Adeladius Makwega-MBAGALA
Mwaka 2015 nikiwa Mtayarishaji Vipindi wa TBC Taifa nikitayarisha ripoti mojawapo ya Kipindi cha Habari na Muziki cha Shirika hilo, kipindi kilichokuwa kinaruka hewani kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa Saa 12.00-1.00 Jioni, Fundi Mitambo wa TBC Taifa (tangu RTD) Isaya Odinga ambaye leo hii ni marehemu aliniambia jambo hili.
“Nyinyi mnafanya mahojiano na watu wengi wa mbali, na wakubwa wakubwa ambao mnadhani walishiriki kupigania uhuru, lakini mnatuacha siye tuliyofanya nao kazi kwa karibu mno wakati wa harakati hizo za ukombozi wa bara la Afrika na yapo mengi tunayoyafahamu kuliko hata hao akina Brigedia Hashimu Mbita, mengi hamuyatambui kabisa na hayapo hata katika maktaba yenu, bali yapo ndani ya mashuhuda ambao ni sisi.”
Jambo hilo lilinigusa sana, kwa hiyo na siku iliyofuata ambayo ilikuwa ni siku ya uhuru wa Msumbiji Juni 25, 2015 nilimuhoji Fundi Mitambo huyu Isaya Odinga ambaye alikuwa na ujamaa na mwanahabari marehemu Agolla Anduru.
Ndugu Odinga aliaza kwa kusema kuwa Wapigania Uhuru walitumia vizuri Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na External Service (ES) kama chombo cha kuwafikishia ujumbe ndugu zao waliokuwa katika mataifa yao kupitia Ampitude Modulation (AM) na Short Wave (SW).
Ndugu Odinga aliniambiwa kuwa kwa karibu wapigania uhuru wote walikuwa ni watu waliokuwa wakipambania haki zao, kwanza walianza katika mataifa yao na baadaye kuzihamishia harakati hizo katika mataifa mengine likiwamo Tanzania.
Wakiwa Tanzania walikuwa na changamoto kadhaa, kubwa lilikuwa ni matumizi ya lugha ambapo wengi walikuwa wakitumia lugha za kwao za asili na kidogo Kiingereza,. huku wengine waliweka juhudi za kuijfunza Kiswahili.
Fundi Mitambo huyu aliniambia kuwa kuna siku walikuwa wakirusha hewani kipindi kimojawapo chenye maudhui ya harakati za ukombozi na miongoni mwa waliopaswa kushiriki kipindi hicho ni aliyekuwa mpigania uhuru alichelewa kufika studioni.
Kipindi kilianza kwa waliowahi na ndugu huyu alipofika aliingia katika mlango wa studio husika na alipoambiwa matangazo yapo hewani alitaka kuingia kwa fujo. Wakati anataka kuingia alizuiliwa na walinzi wa RTD, jambo hilo lilileta mgogoro mkubwa baina ya mpigania uhuru huyo na watumishi wa RTD.
Huku mpigania uhuru huyu akiibua dhana kuwa kukatazwa kuingia studio kulikuwa ni kukwamisha harakati za ukombozi.
“Baadaye lilizungumzwa, mpigania uhuru kuelezwa utaratibu ulivyo wa studio na mwisho wa siku jambo hilo lilikaa sawa na dhana ya watumishi wa RTD ilieleweka kwa mpigania uhuru huyu kama walitakakukwamisha harakati za ukombozi iliondoka kichwani kwa mpigania uhuru huyo.”
Isaya Odinga ambaye alikuwa mtu mpole sana alimwambia Mwanakwetu kuwa haya anayosema hata Brigedia Hashimu hayafahamu.
Mzee Odinga alisema kuwa Mwanakwetu unataka nikupe jambo lingine, Mwanakwetu akajibu NAAAAM.
Fundi Mitambo Isaya Odinga akasema mwanangu Makwega sasa tutoke hapa studio nikupeleke uwanja wa mapambano. Mwanakwetu akauliza huko UWANJA WA MAPAMBANO TUNAFIKAJE AU NI HAPA JESHI LA WOKOVU?
Isaya Odinga akajibu akisema Bwana Mdogo Makwega hapana ninakupeleka kimawazo tu.
“Desturi za mapambano ya kupigania uhuru ilikuwa mataifa kadhaa yalijumuika katika kulikomboa taifa lingine kwa dhana ile ya mwalimu Julius Nyerere,-Tanzania haiwezi kuwa huru kama mataifa mengine ya Afrika yakiwa chini ya mikono ya mabeberu. Mataifa haya yalikuwa yanapigana kwa kusaidiana huku wale wanaosaidia wanajifunza mbinu za kijeshi ambazo zinawapa uzoefu kwenda kupambana katika taifa lao wakati ukifika.
Siku moja wapigania uhuru wa mataifa kadhaa wakiwa katika uwanja wa mapambano huko Msumbiji siku hiyo vita vilikuwa vigumu mno, kwani vikosi vya FRELIMO vilishambuliwa mno na kusababisha wanamgambo kadhaa kupoteza maisha.
Hali hii haikuwakatisha tamaa wapigania uhuru wa Msumbiji na wenzao katika uwanja wa vita, bali iliongeza ari ya vita kwa wachache waliosalia vitani waliokuwa mstari wa mbele.
Kiongozi mmojawapo katika vita hivyo akiwa na msaidizi wake waliomba msaada kwa wenzao waliokuwa nyuma ya uwanja wa vita baada ya kuwajulisha kilichotokea.
Ili kuwasubiri wenzao waje, waliamua kuingia katika handaki mojawapo ambalo lilikuwa kando ya uwanja wa vita. Walipoingia ndani ya handaki hilo walikubaliana kuwa kwa usalama wao kila mmoja aingia katika handaki lake.
Kwa hiyo msaidizi wa kiongozi huyo alitoka katika handaki nambari moja na kuingia handaki nambari mbili.
Hali ilizidi kuwa mbaya huku maadui waliporomosha risasi na mizinga mizito katika eneo hilo. Sasa wakakaribia eneo walipojificha ndugu hawa wawili.
Wakiwa katika eneo hilo, walisogelea msitu mdogo na walikutana na handaki la kwanza wakaingia na mienge na tochi humo alipojificha kiongozi wa wapigania uhuru na hawakuweza kuona chochote.
Walingia katika handaki la pili, kama kawaida kwa mienge na tochi, kwanza hawakuona kitu, walirudi tena handaki la kwanza hawakuona kirtu na wakarudi handaki la pili, ahmadi! walikutana na kigoda. Kigoda hicho ndicho kilikuwa kiti cha kiongozi wa wapigania uhuru akikalia wakati akizungumza na wapigania uhuru uwanja wa vita.
Kama unavyofahamu askari vitani wanakaa chini wakati wakipokea maelekezo, naye mkubwa anakaa katika kigoda ambacho kinaokotwa tu katika makazi ya watu baada ya watu kukimbia vita.
Kigoda hicho kilitoa picha kuwa hapo kuna watu, walikitoa nje na kuendelea kulikagua handaki hilo nambari mbili.
Kigoda hicho kikatoa ishara hapa yupo mtu na ilisababisha waingie nakumuona msaidizi wa kiongozi wa wapigania uhuru na kumtoa hadi nje ya handaki namba mbili. Kwa kuwa handaki namba mbili lilikuwa kwenye kichaka walimbeba na kumpeleka eneo la wazi kidogo jirani na handaki nambari moja ambalo alikuwemo kiongozi wa wapigania uhuru.
Walipofika hapo walimketisha katika kigoda msaidizi wa kiongozi wa wapigania uhuru na kuanza kumsulubu kwa kipigo, huku wakimkata kiungo kimoja hadi kingine, wakianzia na vidole, kiganja cha mkono na mabega ya upande mmoja na kisha upande mwingine. Wakaja vidole vya miguu, magoti na hadi mapaja walipomaliza waliamia ya upande mwingine.
Msaidizi huyu alilia bila ya kutaja alipojificha kiongozi huyu wa wapigania uhuru-huku akifahamu yupo katika handaki kando anaposulubiwa. Cha kusikitisha damu ya msaidizi huyu ilikuwa inatiririka kwenye kigoda na kushuka hadi ndani ya handaki ambalo ndani yake alikuwamo kiongozi huyo wa wapigania uhuru.
Zoezi hilo lilifanyika hadi msaidizi huyo kukata roho na wakauwacha mwili wake eneo hilo hilo na wao kuondoka zao.
Kiongozi wa wapigania uhuru alijificha hapo kwa siku kadhaa hadi walipofika kikosi kingine cha upande wao na kuuchukua mwili wa msaidizi huyo kwa maziko ya heshima zote na wao kuendelea na mapigano na mwishoni kushinda vita hivyo.
Baada ya vita hivyo, kiongozi huyo wa wapigania uhuru alirudi kwao na kuwa rais taifa lao hadi hii leo hii2015, narudi kusema kuwa kiongozi huyo ni rais wa taifa mojawapo la Afrika.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anasimuliwa na Fundi Mitambo Isaya Odinga, Ndugu akanitania tena akisema,
“Hao
mnaofungia safari wanaweza kuwambia haya?”
Mwanakwetu akajibu hapana.
Msomaji wangu Isaya Odinga sasa ni marehemu , haya Mwanakwetu anaambiwa mwaka 2015 na hata leo hii Kiongozi Yule aliyeponea Tundu la Sindani bado ni Rais wa Taifa Moja la Afrika.
Mwanakwetu anasema nini?
Msomaji wangu mara nyingi huwa tunakutana mitaani na Wanajeshi wakiwa katika magari yao au wakati mwingine wakitembea kwa miguu, huku sie tunaowatazama tunaweza kuvutiwa na mavazi yao, namna wanavyotembea kikamavu, nyimbo zao na hata magwaride yao. Mara nhingi sie tunawaotazama ndugu hawa tunawatazama kwa vitu vidogo lakini tunasahau kazi kubwa wanayoifanya kulinda taifa letu.
Unapoitazama kazi ya Jeshi ndiyo kazi pekee ya binadamu anapata ujira wako kumlinda nduguye huku akiwa na kiapo cha kuwa tayari kupoteza uhai, kwa hakika akitoka mwanajeshi anayefuata kwa heshima hiyo na anayefuata ni mama mzazi wa kila mwanadamu kwa hiyo JESHI lazima waheshimiwe sana.
Kulingana na https://dcas.dmdc.osd.mil/dcas/app/summaryData/deaths/byYearManner takwimu zinadokeza kuwa kwa mwaka 2019 watu 80,000 walifariki katika harakati za vita, mwaka 2005 watu 20,000, huku mwaka 1994 takwimu hizo zilitisha zaidi ambapo watu 800,000 walifariki na takwimu hizo zilipanda kwa sababu ya mauwaji ya KIMBALI.Takwimu zinagonga kengele ya hatari kuwa hapo nyuma huko Afghanstan, Pasiktan, Iraq , Yemeni na Syria watu milioni 4.5- 4.7 walifariki dunia kwa sababu ya vita.
Msomaji wangu kumbuka kuwa kila penye vita siyo vifo vyote vinatokana na vita bali zipo sababu zingine ikiwamo njaa maana jamii husika haiwezi kufanya shuhghuli zake hivyo watu wanaokimbia vita wanafariki kwa kukosa chakula na magonjwa na kadhalika.
Takwimu kwa taifa la Marekani pekee zinadokeza kuwa kwa mwaka 2022 walipoteza wanajeshi 844. Japokuwa vifo vyote hivyo lakini uwepo wa wanajeshi duniani unasaidia kupunguza hali ya vifo hivyo kama wanatumika vizuri lakini wakitumika vibaya nalo ni tatizo kubwa.
Katika kila siku inayokwenda kwa Mungu wanajeshi wetu katika mataifa yetu wanapambana kutulinda siye raia, katika hili wapo wanaopata majeraha ya kawaida, wapo wanaopata vilema va kudumu na wapo wanaofariki dunia huku wakiwaacha wake na waume zao ,na watoto yatima, huku hawa wakiwa mashujaa wa taifa husika na wakiungana na wale mashujaa wa vita vya Kagera na hata machifu waliopambana na ujio wa wageni ambapo Tanzania inasherehekewa SIKU YA MASHUJAA kila Julai 25.
Kwa heshima ya kumbukumbu hiyo kwa mwaka huu 2025 Mwanakwetu anatamani sherehe hii ifanyike kwa namna ya pekee na heshima zote.
Mwanakwetu anatamani kuona gwaride la maana hiyo na la heshima kwa roho kadhaa za wanajeshi wetu waliopambana na kufariki katika kulikomboa bara hili na hata wanaofariki wakilinda bara letu na Taifa letu la Tanzania.
Swali la kujiuliza ni Je damu ya msaidizi huyu wa wapigania uhuru inaweza kulipwa kwa nini? Je DHAHABU, ALMASI, MANE MANE , LULU, FEDHA au TANZANITE?
Mwanakwetu! Nakwambia hapo si Tanzanite, si Fedha, si Mane mane, si Lulu, si Almasi wala si Dhahabu inaweza kulipa damu ya msaidizi huyo wa Kiongozi Wapigania Uhuru.
Bali cha kufanya kwa kiongozi huyo ni kuhakikisha taifa lake linawasaidia wananchi wake bila ubaguzi na wanapate maendeleo katika nyanja zote na huko kutakuwa ni kulipa damu hiyo iliyopotea ya msaidizi huyu wa Kiongozi wa Wapigania Uhuru na wapiga uhuru wote waliopoteza uhai wao kulikomboa bara letu la Afrika. Hili ni hata kwetu Tanzania kukumbuka kuwa viongozi wetu watimize wajibu wao kuhakikisha shida za wananchi zinatatuliwa kwa wakati bila ubaguzi na uonevu wowote maana nchi hii wapo watu wengi wanapoteza uhaii kwa faida ya umma wa Watanzania maana Uanejeshi ni Talanta kubwa na mlipaji ni haki kwao ni Mungu pekee.
Mwanakwetu pia anatumia makala haya kuvikumbusha vyombo vingine vyote vya Ulinzi na Usalama Tanzania kuwa waadilifu kwa maslahi ya umma wa Watanzania maana sasa kumeibukua hali ya kutiliana mashaka.
Hapo hapa Mwanakwetu akakumbuka wimbo huu,
“Kuna kiwanja kimoja kiteule, Chakusimama watu wote, Kutoa kazi za kila mwanadamu, Alizopewa na mungu, Wengine watafukuzwa ondoka uhende, Sikujui sikujui mimi , kazi zako na talanda ulizopewa, ulizika Chini wewe×2, Watakuwa wakilia woiwoi,Tulifanya kazi za bure , Watakimbia huku na huku pia , Wakisaga menoyao.”
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Uanajeshi ni Talanta Kubwa”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment