Adeladius Makwega-MBAGALA
“Allahu akbar, Allahu akbar, Allahu akbar, Allahu akbar, Allahu akbar, Allahu akbar.”
Hiyo ilikuwa ni sauti ya muazini akinadi sala saa 1.23 ya asubuhi ya siku ya Mei 3, 2022 katika Msikiti wa Chamwino Kijiji cha Chamwino Ikulu, mkoani Dodoma.
Azana ya namna hiyo na muda iliyonadiwa ni nadra sana kuisikia kwa kuwa saa 1.23 asubuhi si muda wa sala tano za Waisilamu, lakini baadaye nilikumbuka kuwa ni sikukuu ya Idd al Fitr baada ya Waisilamu kumaliza Mfungo wa Ramadhani.
Nikasema muazini ananadi ili kuwajulishwa Waisilamu wajongee kusali salat Idd. Nilikumbuka nikasema hata kwetu Mbagala miaka ya nyuma hiyo azana nilikuwa kutoka MASKIDI SURAMIA Mbagala Sabasaba na MASJIDI SALAMA Mbagala Kizuiani ninaisikia kipindi cha sikukuu kama hiyo.
Nikaiwasha simu yangu ya mkononi na kukutana na ujumbe wa mkono wa idd kutoka kwa watu watatu,
“Wa kwanza ni Abdu-latif Said Matibwa- huyu ni Mtangazaji na Mtayarishaji wa Vipindi vya TBC wa miaka mingi, yeye ni Mgindo wa Morogoro. Ujumbe wa pili ulitoka kwa kaka yangu mwenyewe Abdi Rashid Mohammed, yeye tulisoma naye Tambaza, sasa ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ujumbe wa tatu ulitoka kwa Pascal Mlelema kwa mujibu wa nambari yake ya simu akinipa mkono wa idd na ndugu yangu wa mwisho kunitakia heri na neema ya sikukuu hiyo alikuwa na mama yangu Husna Kombo.”
Kwa hesabu ya namba ndugu zangu karibu wote hao ni wa Dar es Salaam ningekuwa huko iwe pilau iwe biriani ingelika tu.
NIkasema Dodoma,
Sina majirani au hakuna waliofunga Ramadhani?Jibu lake wapo tele shida ni moja tu. Pasaka na Iddi hazijkupishana sana mwaka wa 2022 lakini binafsi sikuwa na deni la kutowaalika majirani zangu, maana nina majirani zangu Waisilamu ninaowafahamu wawili na wakati wa Pasaka wote hawakuwepo Dodoma wakati huo.
Jirani yangu wa kwanza ilikuwa ni familia ya baba mmoja na mama mmoja Mrangi wa Kondoa, mwanzoni mwa mwaka 2022 walipata changamoto za ndoa na kila mmoja akachukua njia yake.
Binafsi sikulijua hilo, hadi najulishwa imepita miezi mitatu baada ya kusikia kuwa kuna nyumba inauzwa, kulikoni? Nikaambiwa ndoa hii imeingia ruba na wanagawana mali, mteja wa nyumba hii alipatikana na mgao kufanyika.
Ndugu hawa niliwazoea sana maana kabla ya kuweka umeme wa makabwela wa shilingi 27,000/- nyumba yao ilikuwa kimbilio ya kununua vitu baridi lakini pia kwa kuchajia simu na isitoshe walikuwa wanatoa huduma hiyo bure bila malipo yoyote yale. Binafsi bado ninawaombea dua kama wakirudiana basi litakuwa jambo jema.
Jirani yangu wa pili yeye nilidhani atakuwepo maana niliona nyumba yake inaboreshwa mno, maua yakipandwa kuzunguka ukuta wa nyumba yake na mbele ya nyumba yake pia wamewekwa twiga wa saruji, nikasema jirani atakuwepo wakati wa iddi na Iddi itafana mno. Jirani yangu huyu anazo nyumba nyingi kila mkoa lakini Dodoma ndiyo nyumba kubwa. Pasaka nilitaka kumualika lakini nikajiuliza maswali lukuki ataweza kuja kula pilau kwangu? Maana wanaweza kuja kukagua wakasema kuwa jirani yako kwake hakuliki. Lakini nikajipa moyo nakusema kuwa hata wakisema hivyo kwani jirani nayeye si kazaliwa huku huku. Wakati wa pasaka nikachunguza sikumuona jirani, mwaliko wangu ukabaki moyoni.”
Kiimani nina hakika jirani zangu wote wawili wamekula pilau yangu ya Pasaka.
Sasa iddi ikafika,vipi jirani yangu wa pili yupo? Jirani yangu huyu majukumu yake ni mengi mara yuko ughaibuni, mara kule, akiwajibika Mwanakwetu. Niseme ukweli nilikuwa ninahusudu mno mwaliko wa jirani yangu huyu, biriani na pilau ya Kizanzibar za iddi zinakuwaje? Maana mdomo wangu bado mgeni wa biriani na pilau za Kizanzibari.
Mwanakwetu nimefulia naambiwa jirani baada ya Salat Idd kaenda kuendelea na kazi. iddi al fitr imepita mwaliko sijapata. Nimejiuliza sana ati mwaliko wa jirani yangu nikale biriani ya Kizanzibari na kazi anazofanya ipi bora? Nikajijibu mwenyewe kama kazi hizo kwa ustawi binadamu, jirani endelea na kazi.
Hongereni sana mliopata mialiko ya majirani zenu sikukuu ya Idd ya mwka 2022, mie niliambulia patupu na kujipa kazi niliamua nivune mahindi katika shamba langu, sasa nimeyarundika yanapigwa na jua, huku mwili wangu mzima nikiwashwa kwa upupu wa mahindi.
Kwa hakika mwaka huu nipo mbali na Chwamiwno Ikulu na kwetu Mbagala. Kule Chamwino Ikulu nimeambiwa yule jirani yangu aliyeachana na mkewe kaoa mke mwingine ndiyo kusema kama ningekuwepo Chamwino ningealikwa na jirani yangu huyu.
NIngekuwa kuwa kwetu Mbagala Waisilamua wa Masjidi SURAMIA na Masjidi Salama wangenialika tu.
Ngoja nioone kwa Waislamu huko nilipo je watanialika au nitakula wa chuya nitabaki nikimsikiliza ndugu yangu wa Morogoro Salimu Abdalah ana wimbo wake wa mkono wa Idd?
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Jirani Zangu Wawili."
0717649257
Post a Comment