Adeladius Makwega-MBAGALA
Unaposafiiri kwa basi kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine nchini Tanzania kumekuwa desturi ya mambo mbalimbali ambayo kwa hakika unaweza kujifunza iwe kutoka kwa abiria wenzako, makondakta, madereva na hata jamii kando ya vituo vya mabasi.
Ndani ya mabasi mengi yana redio na runinga zinazocheza santuri na flashi zenye nyimbo, filamu za kazi zingine za sanaa. Muda mwingine wanacheza miziki iliyounganishwa mwanzo hadi mwisho. Kwa utafiti wangu mdogo mtu akiwa katika basi anakuwa na wakati mzuri mno wa kusikiliza muziki kuliko wakati mwingine wowote ule.
Maana hatarajii kushuka ndani ya chombo hicho muda huo bali baada ya muda mrefu, kwa hiyo mawazo yake yote huwa yametulia kufikiria muziki huo unaosikika katika chombo hicho cha usafiri, mawazo yatahama tu akishuka chomboni.
Kwanini ninayasema maneno haya?
Majuma kama mawili yaliyopita nilisafiri kutoka Lushoto kwenda Dodoma, niliingia katika basi moja linalofanya safari zake huko. Kwanza safari ilianza kwa ukimya mno, lakini walipojaza abiria katika siti zote pale Korogwe dereva wetu alituwekea nyimbo mbambali za lugha ya Kiswahili.
Zilichezwa nyimbo nyingi lakini hadi nashuka nyimbo ya Ndoa Ndoano na Penzi na Mlemavu zilichezwa mara mbili, basi hilo likiwa katika maeneo tofauti. Awali tukiwa kati ya Segera na Chalinze na mwisho tukiwa kati ya Chalinze Nyama na Dodoma Mjini .
Nilichobaini nyimbo hizo mbili ni za Msondo Ngoma Music Band nakumbuka walicheza nyimbo nyingi za wanamuziki wengi vijana wa sasa na wanamuziki wa zamani akiwamo Mwinjuma Muumini.
Nyimbo hizo mbili ni ndefu sana, Ndoa Ndoano(9.40’). Nikasema moyoni kwamba kwa dakika hizo hakuna redio au runinga inaweza kucheza nyimbo hizo kutoka mwanzo hadi mwisho. Redio na runinga za Tanzania zitacheza sana sana dakika tatu na vyombo vya kimataifa wakicheza sana labda sekunde 50 tu.
Nikajiuliza hivi wanamuziki walio hai wa Tanzania wanatambua kazi kubwa inayofanywa na makondakta na madereva wa mabasi kukuza muziki na sanaa yetu?
Wimbo huo unachezwa hadi unamaliziki, anasikiliza kijana, mtu makamo na mzee. Kijana anajifunza awe makini akiwa na ndoa, mtu mzima anatafakari pale alipo na mzee anajikumbusha mambo yalivyokuwa magumu . Tofakari ya namna hiyo haipo katika redio, runinga walachombo chochote cha mawasiliano bali mabasi.
Safari ya Lushoto hadi Dodoma katika basi moja abiria zaidi ya 100 watapanda na kushuka hadi basi linafika kituo cha mwisho, hiyo ni kwa safari ya siku moja tu. Chukua hesabu ya siku 365, hapo abiria 36,500 watakuwa wameusikiliza wimbo wa ndoa ndoano/Penzi na Mlemavu.
Tukadirie tu Tanzania yetu katika barabara zetu tuna mabasi yanayofanya safari zake yapo 10,000 ukizidisha na abiria 36,500 utabaini kuwa abiria 365,000,000. Hao ni abiria wanaojirudia kila mara wakiwamo wafanyabiashara.
Msomaji wangu usiwe na shaka na idadi ya watu milioni 70 wa Tanzania, watu Milioni 365 ni wale wanaofanya safari kwa mwaka tuseme kila Mtanzania amesafiri mara 5.
Ukizifuatilia hizo nyimbo mbili zote wanamuziki wake wengi walioshiriki kutunga na kuimba wamefariki dunia lakini bado zinachezwa mno katika mabasi kuliko nyimbo za vijana wa sasa.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Nionavyo mimi wanamuziki na wasanii wengi wa sasa wanapaswa kwanza kwa sasa kutunga kazi zenye maudhui yasiyokwisha.
Pili wanapaswa kuwekeza kwa makampuni ya mabasi ili makondakta na madereva hao wacheze kazi zao kuliko kuwekeza mno katika redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.
Kwa kufanya hivyo kazi zao za Sanaa zitaenea na kufahamika mno.
Wasalaam ndugu yenu mpendwa.
0717649257
Post a Comment