KICHUNGU HUONJWA

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Mara nyingi nilikuwa mvivu wa kula chakula kwa akina pangu pakavu tia mchuzi kutokana na namna mapishi yake yalivyokuwa yanapikwa, kidogo ilikuwa sijayazoea. Si kwamba mapishi haya yalikuwa mabaya la hasha, bali mapishi mengi yalikuwa katika namna nisiyozoea.

Mapema mwaka ya 2022 ulianza kwa neema kwa siha yangu kwani walikuja wapikaji wapya, nilijulishwa kuwa wanatokea huko Zanzibar bila ya kufahamu kama walikuwa Wagunya, Washirazi, Watumbatu iwe Unguja au Pemba wewe msomaji wangu elewa tu wanatokea Zanzibar.

Wenzangu waliniambia kuwa ndugu hawa wanapika vizuri sana, akilini kwa Mwanakwetu na nduguze wa Mbagala wanasema Kichungu huonjwa. Hii ni hekima ya siye wa Mbagala katika kuonja huko na kitamu hujulikana pia.

Kwa hiyo nilisogelea genge(Mkahawa) la Kizanzibari na kuanza kula. Mapishi haya yalikuwa matamu mno, Mwanakwetu nilijinoma mno. Chakula chao kilikuwa na kipimo kikubwa na huku wakiweka Nyama, Maharage, Dagaa na Kisamvu.

 


Kisamvu hichi kiliungwa vizuri huku wakikiwekea pilipili kwa mbali, maziwa , nazi, mafuta, karanga, ufuta na iriki. Mama huyu wa Kizanzibari alivyokuwa muungwana akasema maneno haya,

 

“Baba usihangaike kuja, tutakuwa tunakuletea chakula hiki pahala ulipo, jukumu lako wewe ni kutuambia mapema wala nini tu.”

Msomaji wangu ushakula mapishi ya Kizanzibari? Dada zake zake hawa Shamsi Vuai Nahodha kutoka kule KIJITOUPELE kule ZANZIBAR wanajua mno kupika, Mabinti wa Zanzibar ni Hodari Sana 


 

Kwa desturi Mwanakwetu Mpogolo mvivu sana kula, lakini siku hii alikula wali wote na kuvutiwa mno na mapishi yao ya KISAMVU na kuuliza wanakipikaje?

Mama huyu akacheka akisema mbona baba una maswali mengi? Kama umependa mapishi oa akina mama kutoka Zanzibara! Siku hii waliombatana na Mwanakwetu wakacheka sana wakimwambia mama huyu kuwa Mwanakwetu ni Mwandishi wa Habari, wewe mjibu tu maswali yake, usipojibu maswali yake ana nogwa mno.

Mama huyu kuepusha nongwa za Mwanakwetu akasema,

 

“Tunakichemsha, kikiiva tunakitia nazi, kinawekwa maziwa, kinawekwa karanga,mafuta, kinawekwa ufuta na kinawekwa viungo vingine kama chumvi, vitunguu maji iriki na vitunguu swaumu kwa kiasi.”

 

Wakati ninaambiwa haya, moyoni nilisema kuwa haya kweli mapishi ya Kizanzibari na yalikuwa yamekamilika kweli kweli. Nikasema Wazanzibari kidogo wanaweza kupika na kumkaribia Binti Mkomangi (bibi yangu mzaa baba). Kila siku niliendelea kula chakula hiki huku nikiogopa kulishwa LIMBWATA LA KIZANZIBARI maana Binti Mkomangi aliniambia kuwa ukiwa mwanaume usipende kula sana vyakula vya wanawake mbalimbali, vingine huwa haviliki, vingine ukila vina mabalaa, vingine ukionja tu hauwezi kuviacha milele.

 

“Usipende kula vyakula vya wanawake mbalimbali, vingine huwa haviliki, vingine vina mabalaa , vingine ukionja tu, hauwezi kuviacha milele.”

 

Niliyakumbuka maneno hayo ya Binti Mkomangi mara mbili mbili, kwangu binafsi kwani mwaka 2004 wakati nakwenda Isimani-Iringa kuanza kazi bibi yangu aliniambia kuwa Wahehe, Wakinga na Wabena wana LIMBWATA lao linalofahamika kama LITAMBULILA kwa hiyo niwe makini sana.


 

Nikiwa Iringa akina Segito, Semuyala, Semdeke, Sechaula, Semlelwa walinipikia vyakula lakini sikuweza kuvionja kuogopa LITAMBULILA, lakini sasa mapishi ya Kizanzibariyako mezani, yapo ubaoni yamenivutia mno nikawa nakula nikinuia kula kila siku tangu Januari hadi Disemba, nikiwa naliogopa LIMBWATA la Zanzibari huku sifahamu linaitwaje?Tambua kuwa Mwanakwetu yu MJI WA SERIKALI JIJINI DODOMA nah ii ni mwaka wa 2022.

Siku ya Jumatano ya Majivu ya mwaka huu ilifika , nilifika kwa akina pangu pakavu tia mchuzi, nikatulia tuli na ilipofika saa sita juu ya alama dada wa Kizanzibari alikuja na chakula chake kuniletea, akisema mbona baba haukupiga simu? Nimeamua nikuletee tu. Nilimjulisha kuwa leo kidogo nina dharura. 


 

Binti huyu alijisikia vibaya mno, akitambua kuwa sasa amempoteza mteja wake, nilimwambia kuwa usiwe na shaka, mimi bado ni mteja wako lakini leo nina jambo langu.Binti huyu hapa alikuja na kikapu chake kikubwa kilichojaa mikebe ya plastiki yenye vyakula, alikaa katika kiti na kuanza kutoa machozi.Binafsi ni muda mrefu kumuona mtu analia jirani yangu, hata mimi hulia sana lakini si hadharani, nikiwa na jambo langu, huingia chemba na kutoa machozi yangu kwa siri, nikitoka nje nanawa uso wangu na kuendelea na maisha kama kawaida, alipoanza kulia nilijiwa na shaka mno, hapa inakuwaje? Akija mtu akimuona binti huyu analia si nitaonekana nimemdhulumu kitu, lakini nikasema namuachia Mungu jambo hilo, alilia kwa dakika kama tatu hivi, nilimpa maji akanawa, nikamuuliza kulikoni? Binti akajibu;

 

“Ninapokuwa na jambo moyoni mwangu linaniumiza huwa ninalia, nikimaliza kulia jambo hilo huwa limetoka moyoni.”

 

Msomaji wangu tambua kuwa hapa kwa akina pangu pakavu tia mchuzi ni MJI WA SERIKALI Jijini Dodoma wakati huo ujenzi wa majengo ya wizara unaendelea.Hapo hapo likanijia swali hili mbona kando ya mikahawa yenu kuna makambi mengi ya ujenzi huko hakuna wateja? Binti huyu alisikitika tu akasema,

 

“Kaka kwenye makambi haya hakuna wateja na wala hakuna watu. Mwanzoni tulitarajia kuwa kuanza kwa ujenzi huu makambi haya yangeongeza wateja lakini sasa hakuna.”

 

Binti huyu huku hasira yake ikiwa inapoa ya kupoteza wateja nilimchokoza nikamwambia sasa si ukawashitakie kwa Mama Samia kuwa makambi hayana watu ili wakija upata wateja. Binti huyu alicheka sana, akasema we waache tu, nitafanya hivyo, umenipa hekima kubwa. Binti huyu aliondoka na kikapu chake cha chakula kurudi mkahawani.Mwanakwetu tangu siku hiyo binti huyu wa Kizanzibari nilipompa hekima ya kuwashitakia kwa rais Samia sikumuona tena ndani ya MIKAHAWA YA MJI WA SERIKALI.Swali ni je alikwenda kushitaki kwa Mama Samia Suluhu Hassan? Mie sikufahamu.

 Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Kikubwa katika makala haya ni kilio cha binti wa Kizanzibari kwa kukosa kuuza chakula chake siku ya Jumatano ya Majivu kipindi hiki kilikuwa nyakati za mwanzoni mwanzoni mwa mwaka wa 2022 ambapo kidogo ujenzi wa majengo ya Mji wa Serikali yalizorota hivyo wateja wa mikahawa walipungua na ngongo ngoo zilipungua, hivyo hata mikahawa mingi ikafungwa hii ya Mama Ntilie, wateja wa maofisini wenyerwe walikuwa wanakula mikahawa yenye hadhi yao, mama ntilie wakakosa wateja na wengi kufunga biashara akiwamo huyu mama kutoka Zanzibar.

Ninachoweza kusema siku ya leo ni hiki miradi mikubwa ya serikali inapofanyika vizuri ukitaka kupima kwa jicho la haraka ni ujenzi wa vibanda vya mama ntilie nje ya mradi huo na nyakati za chai na chakula cha mchana vibanda hivi vina wateja wengi, jambo la pili la maradi kuwa ujenzi unaendelea na ukumbwa wa milio ya ujenzi, pale unapoona kimya au milio imepungua jua tambua hiyo mradi ina shida.Haya msomaji wangu ndiyo mambo makubwa mawili ya jicho la haraka harka katika miradi yoyote mikubwa inayofanyika kinyume chake huo mradi una shida.

 


Ndiyo maana tnabaini kuwa binti huyu wa Kizanzibari alilia, akikumbuka mtaji wake utakata, kodi ya nyumba Dodoma na mengine mengi, kilio kama cha huyu binti wa Kizanzibari viko vingi, je nani wakuwafuta machozi?Kwa hakika tukio hili la kweli kabisa, natambua wapo walio hai leo hii, tuliokuwa nao, tangu tunakwenda kula chakula siku ya kwanza hadi siku ya Jumatano ya Majivu binti wa Kizanzibari analia Ofisini kwetu Wizara ya Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo, hata yule mmoja aliyefariki katika kisa hiki atakuwa shahidi wangu mbele ya Mungu.

 


Mwanakwetu upo ?

Je makala haya niyahitaji? Limbwata la Kizanzibari?, Mikahawa ya Mji wa Serikali? Mwisho wa Mapishi ya Zanzibar, Ishara ya Miradi Mikubwa Inayofanya kazi Au Kichungu Huonjwa?

Mwanakwetu anachagua Kichungu Huonjwa.

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com
0717649257 



 




 


0/Post a Comment/Comments