa hiki cha seminari ni kisa cha kweli na kisa mfano hata duniani katika maisha ya kazi, zipo taasisi nyingi zinakaa na watoto wa watu na kuunda jumuiya zao, wakiweka kanuni, taratibu na sheria hilo halina shida ili maisha yaende. Tunapokaa pamoja sisi ni binadamu na ni jambo la kawaida kutokea changamoto kama zile za vijana wa seminari kwenda kutazama mpira na kadhalika, ikitokea changamoto hawa vijana wetu wanasimulia kwa ndugu zao kule walipotokea, kule walipozaliwa maana Damu Nzito Kuliko Maji,
“…Kule bwana kuna hiki na hiki nalkule bwana hivo na vile…”
Wale wanaosimuliwa wanaweza kukata tamaa kwenda katika taasisi hizo au kukataa kupeleka watoto wao .
“… huko hakuna kwenda, maana umesikia alichofanyiwa fulani…umesikia alichofanyiwa mtoto wa fulani…”
Binadamu namna alivyo anahitaji kuwa salama na siyo kuishi sehemu hatarishi iwe kwa kigezo cha taasisi sheria au kanuni. Kwa hiyo kuna umuhimu kwa wanaofanya maamuzi katika taasisi yoyote wawe makini ili jamii isije kuona kuwa kuna tatizo alafu watu wakakata tamaa kuwapeleka watoto wao huko.
“…taasisi hazizai…”
Mungu bahati huyu jamaa kawa Padri , huyu jamaa anaweza kuwa msaada kwa Kanisa Katoliki, kwa malezi ya vijana na kwa tukio lake mwenyewe maana yeye ni Padri Kwa Neema ya Mungu tu. Taasisi zifahamu kuwa hazizai watoto bali vijana wanatoka majumbani mwao na kwenda huko katika mataasisi, kwa hiyo ili vijana waende huko ni lazima wavutiwe na jambo.
“…ndiyo maana akifa mtu, maiti inarudisha kwa nduguze…”
Unaweza kuona kuwa vijana wanakuja kufanya kazi na taasisi kisa ni mshahara, jamii inaweza ikacha kuifanya kazi fulani hapo itabidi kulazimisha vijana waiingie kazini kwa sheri tusipokuwa makini tunaweza kufikia huko,
“…tuangalie tunaishije na vijana…”
Ndugu zangu wa Kanisa Kisa chenu Mwanakwetu kimemgusa sana lakini kinatumika kuitazama Tanzania ya leo kisa mfano, sote tunaofanya kazi mbalimbali na watoto wa watu tukae nao vizuri, tutambue kuwa Hakuna Taasisi Izaayo Binadamu .
Mwanakwetu upo?
Kumbuka.
“Hakuna Taasisi Izaayo Binadamu.”
Nakutakia siku njema.
0717649257

Post a Comment