Adeladius Makwega MBAGALA
Nilipanda bodaboda ya kunipeleka bandarini Zanzibar, niliposhuka nilimkabidhi shilingi 5000 na yeye kunirejeshea 3000, nikaondoka kuelekea bandarini, kijana huyu aliniita kwa nguvu huku akinikimbilia, akiniambia mzee, mzee, mzee ! unaenda na Helmet yangu. Hapo na mimi ndipo nilishituka kuwa nimevaa kofia hiyo.
“Mara nyingi sana, huwa tunapoteza kofia hizo, mimi nilishapoteza kofia tano tangu Januari mwaka jana hadi sasa.”
Nikamwambia pole na hata mimi nilikuwa sikumbuki kama nilikuwa nimevalia Helmet hiyo. Mara ya mwisho kuvaa Helmet ilikuwa Julai 2020 huko Mahenge Ulanga. Kisha niliivua Helmet hii na kumpa.
Niliingia katika geti la Bandari ikiwa ni saa 9.43 Alasiri, nilionesha tiketi yangu kwa wakala wa kampuni ya Azam Marine, alipokea na kuitazama, alafu akaniambia muda bado na boti haijafika, ingia hapo ndani ukapumzike, kusubiri boti kutia nanga.
Nilitekeleza hilo na kuingia katika chumba hiki, nilipokelewa na ndugu mmoja ambaye alionekana anazungumza lugha zaidi ya nne, maana mbele yangu kulikuwa na wasafiri waliozungumza Kiarabu alijibu, Kingereza alijibu, Kiswahili alijibu na hata Kijerumani nilisikia pia alijibu.
Alinisogelea na kuitazama tiketi yangu na kuniambia kuwa mzee hapa abiria wenye tiketi kama yako huwa hawaingii, wanaoingia ni wale wa Business Class na VIP class tu.Mwanakwetu nikapatwa na bumbuwazi.
Kochi jirani na mimi kulikuwa na watu wakacheka. Nilitoka nje kimya kimya, nakusoma pale mlangoni kusoma kuna maneno gani? Hapo paliandikwa
“VIP LOUNGE/ CHUMBA CHA VIP. Maana ya VIP ni Very Important Person (VIP).”
Nikasema moyoni,
“Kutokata kwangu tiketi ya 35,000/- au ile ya 60,000-80,000/-ndiyo nimepokonywa heshima yangu ya kuwa mtu muhimu?”
Nilikumbuka mbali enzi zangu wakati najifunza habari za CCM na elimu kwa wanachama wapya, ubaya wa ubaguzi na namna wenzetu wa Afrika ya Kusini walivyokuwa wakibaguliwa kutokana na rangi zao. Wakikatazwa kuingia baadhi ya maeneo ya starehe lakini leo hii mimi nimebaguliwa kutokana na kipato changu. Nilimkumbuka marehemu Ramadhani Nyamka aliyekuwa kiongozi wa CCM wakati huo katika mkoa wetu, Mungu amrehemu aliyetufundisha ubaya wa ubaguzi, miaka karibu 60 ya uhuru Mwanakwetu anabaguliwa.
Nikiwa nje, nilijiuliza ilikuwaje yule jamaa wa Azam aliyeniona getini alinielekeza kwenda katika chumba hicho cha VIP au kwa kuwa nilivalia suti yangu ya rangi ya samawati? Nilijisikia mnyonge sana. Nikasema VIP si suti bali VIP ni pesa.
Nikiwa nje, nilimuomba jamaa wa VIP nijifunze zaidi juu ya VIP LOUNGE, jamaa huyu aliniruhusu lakini akisema ,
“Kwa leo nakupa ofa tu ya kupigwa na viyoyozi lakini hautopata ruhusa na kunywa chochote humu ndani.”
Nikasema nashukuru kwa hisani yako hiyo, angalau na mimi nikawasimulie makabwela wenzangu habari za VIP LOUNGE, wale jamaa waliokuwa jirani na mle ndani walionicheka awali waliendelea kunicheka tena. Jamaa wa VIP Alichukua tiketi yangu na kukikata kishungi na kukichukua kipande kimoja na mimi kubaki na sehemu nyingine.
Nikiwa mle ndani, nilibaini kweli kulikuwa na watu kutoka mataifa tofauti wakichukua vinywaji hivyo, wengine kahawa, wengine juisi, wengine soda wao na familia zao, huku mie udenda ukinitoka.
Mandhari ya VIP LOUNGE ilikuwa ,
“Makochi ya ngozi 48, meza 18 na katika samani hizo kulikuwa na sehemu za kukaa watu sita sita samani zilizo katika mzunguko zikijaza chumba hiki kilicho kama bweni la shule na kila sehemu hiyo ilikuwa na meza tatu. Makochi haya nane ambayo yalikuwa katika mizunguko hiyo sita, mzunguko mmoja ulikuwa na makochi ya watu watatu mawili, makochi ya watu wawili (Love seat-Bibi &Bwana) kiti kimoja na makochi ya mtu mmoja mmoja matano, jumla ya makochi yote ndiyo hayo nane.Nilibaini kuwa katika mizunguko sita mzunguko mmoja wanaweza kukaa watu 14 jumla ya watu hao watakuwa 84 hapo ni sawa na madarasa mawili.”
Kwa hesabu yangu nilibaini kuwa watu waliokuwemo humo hawakuzidi 29 ambayo ni nakisi (tofauti) ya watu 55. Hata kama boti nzima waliopanda Dar es Salaam wakiingia humo kukaa na kusimama wangetosha.
Boti iliwasili na mimikuingia botini ili kurudi zangu Dar es Salaam.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Nikiwa botini nilibaini kuwa Sultani Jamshidi Bi Abdulla wakati huo alikuwa hajafariki sasa amefariki, wakati huo alikuwa na miaka 92 akiishi huko Omani. Wakati Afro Shirazi Party ya Abeid Karume iliyoungana na TANU na kuunda CCM wakati hawa ASP inadai uhuru walitoa fasili ya uhuru.
“Kuondoa Unyonge, Kuondoa Dhuluma, Kuondoa Shida, Kuondoa Kuogopana na Kuondoa Mengine Mengi.”
Natambua Sultani Jamshidi akiwa hai aliyaogopa mapinduzi matukufu ya Zanzibar ambayo tunayasherekea kila mwaka, jamani jamania jamania tunatakiwa kujitahidi mno kuonesha kuwa sasa tu huru, madhaifu madogo madogo yote yafanyiwe kazi.
Miaka 60 na ushehe ya Mapinduzi bado tuna VIP LOUNGE/CHUMBA CHA VIP? Binafsi kwa ukweli wa Mungu nilikuwa mnyonge kutokana na tukio hilo na huku ni kuitusi fasili ya maana ya uhuru kama alivyosema Shekhe Abeid Amani Karume.
Yale yale yaliyolalamikiwa sasa yanarudi je nia ya kudai uhuru ilikuwa ni kuwaondoa wale kwa wasababu ni Wazungu? Kwa hoja Uhindi wao ? Kwa Uwarabu wao?Au Kwa wao ni chotara? Kama ilikuwa ubaya wa matendo yao na sisi tutafanana na wao hivi punde lazima tujirekebishe,Ubaya wa haya mambo yakisemwa unaweza kuona kama ni kichekesho, kama utani vile kama dhihaka lakini na hata Wakoloni walikuwa na mtazamo huo huo, kumbuka Mwanakidonda Mjukuu ni Kovu.
Mwisho, niwaombe ndugu zangu wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuwa katika kila pahala palipoandikwa VIP LOUNGE tafsiri yake imeandikwa CHUMBA CHA VIP ningeomba iandikwe CHUMBA CHA WATU MUHIMU kwa kufanya hivyo tutajitambua kuwa siye siyo watu muhimu.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
Je makala haya yaitwahe?Chumba Cha Watu Muhimu. Safari yangu ya Zanzibar, Hata wakolini waliona hivyo hivyo au Mwana Kidonda Mjukuu Kovu?
Mwanakwetu anachagua Mwana Kidonda Mjukuu Kovu
Nakutakia siku Njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment