Na Samson Kalekwa - Mwanza
Mwanakwetu, hebu tulisiane! Wakati huu wa majonzi kwa wale waliozoea utawala wa chama tawala, na wakati wa matumaini kwa wale waliochoka na "haki sawa kwa wote" kwenye makaratasi tu, swali moja limeanza kuvuma mitaani: "Nani atapeperusha bendera ya CHADEMA 2025?"
Hii si hadithi ya kubahatisha kama ramli za mpiga bao, bali ni simulizi linaloendelea kuandikwa kwa vitendo, kwa mikakati, na kwa mazungumzo ya faragha kwenye kumbi za vikao vya ndani. Mzee wa busara za mitaani kasema, "Kwenye siasa, usiseme hakuna, sema tusubiri!"
Jicho la wengi limewaelekeza watu wawili: Tundu Lissu na Freeman Mbowe.Lissu, mwenye lugha kali na hoja nzito kama kifaru wa vita, amekuwa alama ya mapambano ya haki na demokrasia. Amewahi kumiminwa risasi na bado anasimama, akihubiri mabadiliko kwa sauti isiyotikisika. Lakini Mwanakwetu, je, mazingira yanaruhusu? Viongozi wa chama chake wanajua kuwa jina lake peke yake ni mzigo wa vita, na si vita ya kampeni tu, bali hata ya kisheria na usalama.
Mbowe, jemedari wa chama, ndiye aliyeshikilia bendera hata pale upepo ulipovuma kwa nguvu ya kutisha. Ameweza kufanikisha siasa za CHADEMA ndani ya mfumo ambao wengi wangeukimbia. Lakini, je, ataingia tena uwanjani? Ama atabaki kuwa mpambanaji wa nyuma ya pazia, akisuka mipango ya kumleta kijana mwingine kwenye ulingo?
Je, Kijana Mpya Anaweza Kupenyezwa?
Mwanakwetu, kama kuna jambo siasa imetufundisha, ni kwamba si kila anayewaza kuwa rais hupewa fursa ya kugombea. Zitto Kabwe? Aliwahi kuwa mrithi wa CHADEMA kabla ya upepo kumbeba kwenda ACT-Wazalendo. Halima Mdee? Nyota yake ing'aa, lakini baada ya sakata la "maridhiano," bado hajarejea kwenye mstari wa wapinzani wa dhati.
Hii inaacha pengo: CHADEMA inahitaji mtu mpya, mwenye sura inayoweza kuvutia kizazi kipya, lakini pia mwenye mizizi ya chama na uwezo wa kupambana na mfumo uliopo.
Mwanakwetu, Hii Ndio Ngumu Kumeza
Ikiwa Lissu atakubaliwa kuwa mgombea, basi ni wazi kuwa uchaguzi utakuwa vita ya moja kwa moja. Ikiwa Mbowe atajitokeza, basi tutajua kuwa chama kimeamua kucheza karata ya usalama zaidi, kwa matumaini ya kupata washirika wa ndani na nje ya siasa. Na ikiwa jina jipya litatangazwa, basi Mwanakwetu, jiandae kwa mtikisiko!
Lakini kumbuka, siasa za Tanzania ni kama mchezo wa bao – aliyeshika kete za mwisho ndiye mwenye neno la mwisho. Uwanja bado upo wazi, lakini mteule wa CHADEMA atakapojulikana, historia ya siasa za nchi hii itakuwa imeshaandikwa kabla hata kura kupigwa.
Mwanakwetu Upoo!
Kumbuka tu, Mteule wa Urais CHADEMA ni ngumu kumeza.
samsonrichard511@gmail.com
0654653936
Post a Comment