HEKIMA YA SPIKA ZA MISIKITI

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Jumamosi moja ya Disemba mwaka 2010 bibi yangu mzaa baba Edwiki Omari, Binti Mkomangi aliniagiza nimpelekee kwake binti yangu mdogo aitwaye Evon Adeladius, Binti Makwega ambaye alikuwa na umri wa miaka mitano wakati huo.

Kwa kuwa nilikuwa nakaa Mbagala Misheni (Msalabani), mchana wa jumamosi hiyo nikamchukua binti yangu kigulu na njia hadi nyumbani kwetu Mbagala Sabasaba (Mbuyuni) nyumba nambari saba. Nikafika hapo na bibi yangu huyu akazungumza na binti yangu mdogo ambaye ni kitukuu chake akampa na zawadi ikiwamo Khanga ya kuvaa.

Tukiwa ndani tunazungumza hili na lile, binti yangu akatoka nje na wenzake wakaenda kucheza. Ilipofika saa12.30 ya jioni nikasema kuwa sasa ni wakati wa kurudi kwangu. Nikatoka nje kumuangalia binti yangu yupo wapi? Nikamtafuta nje sikumuona, zunguka huku na kule hola. Pita kwa majirani sikujaliwa kumuona. Nikachanganyikiwa sana.

Nilipita kwa kila jirani sikumuona binti yangu huyu. Nilirudi kwa Binti Mkomangi nakumueleza kuwa yangu binti haonekani. Huku bibi yangu akisema kuwa hata yeye amezunguka kwa majirani kitukuu chake hakioni. Majirani na Bibi pale nyumbani wakasema nenda Masijidi SURAMIA-Msikitini wa Mbagala Sabasaba  Mwanakwetu anazaliwa anauona kwa kuwa sasa wanasali wakimaliza tu muombe imamu akutangazie katika spika kupotea kwa mwanao.

Kwa kuwa nyinyi siyo wageni mnafahamika wala usihofu. Nikatoka nyumbani hadi msikitini , nilipofika pale msikiti jirani na nyumbani ambao ni umbali kama wa nyumba 15 nikakuta Waisilamu wamemaliza kusali, bali wachache waliochelewa wakimalizia sala zao kwa lipa na hiyo ilikuwa ni Salat Magharibi.

 

Nikakaribishwa, ehe Shekhe Makwega leo umekuja Kusilimu? Karibu sana, nikajibu hapana , nina shida kidogo, nikamvuta chemba nikamueleza kupotelewa kwa binti yangu.

Imamu wa Masijidi SURAMIA akaandika katika karatasi yake jina la mtoto, jina la baba jina la ukoo, jinsia, wajihi wake na nguo alizovaa. Imamu huyu nilipotazama mwandiko wake alikuwa anaandika kwa herufi za kiarabu. Hakuandika kwa herufu za Kirumi.

Akaniambia Shekhe Makwega, hapa tayari sisi tunatangaza, lakini wewe endelea kumtafuta binti yetu alafu uwe unakuja hapa kuuliza kama ameoneka kila baada ya dakika 45.

 

“Tangazo! Tangazo Tangazo, Ndugu Waisilamu na wale wasio Waisilamu, tunatangaza kupotea mtoto Evon Adeladius, Binti Makwega wa Mbagala Sabasaba (Mbuyuni )nyumba nambari saba, ana umri wa miaka mitano, mweusi, amekata nywele, mrefu, mnene, amevaa sketi ya jinzi, blauzi nyeupe na kandambili nyekundu, kabila lake mpogolo, dini yake Mkristo . Kwa atakayemuona tunamuomba, kwa hisani yake, amlete hapa msikitini Kwa Imamu wa Masjidi Sulamia-Mbagala Sabasaba Magengeni, asante.”

 

Kisha zikawa zinachezwa Kashwida

Tangazo hilo nilisikika kila mara katika spika za msikiti huo. Mimi mimi na jamaa tukiendelea kumtafuta binti yangu Evon.

Jirani na Masijidi SURAMIA-Misikiti tuliokwenda kutoa taarifa ya kupotea mtoto, miaka 1980-1990 palikuw na mzee mmoja ambaye alikuwa Fundi Mshonaji wa Nguo nayeye ndiye aliyetoa eneo la sehemu ya kiwanja chake ukajengwa msikiti huo. Huyu mzee nilimfahamu kwa kuwa ndiye aliyekuwa Fundi Mshonaji wa Nguo pekee miaka mingi ya utoto wetu. Nakumbuka hata nguo zangu za kupokelea Komuniyo ya Kwanza alinishonea yeye mwaka 1988.

Ninachokumbuka miaka ya 1990 mzee huyu alifariki na nilishiriki kumzika. Baada ya kufariki familia yake iliheshimu maamuzi ya baba yao na wakatenga eneo la msikiti na eneo la nyumba yao kwa mipaka, huku Waisilamu wa eneo letu wakiuboresha kidogo japokuwa eneo lao ni finyu likiunganika na nyumba ya marehemu Fundi Mshonaji wa nguo zangu za Komuniyo ya kwanza.

 Hiyo ni Mbagala ya mwaka 1986 na Mwanakwetu yumo mtafute.

Kumbuka msomaji wangu mtoto amepotea, sasa hiyo inakwenda saa mbili usiku, bibi akaniambia kuwa mtoto akipotea unakwenda kutoa taarifa polisi. Kwa hiyo mimi nikaanza safari hadi polisi Maturubai Mbagala Kizuiani, wakati huo boda boda ndiyo zinaanza, mimi nilitembea kwa miguu hadi huko.

Nilipokuwa nakaribia Polisi Kizuiani, kwa mbali nikamuona mama mmoja amemshika mtoto akiogoza polisi, nilimpotazama vizuri, nikasema yule ni binti yangu.

Nikaita Evon ? Akajibu baba mimi hapa. Nikamkimbilia, Nikamsalimu yule mama na kumwambia huyu ni mwanangu. Mama huyu akaniambia’

 

“Baba huyu mtoto nimemuona anacheza na wanangu hadi saa moja jioni nikashangaa mara anaaza kulia, anamlilia baba yake, namuuliza kwao wapi ananiambia kuwa kwao kuna Kanga, kuku na bata wengi, nikimuuliza eneo, halitaji vizuri, kwanza nilimpeleka Masjidi Salama-Msikiti wa Mbagala Kizuiani wametangaza. Imamu akaniambia sasa nimlete kwenye serikali, ndiyo ninakwenda polisi.”

 

Hapo mama huyu anaongea huku kamshika binti yangu mkono, tupo nje ya kituo cha Polisi Maturubai. Mama huyu akasema kwa kuwa dunia imeharibika, mtoto huyu nitakukabidhi mbele ya serikali twende kwa polisi wa zamu nitajitambulisha na wewe ujitambulisha ndipo serikali ikukabidhi. Hilo likafanyika vizuri polisi wakalisimamia zoezi hilo. Polisi mwanamke akamkagua binti yangu vizuri wakiwa pembeni alafu akasema hajafanyiwa baya lolote.

shangazi wa Mwanakwetu 1986
 

Nikasema asante mama, nikakabidhiwa , tukawaaga polisi tukaanza kurudi ili nipafahamu kwake mama huyu, nilipofika kwake jirani na shule ya Msingi Mbagala niliwasalimu wapangaji wenzake alafu nakumuaga mama huyu mwenye asili ya Masasi Kusini mwa Tanzania.

 

“Unataka kumpoteza binti yako mrembo kiwepesi wepesi, baba utakosa mahari.”

 

Wapangaji wenzake na mama huyu wakawa wananitania, mama huyu akaniambia kuwa yeye sasa anakwenda kumueleza imamu wa Masjidi Salama kuwa baba wa mtoto kapatikana sisi tukaondoka zetu kurudi Mbagala Sabasaba. Tukapitia Masijdi Suramia kuwaeleza binti amepatikana na kurudi nyumbani kwetu.

Tulipofika nyumbani Kwa Binti Omari nilimuuliza binti yangu ulifikaje Mbagala Kizuiani kutokea Mbagala Sabasaba?

Binti yangu huyu ambaye sasa ni mwanafunzi wa kidato cha sita aliniambia kuwa

 

“Nilimuona baba yangu mdogo anayeitwa Mkomangi Mkundi akielekea huko, kwa hiyo nikawa na,fuata nyuma nyuma , bila ya baba mdogo kufahamu. Kwa kuwa njia za Mbagala Kizuiani jirani na Shule ya Msingi Mbagala kuna kona na vichochoro vingi, baba yake akanipotea ndiyo nikafika sehemu nikawakuta watoto wadogo wanajipikilisha nikaungana naoa kuchezaa mchezo wa kupika pika.”

 

Binti Makwega aliendelea kusimulia,

 

“Nikakutana na watoto wanajipikilisha (wanacheza mchezo wa kupikapika) barazani kwao nikakaa na mimi kupika nao hadi usiku unaingia, lakini baba usinichape.”

 

Eneo la Mbagala Sabasaba kwa asili ni eneo lililokuwa sehemu ya Kijiji cha Ujamaa cha Mbagala, eneo la watu fukara sana. Wakati huo kulikuwa na tajiri mmoja mwenye mabasi mengi anaitwa Kitotola. Hata ujenzi wa mbaoreshi ya Masjidi SURAMIA ulionifanyia hisani ya kutangaza tangazo la kupotea binti yangu ulikuwa wa kuchangishana wenyewe kwa wenyewe, nyumba kwa nyumba nakumbuka kwa awali hawakuwa na muhisani. Huku hata huyu tajiri Kitotola alikuwa na tajiri mwenye makazi mengi huko Kimanzichana na Mbagala.

Evona, Albarty, Joshuam Joseph na Wimfrida Makwega 2021.
 Watoto wa Mwanakwetu.

Nikamuuliza bibi yangu mzaa baba Hedwiki Binti Omari, akasema wakati msikiti huu unajengwa hapa nyumbani kwetu tulichangia? Bibi alinijibu kuwa alichangia shilingi 500/- alimpa mzee mwenyewe aliyetoa eneo, Fundi Mshonaji .

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Msomaji wangu nakuomba kwanza tilia maanani majina ya misikiti ya zamani ya Mbagala ambaye ndiyo misikiti ya awali ya Mbagala; MASJID SURAMIA MBAGALA SABASABA na MASJIDI SALAMA MBAGALA KIZUIANI.

Msomaji wangu nakuomba utilie maanani juu ya hekima ya spika za misikiti na hasa vyombo vya habari vinatoa haki kwa wote bila kubagua? Wiwe vya vyama vya siasa, viwe vya taasisi binafsi, viwe ya dini yoyote ile au vya serikali je mnalo la kuliokota katika hekima ya spika za misikiti ya kwetu? Mulitafakri hili kwa kina. Mnachoweza kufanya mnatoa nafasi wale wa upande mwingine kusema ya kwao bila ugomvi bila fujo. Iwe katika gazeti, redio, runinga, blogi na hata mitandao ya kijamii?

Kumbuka wanaosikiliza, kutazama na kusoma wanatoka pande zote, japokuwa chombo hicho ni mali ya upande fulani. Kwa hiyo hekima ya spika za misikiti zenyewe zinarusha hoja ya mtoto kupotea, aliyemuokota, asiyemukota wote wanasikia, yaani yule linalomuhusi analichukua na yule lisilo muhusu analiacha. Katika mambo kenda hata kama si ya dini yako lipo moja, mawili au matatu yenye manufaa kwa binadamu wote usibague.

Huyu binti yangu kaingia kazini kambagua Muisilamu, kashindwa kumpa huduma kwa Uisilamu wake, Mungu atamuadhibu kwa maana Msiikiti Mikongwe ya Mbagala Masjibi SURAMIA na Masjidi SALAMA ilipaza sauti siku alipopotea.

Makala yanatayarishwa na Mwanakwetu kwa nia kuhifadhi kumbukumbu lakini pia nia ya kilabinadamu kutenda wema bila kujali tofauti tulizo nazo.


 Mwanakwetu na Bintiye Evona.

 Mwanakwetu Upo?’

Kumbuka

“HEKIMA YA SPIKA ZA MISIKITI.”

 

Nakutakia siku njema.

makwadeladius @gmail,com

0717649257 


 

Hapo Mwanakwetu ameketi na rafiki zake Mbagala jirani na Masjidi SURAMIA 2012.

Mama wa Mwanakwetu (Gauni nyeupe), Binti Omari aliyevaa Kitenge na Mwanakwetu na wadogo zake Modestus Maiko na Samweli 1985 Mbagala Sabasaba.
Baba wa Mwanakwetu na Namsi Peter Mtu na mjombae hapo


 

 Mwashabani Mchafu miongoni mwa Waislamu wanaosali Masjidi SURAMIA

 

0/Post a Comment/Comments