Adeladius Makwega-MBAGALA
Kwa hakika habari kubwa ambayo ilikoza wino katika vyombo vingi vya habari kuufunga mwaka wa 2021 nchini Tanzania ni suala la ukopaji kwa taifa letu, huku kukiwa na pande kubwa kubwa mbili, wengine wakisema tukope na wengine wakisema kuwa mikopo ina madhara.
Mjadala ulikuwa dhaifu kwani ulihamia kumtuhumu mtu binafsi na hata kushambuliana mambo binafsi ambao sioni kama kulikuwa na tija ya kufika huko.Kwa ukweli wa Mungu kama yangekuwepo masanduku ya kupigia kura, jambo hilo lilikuwa na masanduku mawili kukopa kuzuri au kukopa ni hatari.
Katika maendeleo ya taasisi yoyote jambo lenye majibu mawili huwa ni zuri, kwa kuwa upande wowote utakaamuliwa kufuatwa, baada ya miaka kadhaa majibu yatapatikana yanaweza kuwa si mnaona mikopo ilivyotusaidia au unaweza kusikia si tuliwaambia, sasa mmekwama.
Binafsi, mapema mwaka 2021 nilitembelea Benki ya NMB makao mkuu Dar es Salaam ambapo nilikuwa na jambo langu huko, nilifika hapo angalau kukubaliana juu ya namna nzuri ya makato yangu ambayo yalikuwa hayaeleweki. Kweli nilifika hapo nilipokelewa mapokezi ya ofisi hizo zilizo jirani na Mtaa Ohio. Niliwasiliana kwa simu na mhusika anayeshughulikia mikopo, suala hilo halikwisha na sikuweza kumuona mhusika huyo.
Baadaye nilipewa nambari ya simu na kuendelea kuwasiliana naye kwa simu. Ilikuwa ngumu kuzungumza naye vizuri, japokuwa nilikaa hapo kwa zaidi saa 3 sikuweza kuonana naye kwa hoja ya Korona. Nilishangazwa na tabia hiyo, kwani taasisi hii ya fedha hawakuwa wakarimu tena kama walivyokuwa mara ya kwanza wakati wakinishawishi kuchukua mkopo huo.
Hadi saa saba mchana sikuweza kutatuliwa shida yangu, zaidi ya kupewa namba na kuambiwa kuwa tunaendelea kulifanyia kazi jambo hilo. Mawasiliano yaliendelea lakini mwisho wa siku nilijifunza jambo moja kubwa sana maishani mwangu.
Nilitoka hapo hadi Barabara ya Titi Mohammed, kabla sijavuka niwe upande wa Maktaba ya Taifa nilishangaa gari moja ilisimama mbele yangu, jamaa alifunga breki miguuni mwangu, nilishituka kidogo, alinisalimia na kuniuliza Makwega unatokea wapi?
Nilimsimulia nilipotoka, huyu alikuwa jamaa yangu ambaye nilisoma naye siku nyingi. Hivi sasa akihudumu katika taasisi moja kubwa ya dini, alinipakiza katika gari hilo kwa kuwa kwetu anakufahamu, aliniuliza si unakwenda Mbagala, nilimjibu ndiyo. Tulianza safari ya kuitafuta Mbagala, nikiwa ndani ya gari hilo tuliongea mengi. Nilipomsimulia nilipotoka na kilichonikuta ndugu huyu alinijibu tu.
“Kila jambo lina Arubaini yake, mimi(yeye) nimekabidhiwa taasisi moja ambaye ina madeni hapa nilipo natoka kuelezea namna ninakavyolipa madeni hayo ambayo yalikopwa na mtangulizi wangu.”
Sasa kibaya, hata hiyo miradi inayodaiwa kukopewa haijafanya vizuri, kwa hiyo sasa anajukumu la kulipa huku akitakiwa taasisi hiyo kuweza kusonga mbele na mipango mipya ya maendeleo.
Aliniambia kuwa madeni ambayo yalikopewa yalikuwa kwa miradi ya kujiendesha kibiashara, wakati hivi sasa pesa inayokusanywa kwa miradi hiyo haifiki hata robo ya rejesho hilo kwa mwaka, kwa hiyo walichofanya walitazama vyanzo vingine vikiwamo misitu, mashimo ya madini, akiba yao ya dhamana ya benki vitumike kulipa madeni hayo ili taasisi iwe salama.
Huku akiniambia kuwa katika hilo wanaweza wakapata 75 ya asilimia ya rejesho angalau kukwepa migogoro ya mashauri kupelekwa katika mahakamani na kufilisiwa, lakini pia kudaiwa huko kunafanya kuzungumzwa vibaya na taasisi za fedha, jambo ambalo linawafanya washindwe kuaminiwa tena.
Basi, tuliendelea na safari, tulipofika Mbagala 77 nilishuka na ndugu huyu kuendelea na safari yake kwenda huko Kusini mwa Tanzania.
Ndugu yangu huyu sikuwasiliana naye kwa muda kama wa miezi 6 hivi lakini ilipofika Agosti 3, 2021 nilimuona wakati wa kuuwaga mwili wa Padri Raymond Saba aliyefariki dunia ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Tulipokutana na ndugu yangu huyu tuliongea kwa uchache huku akiniuliza naendeleaje? Nikamwambia naendelea vizuri.
Katika msiba ule mahubiri yalihubiliwa na Padri Charles Kitima ambaye ni Katibu Mkuu wa TEC wa sasa. TEC walizungumzia namna marehemu Padri Saba alivyoisaidia sana taasisi hiyo akiwa Katibu Mkuu.
“Moja, aliweka mfumo wa mpya wa Sekretarieti namna inavyoweza kujiendesha kwa njia ya Kurugenzi. Baraza lazima liendane kama jamii ya kidunia inavyoenda hasa taasisi kubwa na sisi tunaendelea kutekeleza majukumu yetu huku tukifuata huo mfumo wa Kurugenzi, ameuanzisha yeye, alithamini sana kuwatumia wataalamu, wataalamu ndiyo walioweza kufanya kazi na hatimaye maaskofu wakaupitisha huo mfumo. Hii ni kazi ya kichwa ambayo Baba Sada aliifanya, hili tutamkumbuka daima.”
Mahuburi ya Ibada hiyo ya kuuga mwili wa Padri Raymond Saba yaliendelea kutolewa na Padri Kitima.
“La pili Padri Saba alihakikisha baraza linamaliza madeni yote yalikuwa yanadaiwa huku na kule. Nimefika ofisini sikukuta baraza na deni hata la senti tano. Nimekuta amelipa kila kitu, nimefika Julai 10, 2018 vitabu vyote viko vizuri, mahusiano ya kifedha na taasisi za serikali yako vizuri sana. Padri Saba alisafisha mapungufu yetu yote na wahisani wetu wote dunia nzima, mapungufu yaliyokuwepo mpaka tunanyima misaada, alijitosa mtoto wa watu. Padri wetu mpendwa alihakikisha anaweka ripoti zetu vizuri, kuhakikisha anajitoa sadaka, aliweka mahusiano vizuri. Sisi tulipofika, tunapiga hodi tunaambiwa ahaa TEC imejisafisha karibuni sana.”
Hiyo ni kazi ya mpendwa wetu Padri Saba akiwa hai.
“Hivyo, hata mahusiano yetu mazuri kwa sasa yanafanya baraza hata katika nyakati hizi ngumu za kiuchumi kutokana na ugonjwa kwa Korona, baraza linaenda. Marehemu hakujua kuwa Korona itakuja kuwa tatizo la uchumi la baraza, lakini kutokana na alivyofanya labda Mungu alimtuma afanye na sasa hivi baraza linaendelea vizuri, kutokana na mahusiano mazuri na wafadhili wetu wa Kikanisa na taasisi zingine.”
Aliendelea kuhubiri Padri Kitima.Ibada hii ilipomaliza nilidoea tena usafiri wa ndugu yangu huyu nayeye kurudi Kusini na mie kushuka zangu Mbagala 77
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?.
Ukiwa umevisoma vizuri visa vyangu vitatu vizuri , kile cha NMB na mimi mwenyewe, cha huyu ndugu yangu wa Kusini mwa Tanzania na hata hiki cha TEC cha Marehemu Padri Raymond Saba kama kilivyosimuliwa na Padri Charles Kitima inatoa taswira ya taasisi za kifedha zilivyo na pale panapotokea kushindwa kulipa madeni hali inavyokuwa.
Swali ni Je Tanzania itaweza kufanikiwa kwa kukopa? Au tulipashwa kutazama vyanzo vingine? Je mwezangu unayesoma matini haya unayo majibu? Mie sina majibu, zaidi ya kuzingoja hizo arubaini, panapo majaliwa yake Mola.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Nazingoja Arubaini.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment