Julai 16, 2020 mwanahabari wa Shirikia la Utangazaji la Ujerumani DW Veronika Natali aliripoti;
“Mahakama ya haki za binadamu ya Afrika imeitaka serikali ya Tanzania kurekebisha baadhi ya vipengele vya katiba ya taifa hilo vinavyozuia matokeo ya urais kupingwa mahakamani, kufuatia kesi iliofunguliwa na mwanasheria. Baada ya uamuzi wa mahakama hiyo, baadhi ya wachambuzi wa haki za binadamu wanasema kuna mashaka ya utekelezwaji wa agizo hilo kwa kuwa Tanzania ilishatangaza kujitoa katika mahakama hiyo inayoshughulika na haki za binadamu.
Huku Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 41 kifungu kidogo cha saba kinaeleza kuwa baada ya matokea ya rais yaliyotokana na uchaguzi mkuu kutangazwa na tume ya uchaguzi, matokeo hayo hayawezi kuhojiwa mahakamani.
Msimamo huo unakiuka ibara ya pili na ya saba kifungu kidogo cha kwanza cha mahakama ya haki ya Afrika, ambacho kinaeleza kuwa endapo mtu hatoridhika na matokeo hayo ya urais, anahaki ya kukata rufaa. Kesi hiyo ilifunguliwa na wakili Jebra Kambole wa Tanzania akitaka vifungu hivyo vilivyopo katika katiba vibadilishwe kwani vinakiuka haki za kisheria za binadamu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zilizotangaza kujitoa katika mahakama hiyo, nchi zingine ni Rwanda, Benin na Cote d'lvoire iliyotoa maamuzi hayo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huo wa 2020. Hata hivyo mahakama hiyo inasema kujiondoa kwa nchi hizo katika mahakama ya Afrika hakuzuii nchi hizo kutekeleza na kulinda haki za binadamu.
Dr. Robert Eno, msajili wa mahakama ya Afrika na haki za binadamu, alisema nchi zote nne zilizojitoa zimeeleza wajibu wa kulinda haki za binadamu na kuendelea kutekeleza mkataba wa haki za binadamu.‘Nchi tatu kati ya hizo majaji wake walikuwa majaji wa mahakama hii ya haki za binadamu, hata Rais wa mahakama hii wakati huo alitoka Cod'lvoir, kwa hiyo siwezi kusema kwamba wanakimbia majukumu ya kulinda haki za binadamu,’ alisema Dr Eno. Kenya na Malawi ni nchi ambazo zilipinga matokeo ya urais waliyotangazwa katika nchi zao jambo ambalo watetezi wa haki za binadamu wanasema ni ukuaji wa demokrasia na ulinzi wa haki za binadamu.”
Maelezo ya Ibara ya 41,7 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanasema;
“Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”
Historia ya Tume ya taifa ya Uchaguzi ya Tanzania inadokeza haya;
“Mwaka 1991 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi aliteua Tume ya kwanza chini ya Uenyekiti wa Marehemu Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali Madhumuni ya Tume hii ilikuwa kukusanya maoni ya wananchi juu ya kuendelea na mfumo wa chama kimoja au kuwa na mfumo wa vyama vingi. Kutokana na ushauri wa Tume ya Nyalali ,Sura ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ilirekebishwa na kufanya Tanzania kuwa Taifa linalofuata mfumo wa Vyama vingi vya Siasa.
Sheria ya Vyama vya siasa, (Na. 5 ya 1992) ilirekebishwa ili kuwezesha kuandikishwa kwa vyama vya siasa. Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,(Na.1 ya 1985), Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa,(Na. 4 ya 1979) na sheria zinazoendana pia zilirekebishwa ili kuondokana na matakwa ya chama kimoja na kuruhusu mchakato wa Kufanyika kwa Uchaguzi chini ya Mfumo wa vyama vingi vya siasa. Mwaka1993 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilianzishwa chini ya Ibara ya 74 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Wajumbe wa Tume waliteuliwa kwa mara ya kwanza tarehe Januari 14,1993.”
Tangu mwaka 1993 Tanzania imefanya uchaguzi mkuu mara kadhaa; 1995, 2000, 2005, 2010, 2015, 2020 na pengine mwaka wa 2025 ikawa mara ya saba, yaani karibu miaka 35 na kwa kipindi chote hiki uteuzi wa wenyeviti wa tume ya uchaguzi umekuwa ukiwadondokea majaji kutoka mahakama Kuu , Mahakama ya Rufaa au wale walistaafu. Kikubwa ni Watanzania waliowahi kukaa katika kuta za mahakama kushughulikia masuala ya sheria. Ndiyo kusema majaji hao wanakwenda kusimamia jambo ambalo mahakama haina mamlaka ya kuhoji.
Ndiyo kusema katiba inazuia kabisa jambo hili kugusa kuta za mahakama lakini watendaji wake katika tume wanatoka mahakamani na wanayo haki ya kuweka mikono yao katika jambo hilo lisilohojiwa na mahakama.
Jambo hili tayari lilishafanyiwaa kazi na Tume ya Jaji Warioba ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2013 ambapo ibara ya 78 1 inanadi haya;
“Kwa kuzingatia masharti ya Ibara ndogo ya (2), endapo mtu yeyote aliyeshiriki kama mgombea nafasi ya madaraka ya Rais katika Uchaguzi wa Rais hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo, anaweza kuwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo wa Rais yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi.”
Jaji Warioba na wenzake walikwenda mbali zaidi kwa kulifafanua jambo hili kuwa na ibara nzima na ibara ndogo tano, wakati sasa jambo hili lipo katika ibara ndogo tu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Hoja hii nyepesi sana kutoka katika hukumu ile ya mahakama kama alivyoripoti VeronikaNnatalis wa DW hatuna budi tuubebe mzigo huu na tuutue kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilivyosema .
Tupewe katiba mpya ili kuondoa malalamiko yasiyo na tija jamii ya Watanzania ishuhgulikie na mambo ya maendeleo na hili suala la Katiba Mpya tulifunge ukurasa wake.
Mwanakwetu upo/
“Suluhu Katiba Mpya.”
Nakutakia siku njema,
0717649257
Post a Comment