Adeladius Makwega-MBAGALA.
Siku ya leo msomaji wangu nakuomba nikupitishe katika visa kadhaa vya kweli kabisa, kimoja baada ya kingine katika maisha ya Mwanakwetu kisha tuvioanishe visa hivyo na Tanzania yetu ya leo.
Kisa cha Mwanzo;
Mwanakwetu alipokuwa anasoma Shule ya Msingi Mnazi Mmoja alikuwa hapendi kuongozana na Mama yake kila anapokwenda kazini na hata wakati anaporudi. Mwanakwetu alipokua mdogo hakuona kuambatana na mama yake ni shida lakini umri ulivyokuwa unasonga alibaini jambo hilo lilikuwa na kasoro,
Je ilikuwa nini?
“Desturi ya wanaume ni kiumbe anayewinda mara zote, hivyo anapopita mwanamke mzuri ,yupo mwanaume anayesifia moyoni, yupo anayesifia kwa kusema na yupo mwingine ule urembo hataki umpite anataka kuvuka mipaka.
Mama wa Mwanakwetu alikuwa mrembo sana, unatoka nyumbani kue;ekea kazini kutoka Mbagala hadi Mnazi Mmoja maneno dada kwema , unaitwa nani/ Unafanya kazi wapi ?
Hawa akina nani? Kama Ingekuwa leo hii mama wa Mwanakwetu angeomba sana namba ya simu.
Mwanakwetu kitendo cha kuona hawa wahuni wa Dar es Salaam wanatupa ndoano lilikuwa linamkera sana tena sana, hivyo uamuzi sahihi ni kuacha kuyasikia maneno hayo ni kwenda shuleni mwenyewe na kurudi mwenyewe, mama apite njia yake.”
Msomaji wangu jambo hili si la watoto wa kiume tu kwa mama zao bali hata kwa watoto wa kike kwa baba zao. Mabinti wakimuona baba yao anazongwazongwa na Mwanamke mwingine wanachukizwa sana na hilo.
Kwa hakika katika maisha yangu nikiwa mdogo hata kijana lipo jambo ambalo sikuhaingaika nalo saana nalo ni kuvaa, maana Mwanakwetu anao utajiri wa kuwa Wajomba wengi upande wa mama yake na Mashangazi wengi upande wa baba. Mama akienda kwa kaka zake anakutana na marobota ya nguo zilizoachwa na wajomba au zile Kafa Ulaya Mazishi Afrika-Mitumba.
Hili hata leo hii nikienda kwa Bibi Mzaa Mama -Mdala Elizabeth Mwimbwa sibebi nguo maana hadi kesho yapo masanduku ya chuma yenye nguo za wajomba zangu za kale, kwa hiyo nguo zipo na wajomba walishaondoka nyumbani kwa mama yao siku nyingi.
Msomaji wangu tambua Mwanakwetu Tajiri Wajomba Tajiri Shangazi.
“Mara chache mno Mwanakwetu nilinasa kuambatana na mama kwenda kununua nguo za sikukuu ile ya Pasaka au iwe Krisimasi. Hapo sasa Mwanakwetu anavumilia zile tabia za wahuni na wasumbufu wa Dar es Salaam
‘Dada unaitwa nani? Kila siku nakuona unapitia asubuhi na jioni ! Unafanya kazi wapi? ’
Sasa siku hizo mnazungnuka weee mitaa yote ya Karikoo, Agrey, Maxi Mbwana , Kongo. Uhuru, Sikuuu , Pemba na Lumumba. Tukiwa katika mizunguko hii kiu ya maji ilikuwa wajibu, sasa katika maduka mengi ya Dar es Salaam yalikuwa na mitungi ya maji na kikombe maji ya bure kwa wateja na wapiti njia.
Wakati mama anachagua nguo, nitungulie hiyo !Nitungulie ile ! Rangi hiyo siitaki! Mwanakwetu alikuwa anakimbilia mtungu wa maji anachota na kunywa. Maji haya yalikuwa yanatolewa bure na madaku haya mengi yalikuwa ya Wahindi na Waarabu. Kwa hiyo unakunywa maji kisha mama anakununulia nguo kwa ajili ya sikukuu husika.
Ukishanunuliwa nguo siku inayofuata hauambatani tena na mama yako.
Kumbuka tu Siyo Kila Ndoano Inayotoswa Ziwani Inaibuka Samaki lakini kwa ile ndoano iliyotoswa ziwani na kuibuka na samaki ndiyo maana akina Mwanakwetu wakazaliwa.”
Kisa cha Kati,
“Babu yangu Mzaa Baba Fidelis Makwega alikuwa analima huku Kisele, kwa utaratibu wa wakati huo hakukuwa na simu hivyo babu akiwa shambani kumpelelkea taarifa ya msiba, njia ilikuwa na kutumwa mapema ya siku hiyo kupanda basi kutoka Mtoni Mtongani hadi Kiparang’anda kisha kutembea kwa mguu kutoka Kiparang’anda hadi Kisele ukiwa ni mwendo karibu saa nzima. Unamkuta unampa taarifa kisha anabadilisha nguo mnarudi naye Mbagala.
Mwendo huu wa mguu wa saa nzima unapambana na kiu, ukiwa jirani ya nyumba unapiga hodi unasalimu wenyeji kisha unawaambia mie Mjukuu wa Mzee Makwega natoka Mbagala Dar es Salaam naenda kwa babu naomba maji ya kunywa. Anayeambiwa haya mara nyingi ni mabinti wadogo wanaolinda nyumba wakati wazazi wao wako mashambani anakuchotea maji katika kata na kukupa unywe.
‘Kata hizo zilikuwa za aina mbili mojawapo inakuwa ya kopo alafu inakuwa na mti wa kushikia au kata ya kifuu cha mnazi na ina mshikio wa fimbo ya mti’.
Binti Huyu Akija na Maji Anaanza kuyanywa Yeye Kisha Anakupa Wewe-maana yake maji haya ni salama kwake na salama kwako. Hapo Mwanakwetu anakunywa maji na kuendelea na safari.
Wakati wa kurudi na babu namwambia huu mji niliomba maji, Baba anajibu hawa Wandengereko, Hawa Wazaramo au hawa Wasukuma hawana shida. Babu na yeye anasema ngoja na mimi ninywe maji na kweli tunabisha hodi na kuomba maji tunakunywa kisha tunaendelea na safari na kufika Kiparang’anda na tunapanda gari Kuelekea Mbagala Msibani.”
Kisa cha Tatu
Mwanakwetu alikuwa na ndugu zake wawili ambao walikuwa viongozi wa Wazee Ngazi ya Mkoa wamekaa pahala fulani wanamgoja kiongozi mmoja afike, wakiwa hapo iliibuka hoja,
“Kwanini kwa sasa Tanzania imeupa kisogo uhamasishaji wa uvunaji wa maji ya mvua majumbani?”
Mama aliyekaa mkono wa kulia wa Mwanakwetu akasema,
“Sasa hivi ajenda kubwa ni ukusanyaji wa mapato, kwa hiyo ukihamasisha sana kuvuna maji ya mvua, hizo mita na bili majumbani zitapatikanaje?”
Maelezo ya mama huyu ambaye kwa kumtazama lazima awali alikuwa mtumishi wa serikali niliyaelewa sana huku mama huyu akiongeza na hili,
“Si unaona miundo mbinu hii, matenki haya yanabaki kukaliwa na mijusi tu, lakini kama yangeendelea kutumiwa ingeondoa gharama za watumiaji wa maji ya bomba.
Pia kuna hoja ya suala la usalama wa maji hayo lakini maji yana matumizi mengi, hata kumwagilia kwenye bustani kwa hiyo uvunaji wa maji ya mvua kwenye jumuiya na hata katika ya mtu mmoja mmoja ni jambo lazima siyo jambo la kukwepa”
Siku hiyo tukakifanya kilichotupeleka hapo, kisha kufungasha virago vyetu kurudi tulipotoka.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Katika visa vyote vitatu maji yametajwa kwanza Mitungi wa Maji madukani na pili kuomba maji safarini na kudolola hamasa ya uvunaji wa maji ya mvua Tanzania. Hivi visa vinayosimulia na Mwanakwetu kwa Tanzania ya leo hii haya mambo hayapo, maji ya kunywa yanauzwa katika chupa, kama hauna pesa maana yake utakunywa maji ya miferejini na utaugua matumbo na hata kununua kifo. Huku wapo wapo wanakusanya mabilioni ya pesa kuuza maji ya kunywa na kuwa matajiri kwa kitu ambacho hakipaswi kuuzwa na binadamu yoyote yule.
Mwanakwetu anaona kuwa katika hili kuna pahala Tanzania tumepotea njiani na lazima turudi katika msitari. Kama maji yanayopita katika mabomba si salama kwanini yasiwe salama na maji ya mtu binafsi kwenye chupa moja yawe salama? Hapo kuna pahala hapapo sawa.Au shida ya maji ya chupa tunakusanya kodi?
Ebu tuutazame mfano huu;
“Kama wanafunzi shuleni wanakunywa maji ya bomba, hawana nafasi ya kununua maji salama dukani, shule hiyo hiyo inapata nafasi ya wajumbe wa kamati ya elimu wanakuja kukagua mradi wa jengo, wajumbe wa kamati ya Bunge wakiitembelea shule hiyo hiyo wanakuja na chupa zao za maji safi na salama, walizonunua dukani.
Kwanini tumefikia hapo? Kwani tunajali usalama wa wachache na usalama wa wengi upo hatarini? Mbona zamani hali ilikuwa tofauti? Shida ipo wapi? Maji ndani ya mtungi dukani na hata nyumbani mwenye duka na mwenye nyumba anakunywa hayo hayo.”
Kesho mwenye Maji yake Mwenyeenzi Mungu akiuliza kwanini mlikuwa mnauza maji mtakuwa na majibu?
Kanisa Katoliki Ulimwenguni liliwahi kusema maneno haya,
“Watu wengi ulimwenguni hawapati maji safi na salama, kule Ufilipino tunanunua maji ya kunywa , tunanunua chupa ya maji ya kunywa, Je nyinyi hapa Marekani mnanunua ? Mmeshawahi kujiuliza kwanini tunanunua maji ya kunywa? Je kama hauna pesa ? Uhai wako unaupeleka mwenyewe mashakani. Naomba ngoja niishie hapa.”
Haya ni maelezo ya Kadinali Luis Antonie Tagle Mkuu wa Proapaganda Fide inajuhusosha na Uinjilishaji wa watu ndani ya Kanisa Katoliki Duniani.
Wapanga sera vipi? Wanasiasa vipi? Tanzania vipi? Kwa leo inatosha sana. Ngoja Niishie Hapa.
Mwanakwetu upo?
Je Makala yaitwaje? Kuelekea Mbagala Msibani, Tajiri Wajomba tajiri Shangazi au Ngoja Niishie Hapa.
Mwanakwetu anachagua, Ngoja Niishie Hapa.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment