ITAKUWA KIVUMBI NA JASHO

 

Lucas Masunzu- TABORA

Timu ya mpira wa miguu ya wasichana ya shule ya sekondari Urambo –Tabora imeichabanga bila huruma timu ya mpira wa miguu ya Shule ya Sekondari Mkangwa katika mchezo wa soka uliofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Urambo Aprili 2, 2025, ikiwa ni kuchuana kwa michezo ya UMISETA mwaka 2025.

Mchezo huo ulianza kwa halambe ya nguvu sawa kwa pande zote mbili. Mashambulizi ya pande zote yalikuwa yakifanyika lakini hakuna upande ulioweza kuliona goli la mwenzake. Mchezo huo uliendelea na katika dakika ya 26 kipindi cha kwanza Agnes Chole aliweka ndani ya goli bao la kwanza la shule ya sekondari Urambo baada ya kuwapiga chenga walinzi wa goli la Mkangwa akapata nafasi ya kupita na kuwanyuka bao hilo.

Goli hilo liliwaibua wanafunzi wa urambo kutoka katika kila pembe ya uwanja wa mpira kushangilia goli hilo huku wakirusha maneno ya tambo kama pongezi kwa Agnes Chole kwa kufungua ukurasa wa ushindi kwa timu yao. Shangwe ziliongezeka na kuwavuta kiwanjani wanafunzi na mashabiki hao wakauzunguka uwanja wa soka wa shule hiyo. Mchezo huo uliendelea, timu ya Mkangwa ikaongeza nguvu lakini haikuweza kusawazisha na dakika za kipindi cha kwanza zikamalizika.


 

Mchezo huo uliendelea baada ya kipindi cha pili kuanza, mabadiliko ya pande zote mbili yakafanyika kwa kuingiza wachezaji wapya ili kuimarisha ngome na mashambulizi kwa timu zote. Kunako dakika ya 15 ya kipindi hicho Halima Kihoza fowadi wa timu ya shule ya Sekondari Urambo alitupia bao la pili. Bila kupoteza dakika mwamuzi wa mpira mwalimu Kenyatta Sylivester alipuliza kipenga akaonesha ishara kuashiria mpira upelekwe katikati ya uwanja. Mashambulizi yakaanza tena.

Bila kurembaremba mchezaji Halima Kihoza alipokea tena mpira kutoka kwa mchezaji nambari 17 mgongoni uliopigwa kwa pasi ya kichwa, akauweka kifuani kisha akaushusha kwa umaridadi chini upande wa mguu wake na kushoto, akaanza mbio kuelekea kwa gorikipa wa timu ya Mkangwa. Pasipo huruma akaichabanga tena timu hiyo bao, likawa bao la tatu, akawa amebadili kabisa ubao wa matokeo ya mchezo huo. Hadi dakika ya mwisho mpira unamalizika, timu ya shule ya sekondari Urambo ikanyakua ushindi wa magoli 3 kwa 0.

Wakizungumza kwa njia ya simu na Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya wasichana ya Urambo sekondari mwalimu Maganga Lucas (Kaka Mrefu) alisema mechi ilikuwa kali huku akiendelea kunadi kuwa wachezaji wake amewafua vizuri hakuna wasiwasi watapeperusha bendera ya ushindi. Mwandishi wa ripoti hii akizungumza na mwakilishi wa timu ya shule ya sekondari Mkangwa akasema

 

“Mchezo uko hivyo, ni kweli tumeshindwa, wenzetu walikuwa kiwanja cha nyumbani, pamoja na kutuzidi nguvu, gorikipa wetu anakiwango kizuri amaeokoa mabao mengi”.

 

Akaendelea kusema

“sasa tunakwenda kujifua upya, tukikutana mzunguko wa pili wajiandae itakuwa kivumbi na jasho”.

 

Wakati mazungumzo hayo yakiendelelea, pembeni ya kiwanja hicho cha soka, Judith Gallus ameendelea kumpiga msasa wa kuendesha baiskeli Swaumu Rehani ambaye anashauku kubwa ya kujua kuendesha baiskeli. Angalau kwa sasa Swaumu anaunafuu, anaweza kuzungusha pedeli za baiskeli hatua kadhaa bila kuanguka lakini ni lazima awe ameshikiliwa.

Nakutakia siku njema, Kwa heri.

 theheroluke23@gmail.com

 0762665595











 

 

0/Post a Comment/Comments